Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Baada ya kuonyesha uwajibikaji, Rais JK aboreshe usimamiaji

22nd April 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Kujiuzulu kwa mawaziri wanane kutokana na kilio cha wabunge wa pande zote, na hoja ya wabunge wa upinzani (kwa kiwango kikubwa zaidi) kuwataka wajiuzulu ni tukio la kihistoria hapa nchini.

Ni tukio ambalo linafuta mazoea kongwe ya miaka takriban 40 ambako uzembe unawajibishwa kwa kuhamishwa, na ni pale tu inapoonekana kuna kosa linalokaribia jinai ndipo waziri anahitajika kujiuzulu. Ni mara ya kwanza mawaziri wametakiwa kujiuzulu kutokana na usimamizi hafifu wa wizara na sekta zao, ikawabidi.

Ni wazi kuwa kusingekuwa na yote hayo kama siyo ushindani kufikia viwango vya juu zaidi katika medani ya siasa, kiasi kwamba ilikuwa inaonekana chama tawala kinapoteza sifa yake kwa kasi, kila kukicha.

Katikati ya wiki aliihama CCM Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, James ole Millya akilalamikia migongano ya makundi na uhitaji wa uadilifu katika chama tawala. Kuondoka kwake kukafuatiwa na makada kadhaa wengine katika wilaya tofauti kuonyesha kuwa zipo nyasi kavu, bado tu kiberiti.

Ni katika mazingira hayo ambako ilibidi hatua kuchukuliwa kwani ripoti takriban zote za kamati za kudumu za Bunge kushughulikia hesabu za maeneo tofauti zimefichua ‘madudu’ ya kushangaza, na haielekei kuwa mawaziri walikuwa wanajali kupita kiasi.

Ilielekea kuwa yapo maeneo ambako tatizo lilikuwa waziri mwenyewe kufanya ‘madudu’ hayo na siyo tu kushindwa kusimamia maovu yasifanyike. Ikawa hakuna haja uangalifu kupita kiasi, ajiuzulu mmoja tu kuonyesha mfano, ila ionekane kabisa kuna mabadiliko.

Pale kilio cha Bunge na wananchi kwa jumla kinapofanyiwa kazi, ni taasisi za nchi kwa jumla ambazo zinapata nguvu zaidi, kuwa kanuni za malipo serikalini si za kudharauliwa, na hakuna saini za watu wasioguswa.

Ule msemo wa ‘men whose decisions are final’ ni wazi umetawala kwa muda mrefu, kutokana na utegemezi ambao miaka yote umekuwepo kati ya serikali na chama tawala, kuwa wakijisikia vibaya kwa kuwajibishwa kuna hatari ya mshikamano kupungua kwa uchaguzi mkuu. Inafikia mahali tishio hilo linapanguliwa.

Kimsingi ndiyo hapo tulipofikia, kuwa CCM inajikaanga kwa mafuta yake yenyewe kuruhusu uzembe wa kutisha na ubadhirifu wa wazi kutawala katika wizara, idara maalum, mamlaka na taasisi zinazojitegemea.

Kukubali hitaji la kuwajibika mawaziri ni mbiu ya mgambo, kuwa sasa kanuni zitakuwa zinafuatiliwa, kwani vigogo wa ubadhirifu wanapopigwa, wasimamizi na wakaguzi kote wanajua kuwa ‘la mgambo limelia,’ na wasije kuingia matatani pia. Hatusemi hali itabadilika kabisa, ila uangalifu utaongezeka.

Mabadiliko hayo vile vile yanasaidia kupungunza munkari uliokuwa unahofiwa wakati wa kutoa maoni kuhusu muundo wa katiba mpya na sifa za vyombo tofauti vya usimamizi wa shughuli za nchi.

Baada ya kudhihirisha kuwa mabadiliko yanawezekana, mjadala wa katiba mpya utaelekea zaidi katika uboreshaji, na siyo kuleta mapinduzi kwa kupitia katiba mpya kwa vile serikali, au mkuu wa nchi, ‘hasikii wala haoni.’ Na kwa watendaji inasaidia kukumbusha kuwa kulindana kupo, ila si kila mtu afanye tu atakavyo.

Kwa mantiki hiyo tunaona kwamba suala la kulindana haliwezi kuondoka moja kwa moja kutokana na kanuni ya uwajibikaji wa pamoja, kuwa kwa yale ambayo yamekubaliwa serikalini, hata yangeenda vibaya inabidi serikali yote ibebe mzigo kwa pamoja.

Ni njia ya kumwezesha kila mtendaji kujiamini kuwa mradi havunji dhamana aliyopewa kwa maslahi binafsi au kwa uzembe uliokithiri – na kila uzembe una maslahi mahali – basi atalindwa. Pale mtendaji serikalini anapokosea na huku anajitahidi kutenda yanayopasa lazima alindwe, si anapokengeuka.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles