Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Vijana wapinga tarehe ya Nchunga Yanga

13th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga

Vijana wa Yanga jana walipinga tarehe ya mkutano mkuu wa klabu hiyo iliyotangazwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga juzi - Julai 15.

Nchunga aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa mkutano mkuu wa klabu hiyo utafanyika Julai 15 jijini Dar es Salaam.

Lakini akizungumza na NIPASHE jumapili jana, Mwenyekiti wa vijana wa klabu hiyo, Bakili Makele alisema vijana hawakubaliani tarehe hiyo ya mbali wakati mwenyekiti huyo ana uwezo wa kuitisha mkutano huo ndani ya siku 30.

"Nchunga ameshindwa kuangalia hali ya klabu ilivyo sasa," alisema Makele.

"Tulidhani angetumia busara kuitisha mkutano mapema ili kuiweka klabu katika mazingira mazuri lakini yeye kwa sababu zake binafsi ameamua kupeleka mkutano mkuu mpaka mwezi Julai.’’

"Kuna haja gani ya kupeleka mkutano mbali kote huko."

Hata hivyo katika maelezo yake ya juzi wakati akitangaza tarehe ya mkutano mkuu, Nchunga alisema kuwa sio kazi rahisi kuandaa mkutano mkuu.

Alisema ugumu huo ndio sababu iliyoifanya kamati ya utendaji kujipa siku 65 ili kukamilisha maandalizi yote muhimu ya mkutano huo.

Lakini Makele alidai Nchunga amepeleka mkutano huo mbali ili kujitengenezea mazingira ya kusimamia mapato wakati wa mashindano ya Kombe la Kagame, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, yanayotegemewa kuanza mwezi ujao jijini.

"Nchunga ameona kuna mashindano ya Kagame... sasa kaona akiitisha mkutano mapema kabla ya mashindano haya hatopata nafasi ya kuisimamia timu huko kwa hiyo anasubiri mashindano yapite," alisema Makele.

Aidha, Mekele alisema katika hali ya kawaida Julai ni mwezi wa maandalizi ya klabu kwa ajili ya ushiriki wa ligi kuu ya Bara hivyo Nchunga alipaswa kuzingatia hilo na kuitisha mkutano mapema zaidi.

"Mwezi Julai nguvu za wanachama na wadau wa soka wa klabu zinatakiwa zielekezwe kwenye maandalizi ya timu," alisema.

Nchunga alisema "nipo kwenye kikao" alipotafutwa jana kuelezea madai kuwa Kombe la Kagame ni moja ya sababu za kutoa notisi ya zaidi ya siku 30 kabla ya mkutano huo.

Katika hatua nyingine, Makele amesema kuwa vijana wa Yanga leo watafanya mkutano klabuni hapo ambapo moja ya ajenda itakuwa kujadili tarehe hiyo ya mkutano mkuu wa klabu iliyotangazwa na Nchunga.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles