Saturday May 25, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mauaji Kanumba: Rundo la askari lamzingira Lulu kortini

24th April 2012
Print
Comments
Msanii wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, akisindikizwa na askari Magereza kuelekea chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana. (PICHA: KHALFAN SAID)

Hatimaye msanii wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ (18), amepata jopo la mawakili watatu, Kennedy Fungamtama, Fuljensi Massawe na Peter Kibatala, watakaomtetea dhidi ya kesi inayomkabili ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven  Kanumba (28).

Kesi hiyo ilitajwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo, baada ya Hakimu Augustina Mmbando aliyepangiwa kusikiliza usikilizwaji wa awali kuwa na udhuru wa kikazi.

Wakili Fungamtama alidai kuwa, mawakili watatu Massawe na Kibatala watamuwakilisha mshtakiwa huyo katika kesi hiyo.

Aidha, Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na aliomba tarehe ya kutajwa.

Hakimu Tarimo alisema kesi hiyo itatajwa Mei 7, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Kabla ya kuahirishwa kesi hiyo, kulitokea mtafaruku mkubwa kati ya askari magereza na waandishi wa habari waliotaka kumpiga picha msanii huyo.

Hata hivyo, kutokana na kundi la askari hao zaidi ya 15 kumzunguka ‘Lulu’, hali ilikuwa ngumu kwa wapiga picha hali iliyosababisha mabishano makali baina yao na askari na kusababisha mshtakiwa huyo kuangua kilio wakati akiingizwa kwenye chumba cha mahakama.

Katika kesi hiyo, ‘Lulu’ anadaiwa kuwa, Aprili 7, mwaka huu, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, alimuua Kanumba.

Aidha, kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Lulu hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusikiliza kesi za mauaji, lakini mara upelelezi wake utakapokamilika itahamishiwa Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

HALI ILIVYOKUWA JANA

Saa 3:45 asubuhi, Lulu akiwa amevaa gauni kubwa na ushungi wa rangi ya hudhurungi (zambarau) na viatu vyeusi,  aliingia kwenye chumba cha mahakama huku akilia kutokana na msongamano mkubwa wa askari Magereza na Polisi waliokuwa wamemzunguka kumfikisha mahakamani.

Baada ya dakika tano kupita na mshtakiwa huyo kutulia, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na waliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mshtakiwa huyo pamoja na kundi la askari wa Magereza wanawake, aliingia kwenye viunga vya Mahakama hiyo akiwa kwenye basi dogo la Magereza lenye namba za usajili STK 4310 aina ya Isuzu ya rangi ya kijana huku akiwa amesindikizwa na basi jingine dogo lanye namba za usajili STK 3057 aina ya Nissan ya rangi nyeupe.

Magari hayo yaliingia mahakamani hapo kwa kasi hadi sehemu ya mahabusu kwa ajili ya mshtakiwa kusubiri kusomewa mashtaka dhidi yake.

Aprili 11, mwaka huu mshtakiwa huyo wakati akisomewa hati ya mashtaka, alidai mahakamani hapo kwamba umri wake siyo miaka (18) kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka bali ana miaka (17).

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment