


Watu wasiojulikana wamevunja na kuingia katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya kwa lengo la kutafuta nyaraka za siri.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Clemence Kasonga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita na kwamba hakuna kitu kilichoibwa.
Watu hao waliingia katika ofisi za mkaguzi wa ndani, wahasibu wasaidizi, masjala ya wazi, mraribu wa vizazi na vifo, mshauri wa mgambo na ya mwandishi wa vikao vya halmashauri na kutawanya nyaraka hizo hovyo.
Baadhi ya watumishi wamesema watu hao hawakuwa na lengo la kuiba fedha bali nyaraka za siri.
Walisema walivunja kabati na droo za ofisi hizo katika haraka za kutafuta nyaraka walizokuwa wakizitafuta.
Hivi karibuni wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya (DCC) wajumbe waliwatupia lawama viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Mamlaka ya Mji wa Kyela kutokana na utaratibu ulioanzisha wa kutowachukulia hatua za kisheria watendaji wanaobainika kufuja mamilioni ya fedha, badala yake wanaambiwa wazirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katibu wa NCCR-Mageuzi Wilaya ya Kyela, Widley Mwasyeka, akizungumza katika mkutno huo, alitoa mfano wa Afisa Afya wa Mamlaka ya Mji wa Kyela, Omari Mbalawa, ambaye alikuwa akituhumiwa kula fedha za soko alizokusanya zaidi ya Sh. milioni 4. Alisema katika hali ya kushangaza badala ya yo kuchukuliwa hatua za kisheria suala hilo lilipofikishwa polisi, uongozi wa halmashauri na mamlaka ukaamua azirejeshe fedha hizo.
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Abdallak Kihato (sasa Maswa), ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, alisema utaratibu huo haupo kisheria na kwamba kilichofanyika ni kulindana, jambo ambalo haliwezi kukubalika.
Katika sakata hilo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka, Fredy Mwaigombe na Mweka Hazina wa Mamlaka, Mwakitalu, walitoa maelezo tofauti ya kujichanganya hali iliyomlazimu Kihato kuuamuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Mamlaka ya Mji wa Kyela kumpa maelezo ya kina ndani ya wiki moja ili hatua zichukuliwe.