Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kim awarudisha Bocco, Samata Stars

15th May 2012
Print
Comments
Kocha mpya wa Taifa Stars, Kim Poulsen

Kocha mpya wa Taifa Stars, Kim Poulsen amewarejesha kikosini washambuliaji Mbwana Samata aliyetemwa na kocha aliyemaliza mkataba wake Jan Poulsen, na John Bocco aliyetangaza kustaafu kuichezea timu hiyo kutokana na kuzomewa na mashabiki, huku pia akiita wachezaji 11 kutoka klabu ya Simba na mmoja tu kutoka Yanga. 

Mshambuliaji wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Samata aliachwa na kocha aliyepita kwa maelezo kwamba haonyeshi kujituma uwanjani huku mfungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania Bara iliyomalizika hivi karibuni Bocco akitangaza kustaafu kutokana na "kukosa sapoti ya mashabiki wanaomzomea kabla hata mechi haijaanza."

Bocco hakupatikana katika simu yake kuzungumzia jambo hilo, lakini afisa habari wa shirikisho la soka nchini (TFF), Boniface Wambura waliiambia NIPASHE kuwa nyota huyo alizungumza na kocha Kim na kukubali kurejea kikosini Stars.

Kim aliyeteuliwa kuchukua madaraka ya Mdenmark mwenzake Jan Poulsen ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa Julai na hataongezwa mwingine, jana aliteua kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia hatua ya makundi Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast.

Kim alisema kikosi hicho kitaingia kambini kesho na kwamba katika uteuzi wake umezingatia uwezo wa mchezaji uwanjani, nafasi anayocheza na ubora wake.

Wachezaji walioitwa ni makipa; Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ally (Azam) na Deogratius Munishi (Mtibwa Sugar). Mabeki ni Nassor Masoud Cholo (Simba), Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Simba), Waziri Salum (Azam), Shomari Kapombe (Simba) na Juma Nyoso (Simba).

Viungo ni Mwinyi Kazimoto (Simba), Salum Abubakar (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Jonas Mkude (Simba), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Edward Christopher (Simba- U20), Mrisho Ngasa (Azam) na Frank Domayo (JKT Ruvu - U20).

Washambuliaji ni Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Ramadhan Singano (Simba-U20), Simon Msuva (Moro United - U20), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Haruna Moshi (Simba) na John Bocco (Azam).

Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro itacheza mechi ya kirafiki nyumbani Mei 26 mwaka huu dhidi ya Malawi kabla kuivaa Ivory Coast ugenini Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles