


Diwani wa Kata ya Mianzini iliyopo Mbagala Charambe jijini Dar es Salaam, Cesylia Macha, amefariki gafla wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Siasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata.
Diwani huyo alianguka juzi mara baada ya kumaliza kuzungumza na wajumbe hao katika ofisi za CCM zilizopo Kibonde Maji na kufa muda mfupi baadaye wakiwa njiani wakati akikimbizwa katika Zahanati ya Zakhiem kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja kama diwani huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi gani yaliyosababisha kifo chake.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo, Mustapha Hakika alithibitisha kutokea tukio hilo na kukataa kuzungumzia chanzo cha kifo chake.
“Ni kweli tukio hilo limetokea juzi tulikuwa kwenye mkutano wa Kamati ya Siasa ngazi ya kata yetu kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili kata hiyo yenye matawi 11 ya CCM ikiwemo elimu, miundombinu na maji ambapo kila mwenyekiti wa tawi alizungumzia changamoto hizo” alisema na kuongeza kuwa:
“Malalamiko mengine yalikuwa ni kukaa muda mrefu bila kuitishwa vikao vya kujadili changamoto hizo… diwani alisimama kuzungumza kabla sijafunga mkutano huo alipomaliza kabla hajakaa kwenye kiti alianguka… tulimkimbiza zahanati lakini alipopimwa tuliambiwa na daktari alikuwa ameshafariki dunia” alisema Hakika.
Alisema kabla ya tukio hilo, aliyekuwa katibu wa kata hiyo kwa miaka 15 mfululizo, Hassan Mang’ulo alizungumza masuala mbalimbali kuhusu katana changamoto sugu zinazowakabili.
Alisema maziko ya diwani huyo yanatarajia kufanyika leo saa 10 alasiri nyumbani kwake kuhudhuriwa na wanachama mbalimbali wa CCM.
Diwani huyo alijiunga na CCM mwaka 1977 wakati kikianzishwa.
Wakati wa uhai wake, aliwahi kukihama na kujiunga na Chama Cha NCCR Mageuzi mwaka 1995 baada ya kushindwa kwenye kura za maoni za kugombea udiwani wa Kata ya Charambe kwa tiketi ya CCM.
Alirejea tena CCM mwaka 2000 ambapo aliamua kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama hicho Kata ya Charambe na ujumbe wa kamati ya siasa ya kata na kushinda nafasi zote hizo 2002.
Mwaka 2005 aligombea udiwani wa Kata ya Charambe kupitia CCM na kuibuka mshindi, mwaka 2010 aligombea udiwani kupitia CCM katika Kata ya Mianzini iliyoanzishwa baada ya kugawanywa kwa Kata ya Charambe ambako aliibuka kidedea.
Vilevile aliwahi kuwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa katika ngazi ya uhasibu.