Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Somalia yaomba mafunzo ya usalama Tanzania

4th June 2012
Print
Comments
Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed

Somalia imewasilisha maombi kwa Serikali ya Tanzania, iangalie namna ya kuisaidia kujenga na kuboresha taasisi za ulinzi na usalama na sekta za kijamii na kisiasa.

Rais wake, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed alisema hayo kwa waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo na wenyeji wake Rais Jakaya Kikwete katika hoteli moja nje ya jiji la Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita jioni.

Mapema akizungumzia mazungumzo yao, Rais Kikwete alisema kuwa: “tumefanya mazunguzo ya kushauriana na kuangalia hali ipoje Somalia, nchi ambayo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu.”

Kwa upande wake, Rais Ahmed, alisema Rais Kikwete ameahidi kuwaunga mkono katika jitihada zao za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo ili taifa hilo lipate amani ya kudumu.

Pia alisema wamekubaliana kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hizo na kwamba Somalia itahitaji kupata uzoefu wa masuala mbalimbali kutoka Tanzania.

Rais Ahmed alimshukuru Rais Kikwete na Watanzania kwa ujumla kwa kusaidia kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa amani ya Somalia katika masuala mbalimbali kama vile ya kisiasa, maendeleo, ulinzi na usalama.

“Bado tunahitaji maendeleo, kujenga taasisi imara za ulinzi na usalama na sekta bora za kijamii na kwa hiyo tunaomba msaada wa Tanzania,” alisema kwa kifupi.

Katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rais Ahmed alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, majira ya saa 8:11 alasiri akitokea nchini Uturuki alikokuwa kwenye vikao vya kutafuta amani ya nchini yake.

Baada ya kutoka uwanjani hapo, alipelekwa moja kwa moja hadi kwenye hoteli moja, ambako mwenyeji wake Rais Kikwete alimpokea na kufanya
naye mazungumzo.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment