



Wakati kocha Thom Saintfiet wa Yanga akitarajiwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuwafundisha mabingwa hao wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), raia huyo wa Ubelgiji anatakiwa afahamu kwamba klabu hiyo ina changamoto mbalimbali zilizowakuta makocha waliotangulia ikiwemo ya kutolipwa mishahara yao ya kila mwezi kwa wakati.
Licha ya kuwepo kwa madai ya mara kwa mara ya kucheleweshewa mishahara na posho za makocha, akiwemo pia Fred Felix Minziro aliyemkuta sasa klabuni hapo, changamoto nyingine anayopaswa kuifahamu mapema Saintfiet ni juu ya nani hasa atakayewajibika moja kwa moja kumlipa mshahara atakaokubaliana na uongozi au wanachama waliokuwa wakifanya naye mazungumzo kabla ya kuwasili nchini juzi.
Akizungumza jana, Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kuwa baada ya Saintfiet kusaini mkataba wa kuanza kuiongoza timu yao leo mchana, baadaye jioni atashuka kwenye uwanja wao wa Kaunda kuanza rasmi kazi ya kuinoa timu hiyo ambayo inajiandaa kutetea ubingwa wa Kombe la Kagame litakalowaniwa kuanzia Julai 14 hadi 29.
Sendeu alisema kwamba tayari uongozi wa Yanga umefikia hatua za mwisho za mazungumzo na kocha huyo na wanaamini ataifanya timu yao iwe bora na yenye ushindani katika mashindano hayo ya kimataifa na pia ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Aliongeza kwamba baada ya kocha huyo kukutana na wachezaji, atatoa mapendekezo yake kama timu hiyo iingie kambini au iendelee na mazoezi hayo ya wachezaji kutokea nyumbani kwao.
"Mazungumzo yako vizuri na kesho (leo) jioni tunatarajia kocha wetu mpya aanze kuonyesha vitu vyake pale kwenye Uwanja wa Kaunda," alisema Sendeu.
Katika kipindi cha miaka mitano, Yanga imekuwa na makocha tofauti na wengi wameshindwa kukaa kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwa muda wa miaka miwili.
Makocha ambao wameifundisha Yanga kuanzia mwaka 2007 na kuondoka kwa sababu mbalimbali, nyingi zikiwa ni za kutotekelezwa kwa makubaliano ya mkataba ni Waserbia Milutin Sredojovic
'Micho', Dusan Kondic, Kostadin Papic na pia Mganda Sam Timbe.
Hata hivyo, Papic ambaye alikuja nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2009, alirejea tena mwaka jana baada ya Mganda Timbe aliyeipa klabu hiyo ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Kagame kutimuliwa.
Micho ambaye sasa ni Kocha wa timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi), aliondoka nchini baada ya timu hiyo kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Ndogo mwaka 2007.
Kabla ya kuondoka, Mserbia huyo alisema kwamba viongozi wa Yanga walikuwa wakishindwa kutekeleza programu za mazoezi alizokuwa akitoa na kusikitishwa pia na tabia ya uongozi wa ‘Wanajangwani’ wakati huo kuithamini timu pale tu ilipokuwa ikikabiliwa na mechi dhidi ya watani zao wa jadi, ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba.
Kondic aliyetwaa mikoba ya Mserbia mwenzake, aliamua kuachana na Yanga baada ya kutofautiana na uongozi ambao ulishindwa kukubaliana naye kwenye maamuzi ya usajili wa wachezaji, huku kocha huyo akidaiwa kusajili wachezaji 'vijeba' wasio na viwango, akiwemo Jama Mba na Honore Kabongo ambao waliishia kusotea viti vya jukwaa la mashabiki katika msimu mzima wa ligi.
Baada ya kuondoka kwa Kondic, ndipo timu hiyo ilipomtwaa Mserbia Papic.
Kocha huyo alitofautiana na Yanga na kutimka kabla ya kurudi baadaye na kuondoka tena kabla ya mkataba wake haujamalizika Aprili 24 kutokana na madai yaleyale yaliyozoeleka kutoka midomoni mwa makocha wengine, ambayo ni ya kutotimizwa kwa mambo mengi ya msingi waliyokubaliana wakati wa kusaini mkataba wao.
Kuna wakati, Papic aliwaeleza waandishi wa habari kuwa uongozi wa klabu hiyo ulikuwa haujali maslahi ya wachezaji na hata yeye mwenyewe baada ya kutolipwa mishahara yao kwa miezi mitatu.
Papic alifichua vilevile kuwa, walishindwa kufanya mazoezi kwa siku saba kwa vile viongozi hawakuwa na fedha za kulipia uwanja waliokuwa wakiutumia wakati huo(Loyola ulioko Mabibo jijini Dar es Salaam).
Wakati Yanga ikijiandaa kwa mzunguko wa pili wa msimu uliopita, Papic akawaambia wazi waandishi wa habari kwamba, endapo timu hiyo itafanya vibaya katika ligi na mashindano ya kimataifa, lawama zote zinapaswa kuelekezwa kwa uongozi ambao haukutaka hata kuwasiliana naye kwa simu, na wala si yeye, wachezaji na maafisa wengin e wa benchi la ufundi.
Rekodi zinaonyesha vilevile kwamba kocha Saintfiet anapaswa kujihadhari na aibu kama iliyomkuta Mganda Timbe, ambaye iliripotiwa kuwa alizuiwa katika hoteli aliyokuwa amepangiwa, iliyoko Mikocheni baada ya uongozi wa klabu yake (Yanga) kushindwa kumlipia gharama za pango.
Saintfiet ajue vilevile kuwa Papic pia alikumbana na tatizo la malazi na kuwahi kulalamika kwamba amepelekwa kwenye nyumba isiyokuwa na huduma za maji wala umeme.
SAINTFIET
Hata hivyo, Yanga pia inapaswa kuwa makini katika kutekeleza makubaliano watakayoingia na Saintfiet. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa kocha huyo havumilii ‘ubabaishaji’.
Novemba 2011, Saintfiet aliyekuwa ameiongoza Ethiopia kwa miezi mitano tu aliachana nayo ghafla, licha ya kuifanya icheze soka safi kiasi cha kupata sare ya ugenini ya 2-2 dhidi ya Nigeria na hivyo kuwakosesha vigogo hao wa soka barani kukosa nafasi ya kushiriki fainali zilizopita za Kombe la Mtaifa ya Afrika (AFCON 2012).
"Licha ya kuwa na mambo mengi mazuri, baadhi ya makubaliano yetu hayakuwa yakitimizwa na hiyo ndiyo sababu ya mimi kuchukua uamuzi huu (wa kuondoka)," Saintfiet aliiambia Reuters baada ya kuachana na Ethiopia.
"Sasa natafuta mahala nitakapokuwa na majukumu makubwa zaidi. Kuwa na majukumu katika mahala ambako wanajali kufanya kazi kwa weledi …," aliongeza Saintfiet , aliyewahi pia kuzifundisha timu za taifa za Namibia (2008-2010) na Zimbabwe alikokaa kwa kipindi cha chini ya mwezi mmoja baada ya kunyimwa kibali cha kufanyia kazi.