


.jpg)
Mgogoro kuhusiana na usajili wa beki wa Kelvin Yondani ulichukua sura nyingine jana baada ya jina la mchezaji huyo anayeichezea pia timu ya taifa (Taifa Stars) kuwasilishwa kwa Shirikisho la Soka (TFF) na klabu mbili za Yanga na Simba.
Hata hivyo, hatua hiyo haikushangaza kwani mahasimu hao wa jadi wamekuwa wakilumbana kwa wiki kadhaa sasa tangu Yondani alipoamua kuchepukia Yanga huku klabu yake ya zamani ya Simba ikidai kuwa bado inammiliki kwavile alisaini mkataba mwingine wa kuendelea kuitumikia timu yao.
Mgogoro mwingine unaofanana na ule wa Yondani unatarajiwa kuendelea kushika kasi pia kati ya klabu za Simba na Azam kufuatia timu zote mbili kuwasilisha TFF jina la kiungo Ramadhani Chombo ‘Redondo’. Mchezaji huyo anayeichezea pia Taifa Stars, aliondoka Azam wiki iliyopita na kujiunga Simba, lakini Azam wakaja juu na kusema kuwa Redondo ni wao kwavile bado hajamaliza kutumikia mkataba wake.
Jana saa 5:59 usiku ndiyo ilikuwa mwisho wa kuwasilisha usajili wa wachezaji wa ndani wa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayoanza Septemba Mosi, huku dirisha la usajili wa wachezaji wanaotoka nje ya nchi likitarajiwa kufungwa Septemba 10.
Katibu Mkuu wa Yanga, Selestine Mwesigwa, alisema jana kuwa tayari wameshawasilisha kikosi chao ambacho kimepata baraka za kocha wao kutoka Ubelgiji, Tom Saintfiet.
Mwesigwa alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo baada ya kufanya taratibu zote za usajili zilizowekwa na kamwe hawakukurupuka katika kukamilisha zoezi hilo.
Alisema kwamba baada ya kukamilisha usajili, kikosi chao kitacheza mechi mbalimbali za kirafiki kujiandaa na msimu mpya huku wakiwa na matarajio makubwa ya kutwaa ubingwa kutoka mikononi mwa mahasimu wao, Simba.
Aliwataja wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho kuwa ni makipa
Yaw Berko, Ally Mustafa 'Barthez' na Said Mohamed, mabeki ni Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende na Stephano Mwasika ambaye wakati mwingine hucheza kama kiungo kutokana na majukumu anayopewa.
Wengine ni Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondan, Mbuyi Twite, Ibrahim Job na adislaus Mbogo.
Viungo ni Athuman Idd 'Chuji', Juma Seif, Salum Telela, Nizar Khalfani, Shamte Ally, Idrisa Rashid, Omega Seme, Haruna Niyonzima, Rashid Gumbo na Nurdin Bakari.
Safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) inaundwa na Hamis Kiiza, Said Bahanunzi, Didier Kavambagu na Jerry Tegete.
Mbali na nyota hao, Yanga pia wamewasilisha wachezaji wa timu ya vijana ya umri chini ya miaka 20 kama kanuni zinavyoeleza.
Juzi, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema ni Azam na Kagera Sugar ndizo zilizotangulia kuwasilisha usajili wao.
Osiah alisema zoezi la kuwasilisha usajili liliendeshwa kwa kasi 'ndogo' kutokana na viongozi wa klabu kushindwa kusajili kwa kutumia njia ya mtandao, hivyo walihitaji msaada wa maafisa wa TFF kuanzia juzi hadi jana mchana kutekeleza zoezi hilo.
Alisema kuwa TFF itatoa taarifa kamili juu ya usajili wa wachezaji hao baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kupitia usajili huo na pia malalamiko mbalimbali ambayo yamewasilishwa.
Wakati huohuo, Simba imetangaza kuwapa mkataba wa miaka miwili kila mmoja wachezaji wapya, beki wa kati wa timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), Pascal Ochieng na mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Hearts of Oak ya Ghana.