Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Serikali isisahau mchelea mwana kulia hulia yeye

25th April 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Juzi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa saba wa Bunge la 10 pamoja na mambo mengine aligusia msimamo wa wabunge juu ya udhaifu uliopindukia wa baadhi ya mawaziri katika kusimamia majukumu yao katika wizara.

Wabunge wengi, kama si wote waliochangia mjadala wa ripoti za Kamati za Bunge, Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na hata ile ya Maliasili na Mazingira, waliunga mkono mapendekezo ya kuwajibika kwa mawaziri kutokana na ufujaji wa fedha za walipakodi katika wizara na taasisi za serikali kwa mwaka wa fedha wa 2009/10 kama ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilivyokuwa inaonyesha.

Pinda bila kutaja neno ‘kujiuzulu’ katika hotuba yake na pia kutaka kuingia kwa undani katika suala la wito wa kutaka mawaziri wanane wajiuzulu, aliliambia Bunge kuwa Serikali inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa ushauri na mapendekezo yaliyomo katika taarifa za kamati hizo.

Ingawa pia Pinda alisema wazi kuwa wabunge wameonyesha hisia zao katika kujadili masuala hayo kwa umuhimu wa kipekee, alianisha kuwa waligusia mwenendo wa matumizi ya fedha za serikali kwenye wizara, taasisi za umma, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa, hata hivyo hakutaka kujipambanua kwa uwazi zaidi kama kweli suala la uwajibikaji litakuwamo kwa upande wa mawaziri kama ambavyo wabunge wamekuwa wakishinikiza.

Kadhalika, katika hotuba hiyo kinyume cha ilivyokuwa ikitarajiwa kwamba Pinda angetamka lolote kama kweli kumekuwako na maamuzi ya kujiuzulu kwa mawaziri hao, alijielekeza tu kuahidi kuwa watafanyia kazi ushauri wote uliotolewa na wabunge wakati wakijadili ripoti za kamati za Bunge, hali iliyoacha maswali mengi zaidi si kwa wabunge tu, bali pia na kwa umma kwa ujumla wake.

Kulingana na joto la kisiasa lililokuwa limegubika nchi kwa takribani wiki moja sasa, juu ya mwenendo wa mawaziri wanane kutokana na kushindwa kwao kuwajibika, kiasi cha ama kuhusika moja kwa moja na ubadhirifu wa mali ya umma au kujiachia tu hivyo waliochini yao kupata upenyo wa kujiendeshea mambo kiholela na kusababisha mabilioni ya Shilingi kuteketea kwa njia za kifisadi, kitendo cha Pinda cha kukwepa kuwa muwazi katika suala hilo, anaonekana kuwa anafunika kombe ili mwanaharamu apite.

Hakuna anayeweza kuukataa ukweli kwamba hali ndani ya serikali ni mbaya. Ni mbaya kwa maana ya kukosekana kwa uwajibikaji wa pamoja, lakini pia ni mbaya kutokana na udhaifu mkubwa wa kusimamia kazi za serikali, kiasi cha kuathiri si hadhi ya serikali tu, bali hata uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake makuu, hususan kuwahudumia wananchi.

Fedha nyingi ambazo kama zingetumika vizuri zingeliweza kutatua matatizo mkubwa ya huduma za kijamii, kama ujenzi wa barabara, na kuboresha mazingira ya sekta ya elimu, zimeteketea kwa njia za kifisadi. Mabilioni haya ama yamelipwa kama mishahara hewa, au manunuzi hewa yamefanywa na pengine misamaha mikubwa ya kodi imetolewa kiasi cha kufikia asilimia 18 ya makusanyo ya ndani ya serikali.

Ukali wa wabunge kwa vyovyote vile, na hata juhudi za kutaka kmpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, si wa bure. Ni ukali unatokana na uchungu kwa sababu nchi hii sasa imegeuzwa kama shamba la mjane asiye na mtetezi, kila anayetamani chochote humo anajichumia bila aibu wala woga.

Sisi tunasema kuwa Pinda ametoa hotuba yake, inawezekana kabisa kuwa ana mipango kabambe ambayo itaonyesha matunda mazuri muda mfupi ujao katika kukabiliana na changamoto zilizotolewa na wabunge, kama huu ndiyo mkakati wake kama alivyoahidia, tunamtakia kila la heri tukijua kuwa mikakati inayotekelezeka na endelevu ndiyo kitu cha maana zaidi kuliko maneno matamu yasiyo na tija.

Hata hivyo, kama ni janja ya kawaida ya watawala wetu ya kukwepa kuwajibika kwa kutoa kauli kwamba tumesikia na tutafanyia kazi kumbe ni mbinu za kufunika kombe mwanaharamu apite, basi Pinda akumbuke kuwa Bunge la bajeti haliko mbali, atakutana na wabunge hao hao aliowaahidi juzi, watamuuliza kiko wapi.

Hapa ndipo hali itakuwa mbaya kuliko ile ya awali. Ni kwa maana hiyo tunasema kwa hali ilivyo sasa, haiwezekani mambo kuachwa tu kama yalivyo kwa matarajio kuwa huu ni upepo unaovuma kwa hiyo utapita. Ni wakati wa kujitafakari kwa kina zaidi sasa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles