Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mafao ya wastaafu yaboreshwe

17th June 2012
Print
Comments

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha mwishoni mwa mwaka jana ya kutoa malipo ya wastaafu wa serikali waliokuwa wakilipwa kila baada ya miezi sita kuwa kuanzia Januari mwaka huu watalipwa kwa utaratibu wa miezi mitatu mitatu, ilipokelewa na wastaafu wengi kwa kutoa angalizo moja kubwa kwa serikali ili iangalie upya viwango vya malipo hayo ambayo wamedai sasa hayakidhi gharama za maisha yaliyosababishwa na mfumuko mkubwa wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha.

Mafao ambayo yanalipwa kwa wastaafu sasa hivi yalifanyiwa marekebisho madogo kwa mara ya mwisho mwaka 2007, ni miaka mitano sasa tangu marekebisho hayo yafanyike na wastaafu hao bado wanaedelea kuishi kwa kutegemea malipo ya uzeeni hayo ingawa bei ya bidhaa muhimu karibu zote zimeongezeka kwa zaidi ya asilimia mia moja. Uwezo wa kujikimu kwa mstaafu huyo pia umepungua kwa asilimia hizo hizo, sasa anaweza kuwa amelazimika kuingia katika mikataba migumu zaidi ikiwa ni pamoja na ya magonjwa ya mfadhaiko wa moyo.

Hakuna kitu duniani kinachompa amani ya kudumu binadamu kama fedha, mtumishi anayekuwa na sifa ya kustaafu anastahili heshima iliyotukuka, anastahili kuendelea kutunzwa na serikali kwa gharama stahiki bila kuwa na visingizio, ni kutokana na mchango wake katika kuimarisha huduma za kijamii, amani uchumi, elimu pamoja na miundombinu mingine katika nyanja mbalimbali muhimu katika taifa.

Mfumuko wa bei na gharama za maisha zinapopanda zinamgusa zaidi mstaafu kwa vile huyo anakuwa hana namna ya kukabiliana na mabadiliko kutokana na umri wake kuwa mkubwa pamoja na mafao yake kidogo na yasiyokidhi mikiki ya gharama zinazopanda kila siku.

Kwa mstaafu wa nchi hii, ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 55, umri wake wa kuendelea kuishi duniani unategemea mapenzi ya Mwenyezi Mungu, na kama haki zake za mafao ya uzeeni yatalipwa kwa utaratibu utaratibu wa kila baada ya miezi sita kama ulivyo sasa, ni dhahiri kuwa baadhi yao wanafariki hata kabla ya kumaliza miezi hiyo sita. Kwa utaratibu mpya uliotangazwa wa kuanzia Januari mwakani, ni dhahiri utapunguza 'pressure' kama tu malipo yao yataboreshwa.

Mtumishi anayestaafu kwa mujibu wa umri wake, anaweza kukabiliwa na mshtuko wa kawaida baada ya kugundua kuwa huduma nyingi alizokuwa akizipata hazitapatikana tena, siyo rahisi kuudhibiti mshtuko wa aina hiyo, na mshtuko wa aina hiyo unaweza kusababisha magonjwa mbalimbali kama ya shinikizo la damu, moyo, kisukari nk. Maradhi ya namna hiyo mwisho wake husababisha vifo vya ghafla kama ambavyo tayari imeshawatokea wastaafu wengi.

Suala la kuwapa malipo ya kila mwezi wastaafu ni la kimataifa, ingawa kwa kiwango kikubwa linategemea hali ya uchumi wa nchi.

Pamoja na vigezo hivyo, serikali zote duniani zinawaheshimu na kuwaenzi wastaafu wake kutokana na ukweli kuwa kwa namna hali ya nchi hizo zinavyoonekana, ustawi wake umefika hapo zilipo kutokana na juhudi za wote waliotumikia kama waajiriwa na ambao kwa wakati huo wanakuwa wastaafu, ni kutokana na nguvu na juhudi za pamoja za watumishi wa umma ndipo inapotokea tathmini ya hali ya maendeleo ya nchi yoyote.

Kwa ajili ya kuyaweka mambo sawa ya wastaafu nchini, na kwa vile wastaafu wanachohitaji zaidi ni huduma ya malipo ya fedha zinazoweza kukidhi gharama zao za kila siku, na kwa sababu kila aliye katika ajira serikalini akifikisha umri wa lazima atastaafu na ataachia ngazi, ni wakati muafaka sasa wa kuanzisha idara ya kusimamia maslahi na haki stahiki za wastaafu kwa kila wizara, ili kitengo hicho kiwe na mawasilisho ya kila wakati kulingana na hali ya maisha ya wastaafu wa kila wizara, na majumuisho yake kupelekwa ndani ya Bunge na Waziri wa Fedha ikiwa kama mswada wa kufanyia marekebisho ya kuboresha mafao kwa wastaafu wote.

Utaratibu wa kulipwa pensheni hizo kila baada ya miezi sita uliwekwa kusudi fedha kidogo anazopata mstaafu zilundikane kwa muda huo ili siku akizipata zionekane nyingi. Mstaafu anayepata pensheni ya Sh.50,000 kwa mwezi walidhani atafarijika kama akilipwa Sh 300,000 baada ya miezi sita, kumbe ukweli upo pale pale kuwa hazimwongezei uwezo wa aina yoyote, matumizi yake yatabakia ya uwezo wa Sh. 50,000 tu.

Katika hali ya maisha ya kawaida, wastaafu wamechangia kiasi kikubwa cha mapato ya serikali katika sekta mbalimbali walizowahi kuzitumikia, na katika kipindi chote cha utumishi wao wamekuwa pia wakipata fursa ya kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali za fedha.

Huduma zote zilizokuwa zikipatikana kabla ya kustaafu zimekoma mara baada ya kuachia ngazi ya utumishi, na hali halisi ikaonekana kama wafanyakazi hao wametupwa, baadhi ya idara zikawa zinawaona wastaafu kama ni mzigo, na hasa wakati wastaafu wanaporudi katika ofisi zao kufuatilia nyaraka kabla ya mafao yao kukamilika.

Serikali pia iangalie namna ya kuwasaidia wastaafu kwa kuwapa fursa ya mikopo katika mabenki, kwani wao ni kama watumishi wa akiba, na ndio maana weanaendelea kupata malipo ya pensheni hadi kifo kitakapowakuta.

Katika Bajeti ya mwaka huu, serikali iangalie kwa umuhimu mkubwa kuboresha mafao ya wastaafu hawa kwani hiyo ni haki yao ya kimsingi na wala siyo hisani. Kila mfanyakazi atastaafu na kustahili kuishi kama binadamu mwenye heshima mbele ya jamii.

Maoni: 0715-047304 na 0762-233116

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment