Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mechi muhimu zaidi Simba kwa miaka 9

13th May 2012
Print
Comments

Wawakilishi wa Bara katika Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika, Simba, watakuwa na mechi muhimu zaidi kwa miaka tisa wakati itakapoikabili Al-Ahly Shandy kwenye mchezo wa marudiano wa mashindano hayo, nchini Sudan leo.

Endapo Simba itamudu kusonga mbele baada ya pambano la leo, si tu itafuzu kucheza robo-fainali bali pia itaingia kinyang'anyiro cha kuwania zawadi ya sh. bilioni 1 ya bingwa wa Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika.

Na ili kusonga mbele Simba ina anasa hata ya kumudu kufungwa si kwa zaidi ya tofauti ya mabao mawili na ikaitoa Shandy kufuatia ushindi wake wa 3-0 nyumbani wiki mbili zilizopita.

Kwenye robo-fainali hiyo ambayo itachezwa kwa mtindo wa ligi ya timu nne-nne, Simba itakuwa na nafasi ya kutwaa zawadi ya kiasi kikubwa zaidi cha fedha tangu icheze hatua kama hiyo ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2003.

Kwa kuingia robo-fainali tu Simba itakuwa imejihakikishia kupata zawadi ya sh. milioni 240 endapo itashika mkia kwenye kundi lake.

Lakini habari njema ni kuwa Wekundu wa Msimbazi wanaweza 'kuamka' matajiri zaidi endapo watatwaa ubingwa wa michuano ambayo ilifika fainali mwaka 1993 wakati ikiwa Kombe la CAF.

Bingwa wa Kombe la Shirikisho huzawadiwa sh. bilioni 1 katika dola za Marekani; sh. milioni 691 endapo timu itafungwa katika fainali na hupata sh. milioni 382.4 kama itashika nafasi ya tatu kwenye kundi lake la robo-fainali.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, kocha wa timu hiyo Milovan Cirkovic amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo na kusema kuwa watacheza kwa nguvu kuhakikisha wanapata goli la mapema.

"Kocha hana wasiwasi, nimeongea naye amesema wachezaji wapo tayari kwa mchezo wa kesho (leo) na anaamini tutasonga mbele kwenye mashindano haya," alisema Kamwaga.

Kamwaga alisema kuwa pamoja na hujuma wanayofanyiwa na wenyeji wao viongozi na wachezaji wamezipotezea kwa kuwa wanafahamu fitina za mpira kwenye mashindano ya kimataifa.

Mchezo wa leo utakuwa na presha kubwa kwa wenyeji Shandy kwa kuwa wanatafuta ushindi wa tofauti ya magoli manne.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles