Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Utesaji wafungwa karne hii ni aibu

10th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Jana ukurasa wa tatu wa gazeti hili kulikuwa na habari kuhusu wafungwa waliohukumiwa kifo kuanza mgomo wa kula katika gereza la Lilungu lililopo mkoani Mtwara.

Nia ya mgomo huo ni kuwasilisha kilio chao dhidi ya dhuluma wanazodai kufanyiwa kwa kupewa chakula cha hovyo, kunyanyaswa, kupigwa na askari magereza pamoja na rufaa zao kuchelewa kusikilizwa, kwa ujumla walalamikia hali mbaya ya gereza.

Wafungwa hao wanamshutumu mkuu wa gereza hilo kwamba amekuwa akisimamia ukatili dhidi yao walidai kuwa ama amefumbia macho vitendo vya unyanyasaji dhidi yao au ameruhusu vitendo hivyo vitendeke. Miongoni mwa vitendo hivyo ni pamoja na kukatiwa huduma za matunda, nyama na sukari kwenye uji badala yake wanakunywa uji wa chumvi.

Kadhalika, walisema wamefutiwa huduma ya matibabu na badala yake wamekuwa wakielekezwa kujitibu wenyewe au kujinunulia dawa, jambo ambalo siyo sahihi.

Wafungwa kadhaa waliozungumza na gazeti hili, bila kuonyesha kuhofia majina yao kutajwa kama ambavyo imekuwa ni utamaduni wa watu wengi wanapozungumza na vyombo vya habari, walisema wazi kuwa hawana wanachohofia, wanataka uongozi wa juu wa magereza na ikiwezeakana Wizara ya Mambo ya Ndani iingilie kati kutatua hali hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwa wafungwa kulalamikia hali duni ya huduma ndani ya magereza; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa taarifa juu ya hali mbaya ya magereza nchini.

Aghalab, magereza mengi yamefurika wafungwa na mahabusu kupita kiasi, huduma za chakula, matibabu na haki nyingine za wafungwa zimekuwa ama haziheshimiwi kabisa au pale zinapoheshimwa ni kwa kiwango cha chini kabisa.

Tunafahamu na kutambua kuwa magereza siyo hoteli ya kitalii kwa maana hiyo iwe na huduma za kiwango cha juu sana, lakini pia siyo sehemu ya kuwatesa wafungwa na kukataa walau kutambua haki zao za msingi, ndiyo maana tunasema kuwa kilio cha wafungwa wa gereza la Lilungu kina maana na ni wajibu wa wenye dhamana na magereza kuingilia kati kutafakari na kutafuta njia ya kutoa majawabu ya changamoto zilizoko.

Kwa miaka na miaka taifa hili limeaminishwa kuwa magereza ni sehemu ya kwenda kukomoa wafungwa; dhana ya kifungo imegeuzwa kabisa kutoka ile ya kurekebisha mkosaji ili akimaliza kifungo chake awe raia mwema na badala yake wanaomaliza kifungo mara nyingi hutoka wakiwa wahalifu sugu kuliko walivyoingia.

Dhana hii ya kufanya magereza kuwa kiama imeathiri sana mfumo mzima wa utawala wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu; pamoja na ukweli kwamba nia ya kifungo kwa mkosaji kuwa ni adhabu, malengo makuu ni kumfanya mkosaji ajutie kosa lake, lakini pia kumbadili kutoka kuwa mhalifu kuwa raia mwema. Kwa kufanya hivyo magereza zitakuwa zimejenga jamii adilifu.

Hawa wanaogoma huko Lilungu kwa hakika wanataka kuwasilisha kilio chao kwa watawala kwamba pamoja na ukweli kwamba wao ni watu wanaosubiri kunyongwa na kwa kweli inapozingatiwa kuwa kwamba unyongaji siku hizi haufanyiki kama ilivyokuwa zamani, kitendo cha kuwanyima huduma muhimu kama matibabu ni sawa tu na kutaka uhai wao utwaliwe katika njia za kawaida. Huu si utu.

Tunajua kuwa kumekuwa na malalamiko mengi sana katika mfumo mzima wa uendeshaji wa magereza nchini; kumekuwa na taarifa na mapendekezo mbalimbali jinsi ya kubadili hali ya mambo ilivyo ili utu utawale zaidi kwa wale waliotiwa hatiani, inajulikana wazi kwamba kila raia mwema ni mfungwa mtarajiwa kwa sababu haijalishi unakuwa mwangalifu kiasi gani katika kutii na kuzingatia sheria, kuna siku isiyokuwa na jina mtu anaweza kuteleza.

Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia watu waliopata kushika nyadhifa kubwa kubwa serikalini hadi uwaziri tena kwa miaka mingi, wakiingia mahabusu, tumeshuhudia waliopata kuwa mabosi katika ofisi za serikali na mashirika ya umma wakiishia mahabusu baada ya kufikishwa mahakamani, lakini pia tumeshudia baadhi wakihukumiwa vifungo jela.

Ingawa ni kweli walitiwa hatiani na mahakama baada ya kesi zao kuendeshwa, bado kukosa kwao kisheria hakuihakikishii jamii kwamba waliteleza kwa kupenda, inawezekana wengine walikuwa wanatekeleza maelekezo ya wakubwa wao kwa nia njema, lakini sasa wamegeukwa.

Hatusemi haya kutetea uhalifu, wala hatukusudii kushabikia uvunjaji wa sheria, ila tunataka haki itawale kila mahali, hata kama mtu amehukumiwa kifungo, bado anabaki kuwa binadamu na haki za binadamu hazibagui, ni haki tu, iwe kwa mfungwa au kwa mtu huru uraiani.

Ni kwa jinsi hii tungefarijika kama magereza ingejigeuza kuwa sehemu ya mafunzo ya kubadili wahalifu ili wawe raia wema wa kesho. Magereza isizalishe wahalifu sugu bali iwabadili kuwa raia wema.
ends

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles