Sunday May 26, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Wachezaji kikapu kufundwa

26th April 2012
Print
Comments

 

Wachezaji mbalimbali wa mchezo wa kikapu kutoka katika taasisi ya Andy1 ya Marekani wamekuja nchini kwa ajili ya kufanya ziara ya kutoa mafunzo kwa wachezaji chipukizi wa hapa nchini yenye lengo la kuinua vipaji vyao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Coca Cola, Evans Mlelwa, ambao ndio wamedhamini ujio wa wachezaji hao alisema kuwa lengo ni kuendeleza vipaji vya wachezaji wa Kitanzania ili waweze kuzitumikia klabu zao na baadaye kupata nafasi kwenye timu za nje.

Mlelwa alisema kuwa kliniki zitakazosimamiwa na wachezaji hao zimeandaliwa ili kuongeza hamasa ya mchezo huo na ni mpango endelevu ambao ulianza kufanyika nchini tangu mwaka juzi. Aliitaja mikoa itakayonufaika na programu hiyo kuwa ni Mwanza ambapo itafanyika Aprili 27 mwaka huu na kufuatiwa na Mbeya, Dodoma, Arusha, Moshi mkoani Kilimanjaro na ya mwisho itakuwa ni jijini Dar es Salaam.

"Tunatambua changamoto ambazo zinapatikana katika kuinua mchezo huu na ndio maana mwaka jana Coca Cola tulisaidia kuboresha baadhi ya viwanja maarufu vinavyotumika katika mchezo huu wa kikapu nchini," aliongeza Mlelwa.

Mmoja wa wakufunzi hao ambao huko Marekani ni maarufu kwa kucheza 'Street Basketball', Dennis Chism, alisema wanaamini kuwa wachezaji watakaojitokeza kushiriki kwenye mafunzo hayo watanufaika katika kusaidia kuinua viwango vyao na kuwataka kuviendeleza kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara.

Wachezaji wa umri wowote wanaruhusiwa kujitokeza kushiriki katika kliniki zote zitakazofanyika katika mikoa hiyo sita ya nchini.

Makamu mwenyekiti wa shirikisho la mchezo huo nchini (TBF), Phares Magesa, aliishukuru Coca Cola kwa kuendelea kusaidia maendeleo ya mchezo huo na kuwataka wadau wengine wajitokeze kusaidia michezo.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment