Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Nani ni raia hususani makabila yanayoishi pembezoni mwa TZ?

14th July 2012
Print
Comments

Makundi mbalimbali ya kijamii na wadua wa siasa wamesikika wakiisifu Tume ya Kuratibu maoni ya Katiba Mpya ambayo iliteuliwa hivi karibuni na Rais Kikwete.

Binafsi naungana na wachambuzi na wadau hao wa siasa kuitakia kila la kheri Tume katika kutekeleza majukumu hayo muhimu waliokabidhiwa na Taifa.

Niseme tu kuwa, Tume ambayo tayari iko kazini mikoani kupata maoni ya wananchi, imekabidhiwa hadidu za rejea ambazo zitakuwa ndiyo mwongozo katika kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yao.

Nisingependa kuingilia majukumu ya Tume, lakini nikiwa kama mdau miongoni mwa kundi la wananchi wanaopaswa kutoa maoni mbele ya tume hiyo, angalabu nitumie fursa hii kuchangia maoni yangu ili tume iweze kuyachambua muda ukifika wa kufanya majumuisho.

Makala haya yatajielekeza katika maeneo matatu ambayo yamekuwa kero kwa kipindi kirefu hususan kwa wakazi wa makabila ya pembezeni mwa nchi (mipakani). Haijalishi ni mipaka ya ukanda gani mwa nchi lakini tatizo hili limekuwa kero kubwa ambalo linawagusa wakazi wa makabila wanaoishi mipakani tu.

Maeneo hayo matatu ya msingi ni kama ifuatavyo; Mosi ombi kwa Tume; ya pili linahusu “Uraia” nani anastahiki kuitwa raia wa nchi hii. Sheria inasemaje kuhusu uraia wa makabila yanayoishi pembezoni mwa nchi yetu, eneo la tatu linahusu nafasi ya Rais, Mbunge na Diwani kitaifa, baada ya kuchaguliwa na kuapishwa kutumikia nchi pasipo kuingiliwa na vyama vyao vya niasa.

TUME IHESHIMU IBARA YA 8 KATIBA YA SASA

Ifahamike kwamba, kimsingi Tume hii imepewa madaraka, mamlaka na uhuru wa kufanya kazi yake kwa mujibu wa sheria za nchi. Pamoja na madaraka na uhuru waliyopewa, napenda kutoa wito au ombi kwamba Tume iheshimu ibara ya 8 ya katiba ya sasa inayosema; 8(1) “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo; (a) Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba”. Mwisho wa kunukuu.

Ninachotaka kusema ni kwamba, endapo Tume itazingatia na kutii ibara hii ya 8(1) – (a), sina shaka kazi yao itakuwa rahisi sana. Wananchi wapewe nafasi kubwa ya kusikilizwa kwani wao ndio msingi wa mamlaka yote.

Baada ya ombi hilo hapo juu kwa Tume, sasa nijielekeze katika maudhui ya makala haya. Kama nilivyobainisha awali, kero ya kwanza inahusu “Uraia”. Nani anastahili kuitwa raia hususan makabila yanayoishi pembezoni mwa nchi yetu.

Kimsingi haiwezekani Katiba (mama) ikaingizwa kero (sheria) zote zinazogusa wananchi. Kero zingine zinatungiwa kanuni, sheria na taratibu kwa mujibu wa mfumo wa nchi. Sheria kanuni na taratibu hizi zinatayarishwa na mamlaka zinazotambulika na kuratibiwa na wizara husika na vyombo vya dola.

Suala la Uraia limetajwa ndani ya Katiba Ibara ya (5) kifungu kidogo cha pili (2) yenye vipengele a, b, c, d, ambavyo vinazungumzia haki ya kupiga kura sheria ya 1984 Na 15 1b.6. Katiba haikemei wala kuzuia baadhi ya watu, mamlaka au vyeo vyao kuwanyima haki wakazi wa makabila yanayoishi mipakani eti kwa sababu lugha wanayozungumza kabila fulani ni sawa na lugha wanayozungumza kabila fulani katika nchi ya jirani.

Kwa mfano; kuna Wakurya wa Kenya na wa Tanzania; Wajaluo wa Kenya na wa Tanzania Wasuba wa Kenya na wa Tanzania; Wahaya wa Tanzania na Uganda; Waha wa Tanzania na Rwanda; Wangoni wa Tanzania na Malawi, Zambia au Msumbiji n.k.

UGAWAJI MAKOLONI KATIKA BARA LA AFRIKA

Historia inatukumbusha tarehe 15 Novemba, 1884 mpaka tarehe 26 Februari, 1885 siku ambapo mataifa ya Ulaya yaliitisha “Berlian West African Conference” na kupitisha makubaliano (Resolution) ya kugawana makoloni katika Bara la Afrika. Mataifa hayo yalikuwa ni Ureno, Ubelgiji, Uingereza, Ujerumani, Italy na Ufaransa.

Baada ya Berlin West African Conference, mwaka 1890 King Leopold II wa Ubelgiji na Bismarck walichochea kwa vitendo ugawaji Makoloni katika Bara la Afrika, Ugawaji huu uliochora mipaka ya nchi, haukuzingatia ustaarabu wa makazi kiutawala, (kinship) kiukoo (clan), makabila (tribes) bali mipaka ilichorwa kulingana na mahitaji na makubaliano ya mataifa hayo. Mipaka hiyo iliyochorwa iliacha makabila, koo, familia wakigawanya pande mbili bila ridhaa yao.

Katika siku za hivi karibuni kumezuka kadhia ya kuwaonea makabila ya hapa nchini yanayopakana na nchi jirani yanayotumia lugha moja. Tatizo hilo linawakumba sana sana makabila yanayoishi mipakani mwa Tanzania na Kenya; Rwanda, Uganda, na Burundi yaani makabila yanayoishi ukanda wa Kaskazini Magharibi (Kigoma, Kagera) na ukanda wa kaskazini – Mashariki (Mara na Arusha)

Kuna baadhi ya watu wamekumbana na kadhia hii ya uraia hasa inapofika kipindi cha uchaguzi au kwa sababu tu ya kutofautiana kimawazo na watawala (Ruling Elite). Mwandishi mahiri na mashuhuri Jenerali Ulimwengu, Mh. Arkado Ntagazwa n.k ni wahanga waliowahi kuonja adha hiyo. Hivi karibuni kijana Bashe naye alienguliwa na (kunyimwa haki) ya kugombea Ubunge kwa sababu ya Uraia. Sioi Summary alitenguliwa kugombea baada ya kushinda kura ya maoni eti kwa sababu ya uraia. Hata hivyo alikuja kugombea baada ya utata wa uraia wake kushughulikiwa.

Hata hivyo, naiomba Tume ya kuratibu maoni ya Katiba Mpya iangalie upya kwa undani maana halisi ya uraia. Nani anastahiki kuitwa raia na kwa wakati gani. Kwanini mtu awe raia wa nchi pale asipogombea nafasi ya uongozi lakini ikifika kipindi cha uchaguzi anahesabika kuwa siyo Raia. Kwanini ukanda wa Kaskazini – Magharibi na Kaskazini Mashariki ndio wanaandamwa sana na kadhia hii?

URAIA MAKABILA YAISHIYO MIPAKANI

Tume iweke wazi haki na uhuru wa makabila yanayoishi mipakani. Eti ukijulikana wewe ni Mjaluo basi tayari unahesabika kwamba wewe ni raia wa Kenya. Kadhalika kabila la Muha, ataitwa Mrundi au Mnyarwanda. Mbona makabila ya kati kati ya nchi na ukanda wa mwambao wa bahari hawasumbuliwi.

Bila kuathiri sheria zilizopo na bila kuathiri haki na uhuru wa makabila haya ya mipakani naiomba Tume itoe ufafanuzi wa kina kuhusu haki ya kuishi kwa makabila ya kutoka ukanda huo niliyoyataja.

Kuna siku, makabila haya yatashindwa kuvumilia uzalendo na kufikia hatua ya kuasi iliwaungane na makabila ya nchi jirani. Tume ijaribu kupata maoni mengi katika kanda hizo. Kama ni suala la uraia, basi iwekwe wazi.

Eneo lingine ambalo nadhani Tume lingeangalia vizuri ni nafasi ya Rais, Mbunge na Diwani, baada ya kuapishwa kutumikia nchi. Sheria inawahitaji Rais, Wabunge na Madiwani kugombea nafasi hizo kupitia vyama vya siasa vilivyosajiliwa. Kwa maana nyingine, vyama husika vinakuwa wadhamini wa wagombea hao.

Sina ubishi wala pingamizi na sheria hiyo ya udhamini. Kitu kinachokera jamii ni pale vyama hivi vinapoweka utashi wa kisiasa mbele na kuweka utaifa pembeni katika kuwang’oa wabunge au madiwani waliochaguliwa na wananchi eti kwa sababu tu ya udhamini.

Nchi yetu ilifanya Uchaguzi Mkuu mwaka juzi 2010, katika kipindi cha mwaka mmoja na ushee tu, tayari tumeshahudia wabunge wawili wa (CUF na NCCR) wakingolewa na madiwani watano wa Chadema eti kwa sababu ya utovu wa nidhamu. Je, tunajenga demokrasia au tunabomoa. Itakuaje siku chama kilichopo madarakani kitakapoamua kumng’oa Rais wa nchi eti tu kwa sababu ametofautiana na watu wachache ndani ya chama chake? Je, huku siyo kuwanyima haki wananchi wasiokuwa wanachama wa vyama lakini walitumia haki yao kumpigia kura Rais au Wabunge bila kujali vyama vyao?

Nashawishika kuamini kuwa, hasara ambayo Taifa linaingia baada ya chaguzi ndogo ukilinganisha na faida ya kufukuzana hovyo ni kubwa. Lakini pia wananchi wanapokonywa mamlaka yao kama ilivyoanishwa kwenye katiba Ibara ya 8-(c) ambayo inasema; “Serikali itawajibika kwa wananchi”.

WALIOCHAGULIWA NA WANANCHI WAPEWE KINGA

Binafsi nafikiri Tume ingekuja na mapendekezo ya kurekebisha sheria hii ndogo ya uchaguzi. Ni vema Rais, wabunge na madiwani na sheria za vyama vya siasa ziweke bayana kuwa watawala hawa wabaki kuwa viongozi wa kitaifa hata pale watakapokuwa wamepoteza hadhi ya uanachama wa vyama husika.

Tume ingefikiria kuleta sheria ya kinga kwa viongozi hawa wa kuchaguliwa bila kuathiri sheria zingine za nchi. Rais, Mbunge au Diwani akifukuzwa kwenye Chama chake aendelee kutumikia wadhifa wake hadi pale mahakama itakaporidhika kwamba kosa alilofanya linaangukia kwenye makosa yaliyoanishwa katika sheria za nchi na si vinginevyo.

Kama nilivyobainisha awali, siyo kwamba sheria zote ziingizwe ndani ya Katiba (mama). Ninachotaka kusema ni kwamba, kwa kuwa Tume hiyo imesheheni magwiji wa sheria na taaluma zingine za kijamii, nadhani wangeenda mbali zaidi ya kuandaa Katiba mpya na kuangalia pia kwa mapana yake sheria zingine za nchi, kanuni na taratibu ili kurutubisha sheria mama (Katiba) katika maeneo yote yanayogusa jamii kimaisha.

Nafunga makala haya kwa kisisitiza kwamba Tume litafute jawabu la uraia kuhusu makabila yanayotoka mipakani.

Makala yameandikwa na John M. Kibasso anapatikana kwa simu 0713 – 399 004 au

0767 – 399 004

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment