Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Dk. Bana: Tuujadili muungano siyo kuuvunja

23rd May 2012
Print
Comments

Mjadala wa Katiba mpya ambao ulitawala mwaka mzima wa 2011 unaendelea na wananchi na wadau mbalimbali wanaendelea kutoa maoni yao kuhusu nini kiwemo ama kisiwemo kwenye Katiba mpya ijayo.Mwandishi Wetu amezungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa, Dk. Benson Bana, kuhusu masuala mbalimbali ya kuwekwa na kuondolewa kwenye Katiba.

Yapo mengi yanasemwa kuhusu  Muungano, wako watanzania wanaotaka uendelee kama ulivyo, wapo wanaotaka uvunjwe kwa maoni yao wakiona hauna manufaa, wapo waotaka ufanyiwe marekebisho lakini uendelee kuwepo.

Dk. Bana yeye anasema kwenye safari ya kuelekea kuundwa kwa Katiba mpya ni vyema pamoja na umuhimu wa Muungano uliopo lazima wananchi waachwe waujadili na waseme wanataka muungano uwe wa aina gani.

“Muungano ni tunu na tukijaribu kuuvunja dunia nzima itatushangaa, mimi sitajali zikiwa serikali tatu, moja au mbili lakini ninachotaka ni kwamba muungano uendelee kuwepo, athari za kuvunja Muungano ni kubwa sana tusithubutu hata kujaribu kuuvunja,” anasema.

“Muungano ni tunu kama vile amani, mshikamano wa kitaifa, undugu, kama kuujadili tujadili muundo wake uweje ila si vyema tukaanza kufikiria kuuvunja, wenzetu huko nje watatuona watu wa ajabu” anasema.
“Mwananchi anayetaka serikali moja aachwe aseme sababu zake, anayetaka serikali mbili na wanaotaka serikali tatu waachwe wazungumze sababu za kutaka hivyo ila mwisho wa siku Muungano huu lazima tuhakikishe upo na uzidi kuimarika,” anasema

Dk. Bana anasema haki za binadamu ni jambo la msingi ambalo linapaswa liendelee kuwepo kwenye Katiba ijayo ili mtu akinyimwa haki aidai na aipate kwenye mamlaka zinazohusika.

Anasema mgawanyo wa madaraka ni kitu kingine muhimu na uwepo utaratibu wa kuhakiki kama mfumo uliopo unafanya kazi au la (check and balance)lengo likiwa ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na wananchi wanapata huduma kwa wakati.

Dk. Bana anasema kuna watu wamekuwa wakililia madaraka ya Rais yapunguzwe lakini yeye kwa maoni yake anasema iwapo Rais atapunguziwa madaraka anaweza kuwa kibogoyo, yaani akawa Rais asiyeweza kutoa maamuzi hivyo baadhi ya mambo yakaenda kombo.

Ila anachopendekeza Dk. Bana, anasema lazima uwekwe utaratibu kwenye Katiba ijayo ambapo maamuzi ya Rais hasa katika uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu yatakuwa yakihojiwa na mamlaka kama Bunge.

Anasema baadhi ya watendaji wanaoteuliwa na Rais lazima wawe wanathibitishwa na Bunge ama Kamati ya Bunge lengo ikiwa ni kupata watu dhabiti na ambao wanaaminika kwa umma wa watanzania.
Anasema kuna nafasi nyeti serikalini ambazo lazima uteuzi wake ufanywe kwa makini zaidi ili wapatikane watu safi na ambao jamii haina shaka bao hata kidogo.

“Mfano Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi, wathibitishwe na Bunge ili tupate watu ambao wanauwezo na jamii inawaamini, huu utaratibu wa kumwachia kila kitu rais afanye peke yake iko siku tutaona mambo ya ajabu” anasema
Dk. Bana anasema makatibu wakuu na maofisa mashuhuri wanapaswa kushindanishwa wanapoomba kazi badala ya kuteuliwa tu na kuanza kazi moja kwa moja.

“Hatukatai kwamba Rais asiteue, awateue lakini lazima tuweke chombo kwenye Katiba ijayo kitakachowathibitisha, mtu aombe kazi aitwe ajieleze watu wapime waseme kama anawafaa au la, hapo tutapata watu makini na watakaotusaidia kwenda mbele zaidi“ anasema

Katiba isichezewe

Dk. Bana anasema Katiba itakayoundwa itoe fursa kwa wananchi kushirikishwa kila inapotokea serikali inataka kufanya mabadiliko makubwa ya Katiba , badala ya kundi la watu wachache kukaa na kuamua kwa niaba ya wananchi wote.

Wabunge wawajibishwe

Kuhusu wabunge wanaotoa ahadi na kutotimiza, anasema lazima uwekwe utaratibu wa wananchi kuwahoji na wakishindwa kujieleza waondolewe kwenye nafasi hizo hata kabla ya miaka mitano.
Anasema Katiba ijayo iweke chombo maalum cha kuwawajibisha wabunge ambao wamekuwa wakitoa ahadi lukuki na kuwahadaa wananchi na kutimkia zao maeneo ya mijini kuponda raha.

“Nani anamwajibisha mbunge?, mfano mtu anakuja anawaahidi wananchi ahadi kem kem kisha wanamchagua lakini hatekelezi na badala yake anafanya mambo kinyume na matakwa ya wananchi, Katiba iweke chombo ambacho wananchi watakitumia kumwajibisha mbunge wa aina hii,” anasema

Wakuu wa mikoa na wilaya

Kuhusu nafasi wa wakuu wa mikoa na wilaya, Dk. Bana anasema lazima ufanyike upembuzi makini kama kuna umuhimu wa wao kuendelea kuwepo na ikibainika kuwa hawana kazi basi nafasi hizo ziondolewe kwenye Katiba ijayo.

“Tufafanue majukumu ya RC na DC na kama ikionekana hawana kazi nafasi hizo zifuwe,”
Anasema wakuu wa wilaya na mikoa wakiondolewa hakutakuwa na athari zozote na badala yake kinachotakiwa ni kuimarisha halmashauri za wilaya ili zitoe huduma nzuri kwa wananchi.

“Kazi zote ambazo DC anafanya zinaweza kufanywa na Mkurugenzi wa Halmashauri (DED) kwa kusaidiana na watendaji wake hivyo nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ni upotevu wa fedha na rasilimali za nchi,” anasema

Uraia wa nchi mbili

Dk. Bana anasema haoni kwanini serikali inakigugumizi kuruhusu uraia wa nchi mbili na ameomba Katiba mpya iwatambue watanzania wenye uraia wa nchi mbili ili wakati wa uchaguzi watumie haki yao ya msingi ya kuwachagua viongozi wanaowaona wanafaa.

Mgombea binafsi

Dk. Bana anasema pia haoni sababu kwa serikali kushindwa kuruhusu mgombea binafsi katika nafasi za ubunge na udiwani.

Kwa nafasi ya urais, Dk. Bana anaunga mkono msimamo wa serikali kwani kunaweza kuwa na utata iwapo mgombea binafsi kwa nafasi ya urais atashinda hasa namna ya kuunda serikali.

Anasema katiba mpya itoe nafasi ya madaraka kupelekwa kwa wananchi na wananchi wapewe fursa ya kuona fomu za mali za viongozi wanapoingia na kutoka madarakani.

Anasema utaratibu huo utasaidia kupata viongozi waadilifu na wanaojali rasilimali za umma kwani wataogopa iwapo watajilimbikizia mali kama inavyotokea hivi sasa.

Anasema hivi sasa wananchi wamewekewa vikwazo vingi kuona mali za viongozi wao hali ambayo inashamirisha vitendo vya ulaji wa fedha na rasilimali za umma.

“Kuwe na uwazi sana kwenye kuangalia mali za viongozi wa umma, naamini hiyo inaweza kusaidia kuwafanya viongozi wawe na maadili mema kwani angalau wanaweza kuwa waogoa kuiba mali za umma,” anasema

Anasema ndani ya Katiba ijayo lazima masuala muhimu kama matibabu kwa wazee, wanawake wajawazito, ielezwe bayana kwamba wananchi watapata bure.

Anasema inawezekana kabisa wananchi wakapata huduma hizo bure iwapo serikali itaziba mianya yote ya wizi wa fedha za umma kama ilivyoripotiwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Huduma hizi ni muhimu kwa wananchi na ninaamini kabisa kwamba serikali ikibana matumizi na kuzuia upotevu wa fedha za umma haya yanawezekana kabisa, kuna fedha nyingi zinapotelea mikononi mwa watu wasio waaminifu, mabilioni ya fedha yanafujwa kama ilivyosemwa kwenye ripoti ya CAG,” anasema.

Dk. Bana anampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukubali ripoti ya CAG isomwe na kujadiliwa bungeni kuwa hali hiyo imesaidia kuweka uwazi na wananchi kujua namna fedha zao zinavyotumika.

Lakini anasema isiishie kwenye ripoti ya CAG peke yake bali hata taasisi zingine ziwe zinakabidhi ripoti zake kwa Bunge na kujadiliwa na ni njia nzuri ya kuwawajibisha watendaji wabadhirifu na wezi wa mali za ummana hata wale watakaoonekana kuzembea kwenye nafasi zao.


 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles