Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Vigogo mafisadi wataendelea kutanua mpaka lini?

13th May 2012
Print
Comments

Serikali ya  awamu ya saba Zanzibar imeamua kuimarisha misingi ya utawala bora kwa vitendo, kwa kutunga sheria za kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kupiga vita vitendo vya rushwa na ufisadi Zanzibar.

Sheria ya kupiga vita rushwa na ufisadi imeleta faraja kubwa kwa wananchi kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa na ufisadi unaofanywa na baadhi ya watendaji na vigogo na wakuu  wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, (SMZ).

Kutokana na tatizo hilo kuendelea kuchukua nafasi kubwa ndio maana Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameamua kupambana nalo kwa vitendo kwa kutunga sheria ya kuanzisha Mamlaka ya kuzuia rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzivbar ya Mwaka 2012 ambayo imeweka adhabu kali kwa watu watakaopatikana na hatia.

Katika mabadiliko hayo ya kuimarisha misingi ya utawala bora pia Rais Dk Shein ameamua kuanzisha Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala bora ili kuongeza Uwajibikaji kwa watumishi wa umma  kwa malengo ya kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.

Hatua ya kuanzishwa kwa Vyombo hivyo ni muafaka kwa vile itasadia kuondoa tatizo la rushwa na ufisadi kwa watendaji Wakuu na viongozi wanaotumia madaraka yao kwa maslahi binafsi na kusababisha hasara kubwa kwa serikali.

Tatizo la rushwa limeathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa haki katika Vyombo vya kusimamia sheria na utoaji wa huduma za jamii na kuwaumiza wananchi wanyonge Zanzibar.

Kwa mujibu wa Ripoti ya uchunguzi wa ubadhirifu wa mali za umma yakiwemo majengo ya serikali na Ardhi ya  Baraza la Wawakilishi (BLW) imebainika kuwepo na ubadhirifu mkubwa wa mali za serikali katika maeneo nane yalifanyiwa uchunguzi na kamati ya BLW.

Kamati hiyo ya BLW imewataja Mawaziri na Watendaji wakuu wa serikali ambao wamehusika na uuzaji wa mali za serikali kinyume na  sheria yakiwemo majengo na ardhi na kupendekeza mali hizo kurejeshwa na wahusika kuchukuliwa hatua.

Ripoti hiyo inasema kwamba katika uchunguzi wao wamegundua wapo baadhi ya Mawaziri wamejigeuza madalali  wa kuuza mali za Serikali bila ya kufuata sheria ya manunuzi na uuzaji wa Mali za serikali Namba  9 ya Mwaka 2005.

“Viongozi wa Juu wa Wizara na Watendaji wao wakuu wanatumia vibaya madaraka yao bila ya kujali maadili ya kazi zao ama bila hata ya kujali sheria na kanuni za utumishi wao ama wadhifa wao, hali ambayo kama hali hiyo itaendelea kuachiwa itafikisha pabaya nchi  inayoongozwa kwa mujibu wa katiba na sheria.”imeeleza Ripoti hiyo.

Ripioti ya kuchunguza kashifa mbali mbali imeongeza kwamba “Hapa inatubidi tuseme kwamba, Mawaziri wa Wizara badala ya kutekeleza majukumu yao, ndiyo wamegeuka madalali wa kuuza mali za serikali kinyume na sheria.”imesisitiza Ripoti ya kamati ya Uchunguzi ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wake Omar Ali Shehe.

Kamati hiyo ya uchunguzi ilipewa hadidu rejea za mpango kazi  nane ikiwemo kuuzwa kwa kiwanja cha Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano, Uuzaji wa kiwanja  cha Livingistone House, Ukodishwaji wa majengo ya Mambo Msiige, Starehe Club na kisiwa cha Utalii cha Changuu.

Mambo mengine ni kuchunguza Jenereta 12 ambazo zilitolewa msaada katika vyanzo vya maji na  Unicef, Uvamizi wa ufukwe na uharibifu wa mazingira katika Chuo cha maendeleo ya Utalii na urasimu wa fidia dhidi ya waathirika mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar.

Kutokana na uchunguzi huo kubaini kuna makosa ya uvunjaji wa sheria na ufisadi yamefanywa na  vigogo na Watendaji wa ngazi za juu wa serikali ipo haja kwa serikali kuhakikisha inachukua hatua za kisheria ili kufikia lengo kujenga misingi ya kweli ya Utawala bora Zanzibar.

Hatua ya vigogo na watendaji walioguswa na kashfa za ubadhirifu kuendelea kushikilia nyadhifa za serikali na kutumia ofisi za umma bila ya  kuchukuliwa hatua ni kwenda kinyume na misingi ya  Utawala bora.

Kwa kuwa tume ya BLW imetumia kiwango kikubwa cha fedha kufanya kazi ya uchunguzi huo ripoti hiyo haitakua na maana yoyote kama itaendelea kuhifadhiwa kabatini au katika droo na watuhumiwa kuendelea kutanua mitaani.

Kwa kuwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi tayali wamepitisha sheria ya Mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu Uchumi Zanzibar yenye adhabu nzito ni vizuri mamlaka hiyo kuanzishwa haraka ili watu wa aina hiyo wafikishwe katika mkondo wa sheria.

Hata hivyo tangu kupitishwa sheria hiyo januari mwaka huu utekelezaji wake hadi sasa bado haujaanza kuonekana katika macho ya wananchi lakini kuendelea kubakia katika nyadhifa vigogo na watendaji wakuu wanaotuhumiwa pia inawezekana kuwa kikwazo katika utekelezaji wa sheria hiyo.

Lazima tukumbuke kwamba hakuna Taifa lolote Duniani ambalo linaweza kuwa na uchumi imara bila ya kuwepo kwa misingi ya Utawala bora na kupiga vita vitendo vya rushwa na ufisadi.

Wakati umefika kwa viongozi na watendaji wakuu wa SMZ kujenga utamaduni wa kuwajibika pale Taasisi zao zinapoguswa na kashfa au wao wenyewe kuhusishwa na ubadhirifu wa mali za umma badala ya kusubiri kutimuliwa na Rais.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles