Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbunge huyu asitoe majibu mepesi

13th May 2012
Print
Comments

Yapo malalamiko kwamba baadhi ya wabunge wetu huamua kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu, majibu ambayo kimsingi hayatoi ufumbuzi wa matatizo ya wananchi, na tabia hiyo ni ishara kuwa wabunge wa aina hiyo hawajishughulishi ipasavyo kujua kwa undani kiini cha hoja za msingi za wananchi wao au labda kwa makusudi hawataki kufanya tafiti za kina ili kupata ufumbuzi wa kweli wa matatizo ya wananchi.

Viongozi wa aina hii hawana tofauti kubwa na kama waliokumbwa na kashfa za ubadhirifu wa fedha za umma kwa baadhi ya mawaziri na wizara zao ambapo Rais alilazimika kufanya mabadiliko makubwa hivi karibuni kwa wizara zilizotuhumiwa. Mbunge anapotetea umbumbumbu wa wanafunzi akidai unasababishwa na mabadiliko ya mitaala...!

Katika hali ya kawaida kabisa, kila mtu atashangaa sana kusikia wapo wanafunzi ambao wamesajiliwa kuingia kidato cha kwanza katika shule za hapa nchini wakati hawajui kusoma wala kuandika!

Inasikitisha, jiulize swali moja la kawaida sana kuwa mwanafunzi huyo amefikaje huko? Ni katika utaratibu upi basi ameweza hata kufika darasa la saba wakati hajui kusoma wala kuandika, amepimwa katika vigezo gani huyo mwanafunzi hata akapitishwa kuanzia darasa la kwanza hadi la saba na kuendelea na elimu ya sekondari wakati hawezi kusoma wala kuandika?

Katika utaratibu wa kawaida kabisa, mwanafunzi anapoingia darasa la kwanza, anakuwa mbumbumbu! Ni huyu anayestahili kuwa na sifa ya kutokujua kusoma wala kuandika, na ni katika darasa la kwanza mwanafunzi anapokazaniwa ajue kusoma na kuandika kabla hajaingia darasa la pili, huo ndio msingi wa elimu yote wa kujua kusoma na kuandika.

Zimejitokeza taarifa ndani ya baadhi ya vyombo vya habari hasa katika magazeti kuwa baadhi ya wanafunzi waliosajiliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari nchini mwaka huu, hawajui kusoma wala kuandika! Kama taarifa hizo ni za kweli basi hilo ni balaa kubwa.

Taarifa hizo zinatakiwa zichunguzwe kwa kina na kama kulikuwepo na njama za wadau wa aina yoyote katika mchakato huo mbaya wasionewe huruma, waburuzwe katika vyombo vya sheria.

Wapo wanafunzi 226 katika mkoa wa Mbeya waliosajiliwa kidato cha kwanza mwaka huu ambao hawajui kusoma wala kuandika, wilaya ya Kyela ikiongoza kwa kuwa na idadi ya wanafunzi 86, inafuatiwa na wilaya ya Chunya yenye wanafunzi 50, Rungwe 29, Mbozi 18, Mbarali 16, Mbeya Vijijini 16, Mbeya Mjini saba na Ileje wanne. Ipo mikoa mingine kama mkoa wa Kigoma ambao nao una idadi ya waliosajiliwa kidato cha kwanza bila kuwa na sifa za kufaulu, yote ikiwa ni katika ukiukwaji wa maadili na wenye dhamana.

Afisa Elimu wa mkoa wa Mbeya Juma Kaponda alisema hivi karibuni kuwa ameliandikia Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) barua ya kulitaka kuchunguza matokeo ya wanafunzi hao na akawasisitizia kuwa kama kukibainika kuwa kulikuwepo na udanganyifu wowote wakati wa kufanya mitihani, wahusika waondolewe madarasani.

Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alidai kuwa sababu inayochangia wanafunzi hao kutojua kusoma na kuandika ni kutokana na kubadilika kwa mitaala ya kufundisha.

Sijaiona hoja ya msingi katika suala la mabadiliko ya mitaala, kimsingi umuhimu wa kusoma na kuandika hauna msongamano wa mitaala itakayovuruga mbinu ya dhamira ya kumfanya mwanafunzi ajue kusoma na kuandika.

Katika madarasa ya awali kabisa ya shule za msingi, masomo yanayosisitizwa zaidi ni mawili, 'Kusoma na Kuandika', hakuna ujanja wa kimitaala zaidi ya hapo, mwanafunzi anayeshindwa kabisa kufikia kiwango kinachotakiwa katika masomo hayo hurudia darasa moja hadi ajue, vinginevyo anatolewa kabisa shuleni, na ni mara chache sana kutokea hilo labda kwa watoto wachache wenye matatizo ya utindio wa ubongo.

Inaelekea sasa upo mchezo wa kuifanyia mzaha elimu, haiwezekani hata mara moja ikaelezwa kuwa yupo mwanafunzi wa kidato cha kwanza ambaye hajui kusoma wala kuandika, kama wapo walimu waliochoka na kukata tamaa ya taaluma hiyo ni afadhali waachie ngazi mapema kuliko kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Ni dhahiri kuwa wadau namba moja wanaotakiwa kubebeshwa lawama za kuwa na wanafunzi walioko sekondari wakiwa mbumbumbu ni walimu. Haiwezekani kabisa mwanafunzi ajifanyie ujanja wa kujisogeza madarasa yote hayo hadi sekondari bila walimu kuhusika. Ikumbukwe kuwa sifa ya elimu ni kuipata elimu yenyewe, na wala siyo idadi ya wanaodhaniwa kuwa na elimu stahiki!

Karne hii ni ya ushindani mkubwa katika taaluma za kisayansi na teknolojia, na ni kupitia katika elimu tu ndipo taifa litakapojikuta lipo katika ushindani wa kweli, inaonekana wengi wanadhani mitandao ya mawasiliano ipo kwa ajili ya kufanya 'short-cut' ya kufikia kilele cha upeo wa maisha.

Wapo waliojilimbikizia vyeti vingi bandia vya taaluma mbalimbali vilivyotengenezwa kutokana na mitandao, vipo kwa ajili ya kuongeza 'cv' bandia wakati wa kutafuta ajira.

Tutajikuta tumeingia katika utapeli wa elimu kwa tabia za 'kuchakachua' taaluma tusizostahili, na hilo litatokana na msingi mbovu wa kutojali elimu yetu kuanzia ya msingi, walimu timizeni wajibu wenu achaneni na kuendekeza sifa bandia za elimu.

Maoni: Simu 0715-047304 na 0762-233116

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles