Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nchunga ajiuzulu Yanga

25th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Yanga mwanasheria Lloyd Nchunga

Hatimaye Mwenyekiti wa Yanga mwanasheria Lloyd Nchunga jana alitangaza rasmi kujiuzulu nafasi yake hiyo aliyokuwa anaishikilia baada ya kulalamikiwa na wanachama wa klabu hiyo kuwa ameshindwa kuwangoza, imefahamika.

Shinikizo lililomsukuma Nchunga kuachia madaraka hayo lilionekana kuzidi pale wanachama zaidi ya 700 walioongozwa na Baraza la Wazee walipokutana kwenye makao makuu ya klabu hiyo Jumapili iliyopita katika mkutano wa wanachama ambao haukuwa rasmi kwa mujibu wa katiba.

Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Nchunga alikiri kuchukua maamuzi hayo ili kuinusuru Yanga ambayo sasa imekuwa kwenye mgogoro mkubwa na ilikuwa imegawanyika kutokana na yeye kuendelea kukaa madarakani.

"Ni kweli nimeamua kujiuzulu ili kuepusha mgogoro ambao uko ndani ya klabu yetu, lengo ni kuinusuru Yanga ambayo ni muhimu zaidi kuliko mimi kuendelea kuwa kiongozi," alisema Nchunga.

Aliendelea kusema kuwa ameona si busara yeye kuendelea kukaa madarakani wakati baadhi ya wanachama wamesema kwamba wako radhi kuona Yanga inashushwa daraja au inafungiwa kushiriki mashindano yoyote kwa sababu yake.

Alisema kwamba licha ya kujiuzulu nafasi hiyo aliyochaguliwa na wanachama mwaka juzi ataendelea kubakia mwanachama mwaminifu na mtiifu wa klabu hiyo.
"Tayari nimeshamkabidhi Katibu Mkuu (Selestine Mwesigwa) barua ya maamuzi yangu," alisema Nchunga.

Hata hivyo, Mwesigwa jana hakuweza kupatikana kuthibitisha kama mtendaji mkuu wa kuajiriwa wa klabu hiyo kama amepokea barua hiyo kutoka kwa Nchunga.

Katiba ya Yanga inaeleza kuwa endapo mwenyekiti atajiuzulu nafasi yake itashikwa na makamu mwenyekiti (Davis Mosha) ambaye naye tayari alishajiuzulu.

Viongozi wa Yanga waliobakia madarakani ambao hawajajiuzulu ni pamoja na Titto Osoro, Salim Rupia na Sarah Ramadhani.

Wengine ambao walishajiuluzu ni Mohammed Bhinda, Mzee Yusuph, Seif Ahmed 'Magari', Abdallah Binkleb, Pascal Kihanga na Ally Mayai.

Sababu nyingine iliyosababisha wanachama kumtaka Nchunga aachie madaraka ni kipigo cha magoli 5-0 ambacho Yanga ilikipata kutoka kwa watani zao Simba, siku chache tangu alipotakiwa aikabidhi timu kwa wazee ili waiandae timu hiyo iliyokuwa haina morari baada ya wachezaji kutolipwa mishahara yao na posho kwa miezi mitatu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles