Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mfumuko wa bei kuongezeka kwa asilimia 20

24th March 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera

Wataalamu wa uchumi wameonya kuwa huenda mfumko wa bei nchini ukafikia asilimia 20 mwezi Juni mwaka huu kutoka asilimia 17 iliyopo sasa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kudhibiti kasi hiyo.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi iliyotembelea mkoa wa Morogoro kutazama hali ya uzalishaji wa sukari katika viwanda vya Mtibwa wilayani Mvomero na Illovo wilayani Kilombero, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Misanga, alisema hali ya mfumuko wa bei nchini kwa sasa ni mbaya sana.

Mapema kabla ya kuanza kwa ziara hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera kuwa dhumuni la ziara ya kamati yake katika viwanda hivyo ni kutazama uzalishaji wa sukari lakini pia kujadiliana na wenye viwanda namna ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.

Alisema kuwa kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu imebainika kuwa chakula na mafuta ni bidhaa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa mfumuko wa bei kama uzalishaji wa bidhaa hiyo utapungua na kushindwa kukidhi mahitaji yaliyopo.

Misanga alisisitiza kuwa tafiti hizo zinaonyesha kuwa chakula kimechangia mfumuko wa bei kwa asilimia 11.8 huku mafuta yakitajwa kuchangia mfumuko wa bei kwa asilimia 2.9 na asilimia zilizosalia zinaonyesha kuchangia na sababu zingine nyingi.

Aliongeza kuwa ili kukabili hali hiyo, Kamati ya Fedha na Uchumi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelazimika kutembelea viwanda vya sukari na kujadili na wamiliki wa viwanda hivyo ili kuona mikakati iliyopo katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kutoka tani 250,000 hadi kufikia hitaji la sukari la tani 330,000 kwa mwaka.

Misanga ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Singida Kusini alisema kuwa upungufu uliopo sasa wa tani 80,000 umesababisha kupanda kwa bei ya sukari nchini kutoka wastani wa Sh 1,500 hadi Sh 1,700 mwaka jana hadi kufikia Sh 2,500 hadi Sh 2,700 mwaka huu.

Ikiwa katika Kiwanda cha sukari cha Mtibwa, kamati hiyo licha ya kupata fursa ya kujionea mitambo ya kisasa ya kilimo cha miwa, lakini pia Ofisa Rasilimali watu, Benard Kiula, aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa kiwanda hicho kimejipanga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema kuwa ili kufikia lengo hilo kiwanda kimeanza shughuli za upanuzi wa mashamba yake ambapo kwa sasa jumla ya hekta 4,000 zimeanza kulimwa katika eneo lake lenye ukubwa wa hekta 10,000 na eneo la sasa lina ukubwa wa hekta 7,500.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles