Monday May 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tume ya Katiba yafaa isaidiwe elimu ya uraia

30th July 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, amesema pamoja na Tume ya Taifa ya Kukusanya Maoni juu ya Marekebisho ya Katiba, kuhodhi utoaji wa elimu ya mabadiliko ya katiba, azaki zitaendelea kufanya hivyo kwa kuwa jukumu hilo ni haki yao kikatiba.

Alisema kifungu cha 17(2) (a) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Katiba, 2011, inatamka kuwa ukusanyaji wa maoni ya wananchi ni jukumu la Tume na si mwingine na kwamba asasi/kikundi nyingine lazima kutoa taarifa/kuomba ruhusa kwa Tume ya Katiba au Mkuu wa Wilaya/Mkurugenzi wa Halmashauri kwa niaba ya Tume ndipo kutoa elimu ya mabadiliko ya
Katiba, ambapo wanatakiwa pia kueleza fedha wametoa wapi.

Alisema hayo wakati akiwasilisha mada kuhusu, “Mchakato wa Katiba mpya Tanzania: Tulikotoka, Tulipo na Tuendako,’ katika semina iliyoandaliwa na Shirika la Hakikazi Catalyst la jijini hapa kwa wananchi, viongozi wa ngazi za kata na vijiji kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.

Aidha, alisema siyo vizuri kuiachia Tume hiyo kufanya kazi hizo peke yake bila kufuatiliwa kwani zinaweza kujitokeza kasoro ambazo zinaweza kufumbiwa macho.

Alitaka Azaki na wadau wa katiba kuona jukumu la kuifuatilia tume hiyo ni yao ili kuibua mapema kasoro zitakazojitokeza.

Alisema kwa mfano, wakati tume hiyo ikikusanya maoni katika moja ya mkoa hivi karibuni, utangulizi uliokuwa ukitolewa na mjumbe wa kuwakaribisha wananchi na maelezo kuhusu kazi za tume hiyo yalidaiwa kuwa ndiyo elimu ya uraia, jambo ambalo alilipinga.

Pia alisema wakati wa kupokea maoni baadhi ya wajumbe huwauliza maswali magumu wananchi bila sababu ya msingi kama vile kutaja Ibara ya Katiba pale ambapo wanataka sehemu hiyo iondolewe au kufanyiwa marekebisho.

Wakichangia mada hiyo, baadhi ya washiriki walitaka kiwepo kipengele cha kuwadhibiti viongozi kwenda kupata matibabu nje ya nchi huku wakiacha kuboresha huduma za hospitali za hapa.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment