Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wananchi wasiwaonee aibu watendaji wote wabadhirifu

13th May 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Mwishoni mwa wiki hii, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewataka wananchi kuwafichua na kuwataja kwa majina mawaziri pamoja na watendaji wa serikali watakaozembea kwa kushindwa kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma.

PM Pinda alitoa wito huo akiwa jijini Mbeya wakati wa sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru zilizoenda sambamba na kampeni ya kitaifa ya sensa.

Waziri Mkuu alisema haileti maana nzuri ikiwa wananchi watawaangalia na kuwaacha mawaziri wakiharibu uchumi wa nchi, akasema badala yake wananchi wanastahili kuwashtaki hadharani mapema ili wachukuliwe hatua kabla hawajaliingiza taifa katika hatari. Alisema wananchi wakiwajibika kwa uadilifu vizuri katika hilo, kutaleta utamaduni mpya wa matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji zaidi.

Zipo dalili nzuri na za wazi za uwajibikaji wa mawaziri waliotangazwa hivi karibuni, tumewasikia kupitia vyombo vya habari namna walivyojipanga kutekeleza majukumu yao na hasa katika kusimamia matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali wanayoisimamia.

Ni vyema sasa tukawapa muda na wananchi tukatathmini jitihada zao, na pia wakati wote wananchi watoe ushirikiano mkubwa wakati wa utekelezwaji wa miradi ya maendeleo wanayoisimamia.

Wito wa Waziri Mkuu wa kutoa taarifa zozote za ubadhirifu wa fedha za umma una nia njema ya kuhusisha kada zote katika kuhakikisha kuwa mali ya umma inatumika bila kuwepo na ubadhirifu, anawahusisha wananchi wote kutokana na ukweli kuwa fedha zote zinazotumika na wizara kwa kazi zozote, zinatokana na jasho la wananchi wote ambao ni wakulima pamoja na wafanyakazi.

Alisisitiza kuwa wananchi wasisubiri watendaji wachache hao wanaoshindwa kusimamia fedha na mali za umma wakaendelea na tabia chafu hizo, badala yake alisema inatakiwa wananchi washiriki katika kuwaumbua kwa kuwataja mapema ili kurejesha nidhamu katika utendaji.

Waziri Mkuu anajua wazi kuwa baadhi ya ubadhirifu wa fedha za umma unaofanywa na watendaji wa serikali, unafanyika kwa uwazi mbele ya wananchi, ambao sasa wamepewa fursa ya kuyasema waziwazi kwa mamlaka husika.

Katika kutekeleza hayo, angalizo linakuwepo la kutotoa taarifa zisizo sahihi zenye malengo ya kukomoana pamoja na kuharibiana sifa za utendaji, kinachotegemewa sana na serikali kutoka kwa wananchi ni taarifa za kweli ambazo zina vielelezo sahihi vya namna ulaji na ubadhirifu wa fedha za umma unavyofanyika, fursa hii iliyotolewa na Waziri Mkuu isitumike kwa nia mbaya ya kutaka kuwaharibia baadhi ya viongozi waadilifu kwa vigezo vyovyote.

Tunaungana na Waziri Mkuu kwa maagizo aliyoyatoa, inawezekana sasa wananchi nao wakawa sehemu ya uratibu wa maendeleo ya kweli ya nchi yetu, wakishirikiana vyema na serikali wataifikisha miradi yote ya maendeleo katika kilele bila fedha yoyote kutumika kinyume na maazimio yaliyokusudiwa.

Tunaamini kuwa serikali inawathamini wananchi wake kwa kuwahusisha katika usimamizi wa fedha za umma, na ni imani yetu kuwa wananchi nao watafanya yawapasayo kwa umakini ili taifa kwa ujumla linufaike na raslimali zake kadri ya mipango itakavyokuwa imeainishwa na serikali yenyewe.

Tunaamini pia wananchi watashiriki ipasavyo katika kutoa taarifa zitakazosaidia kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.Hakuna sababu ya kuwaonea aibu watendaji wote wabadhirifu wa mali za umma.

Mabilioni ya fedha zilizotangazwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa serikali katika ukaguzi alioufanya katika wizara mbalimbali hivi karibuni, sasa iwe ni historia kwani ushiriki wa wananchi katika kuwataja watendaji wanaoonekana kufuja fedha za umma utasaidia kwa kiwango kikubwa kurejesha nidhamu na maadili kwa watendaji wa ngazi zote serikalini.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles