


.jpg)
Wakazi Mkoani Rukwa wamelalamikia ukosefu wa dawa za aina mbalimbali katika vituo vya kutolea huduma vya serikali hali inayochangia wao kushindwa kupata msukumo wa kujiunga na mfuko wa afya ya jamii.
Hayo yalisemwa na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Challa kilichopo katika Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wakati wakizungumza na wataalamu wa Mfuko wa Bima ya Afya Taifa waliofika katika kijiji hicho kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii.
Wananchi hao ambao ni Bi Tekra Sangu, pamoja na Bw. Justin Mwanisawa wamesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya ukosefu wa dawa katika vituo vya serikali jambo ambalo linalalamikiwa hasa na wateja wa Bima ya Afya na hivyo kuwafanya waanchi hao kukosa moyo wa kujiunga na mifuko hiyo ya afya ya jamii.
Hata hivyo wananchi hao wamesema kuwa ili mfuko huo uweze kupata wateja wengi serikali iboreshe hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma
Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Afya ya jamii Bi Joyce Sumbwe amewataka wananachi hao kujiunga na mfuko huo ili waweze kupatiwa huduma za matibabu bila ya kuwa na fedha mikononi ikiwa ni pamoja na kuufanya mfuko huo uweze kuwa na uwezo wa kupata dawa kwa wingi kutokana na michango hiyo ya wananchi.
Awali mfuko huo wa Bima ya Afya kabla ya kutembelea kijiji hicho cha Chala, walifanya mkutano mkubwa na wadau wa mfuko huo mjini Sumbawanga ambapo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya aliutaka mfuko huo kuboresha huduma za dawa na kuwataka watoa huduma kuwa na lugha nzuri kwa wateja wao.