Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Dk. Mengi awaasa wahitimu Vyuo Vikuu kuwakwepa mafisadi na wala rushwa

20th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk Reginald Mengi akizungumza katika sherehe ya Siku ya Wanafunzi iliyofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi juzi.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, amewataka wanafunzi wanaohitimu Vyuo Vikuu nchini wanapoingia kwenye mchakato wa kutafuta kazi kutokubali kutumiwa na mafisadi na wala rushwa ili kujipatia fedha na utajiri wa haraka.

Wametakiwa kuwa na macho yenye kuona fursa mbalimbali zilizopo na kuzitumia kikamilifu kujiletea maendeleo ikiwemo kujiajiri wenyewe pamoja na kutojiunga katika makundi ya ufisadi na ulafi wa mali za umma.

Dk. Mengi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya taaluma iliyofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS) jana, na kuandaliwa na wanafunzi wa Chuo hicho kwa kushirikiana na uongozi wa Chuo, alisema katika kutafuta ajira vijana wengi huenda kwa kasi kubwa na kutaka kuanza kazi na kupata utajiri wa haraka, matokeo yake wengi kutumbukia katika kazi zisizostahili, na kutumiwa na mafisadi na wala rushwa.

“Msikubali kutumiwa kwa kutaka utajiri na pesa za haraka, hata vitabu vitakatifu imeandikwa kuwa kila mtu atakula kwa jasho lake, fanyeni kazi ambayo watu watajivunia na hata Mungu hufurahia…Tanzania ina fursa nyingi sana ili kuziona vijana mnatakiwa kuwa na macho yanayoona fursa zilizopo,” alisema.

Alisema vijana wengi mara baada ya kumaliza elimu ya juu, hufikiria kuwa baada ya kupata ajira watapata fedha nyingi za kuwawezesha kununua magari, nyumba na mambo mengine kwa kuishi maisha ya starehe, bila kuwa na malengo ya kufika mbali ikiwemo kujiajiri.

Dk. Mengi alisema wapo wanaodhani kuwa ukishakuwa na fedha nyingi na utajiri hakuna haja ya kuwa karibu na Mungu, jambo ambalo si kweli kwani bila kumtegemea Mungu hakuna kitakachofanikiwa hivyo ili kufikia mafanikio ni lazima kuwa karibu na Mungu na kumtegemea yeye.

Aidha, alisema vijana wengi wanakosa ajira kutokana na kushindwa kuwasiliana tangu wanavyoandika barua za kuomba ajira, ambapo lugha huwa si ya kueleweka huku wakikosa kujiamini.

“Unapoitwa kwenye usaili kwanza unatakiwa uonyeshe kujiamini, ongea kwa kujiamini na kuangalia watu wanaokufanyia usaili kwa kujiamini, onyesha uwezo wako katika kazi, wengi mkishakuwa na vyeti vizuri mnaamini ndio mtapata kazi, wasichana nao huishia kujiumauma na kutaka huruma bila kuonyesha iwapo wataajiriwa watafanyaje kazi” alisema.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Faustin Bee, alisema miongoni mwa kozi nyingi zinazotolewa na chuo hicho ipo kozi ya ujasiriamali, ambapo wanafunzi huandaliwa kwa ajili ya kujiajiri badala ya kujijenga katika kuajiriwa pekee na kwamba wengi wao wanaomaliza kozi hiyo hufanya kazi za ujasiriamali.

Alisema siku zote Tanzania haiwezi kupiga hatua kimaendeleo kwa kuendelezwa na watu walio nje ya nchi, bali na Watanzania wenyewe kwa kufanya kazi, kwa kujituma, uwajibikaji, uaminifu na uadilifu thabiti na bila kufanya hivyo tutabaki kuwa ombaomba.

Naye, Afisa Mikopo wa Benki ya CRDB, Tawi la Moshi, Petro Chilato, alisema ili kupata kazi nzuri ni lazima unapoitwa kwenye usaili kuonyesha ukweli wa kile kinachoonekana kwenye vyeti ulivyopata, kwani wengi wana vyeti vizuri lakini wanashindwa kujieleza na kuonyesha uwezo wa kazi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles