Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wafungwa watishia tena kugomea chakula

9th May 2012
Print
Comments
Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema

Mgomo wa wafungwa unanukia kwa mara nyingine, baada ya kuwepo kwa taarifa za wafungwa wa kifo waliopo gereza la Ilungu lililopo mkoani Mtwara, kutangaza kugoma kula kuanzia leo.

Nia ya mgomo huo ni madai ya chakula, kupinga manyanyaso ya kipigo kutoka kwa askari magereza pamoja na rufaa zao kuchelewa kusikilizwa na hali ya gereza kuwa mbaya.

Wakizungumza na NIPASHE mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya wafungwa walimshutumu mkuu wa gereza hilo kwamba amekuwa akisimamia ukatili dhidi yao. Walisema tangu Desemba mwaka jana, wafungwa hawapewi matunda, hawapikiwi nyama wala hawawekewi sukari kwenye uji badala yake wanakunywa uji wa chumvi.

Wafungwa waliozungumza na NIPASHE na namba zao kwenye mabano ni Abdul Ali Sunna (303/2008), Salehe Ramadhani Juma (151/2005), Said Ali Majeje (93/2011), Hussein Said Ntanda (95/2011) na Omary Mussa (104/2011); wote wamehukumiwa kifo. Kadhalika, walisema wamefutiwa huduma ya matibabu na badala yake wamekuwa wakielekezwa kujitibu wenyewe au kujinunulia dawa, jambo ambalo sio sahihi.

Kuhusu unyanyasaji, walisema tukio la kusikitisha zaidi lilitokea Desemba mwaka jana baada ya mfungwa mwenzao waliyemtaja kwa jila moja la Selemani mwenye namba 205/2010 ambaye amekaa gerezani kwa miaka 30 alitoroka, lakini akadakwa na askari.

Walisema askari sita walimfunga kwenye mti na kumpiga kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tisa alasiri; bila kuwepo kwa Ofisa Usalama wa gereza, kinyume cha taratibu. Walisema baada ya kutoa malalamiko yao, wamegeuziwa kibao kwa kunyanyaswa na kupigwa.

Mfungwa mwingine Salehe Ramadhani Juma mwenye namba 151/2005, alikaa gerezani tangu mwaka 1995 na hukumu ya kesi yake ilitolewa mwaka 2005 na alikata rufaa, lakini hadi leo haijasikilizwa.

Msemaji wa Jeshi la Magereza, Omary Mtiga, alipotafutwa na NIPASHE kuzungumzia azma hiyo na namna jeshi linavyoshughulikia kero hizo za wafungwa, alisema bado hawajapata taarifa hizo hivyo hawezi kusema chochote.

“Taarifa za mgomo hatujazipata, lakini pengine nianze kufuatilia ili tujue tatizo nini, hadi kesho tunawezakuwa tumepata taarifa ambayo tunaweza kukueleza,” alisema Mtiga.

Kwa mara ya mwisho wafungwa waligoma Juni mwaka jana katika gereza la Maweni, mkoani Tanga kwa madai ya kupewa chakula kibovu.

Kufuatia mgomo huo, aliyekuwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema, alitoa ahadi ya Kambi ya Upinzani bungeni kufuatilia hali za magereza kwa kuwa haiwezekani wafungwa wakagoma tu kula kwa kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo rufaa zao kuchelewa kusikilizwa na pindi wanaposhinikiza ili zisikilizwe wanahamishwa gereza.

Lema alisema asilimia 50 ya mahabusu wanakaa hadi miaka minane bila kesi zao kusikilizwa kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika, jambo linalochangia migomo magerezani.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles