


.jpg)
Hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kushindwa kutoa tamko kuhusu mawaziri wanaotuhumiwa kwa kushindwa kuziongoza wizara zao na wengine kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za umma na hivyo kutakiwa kujiuzulu, imewasononesha watu wengi, wakiwemo wasomi.
Wengi wamekubaliana na ushauri uliotolewa na baadhi ya wabunge kutaka mawaziri hao wajiuzulu ili kuifanya serikali iwajibike kwa wananchi.
Mkazi mwingine wa Mbauda, Juma Sirikwa, alimtetea Waziri Mkuu Pinda kwa kushindwa kuchukua hatua zaidi kwa maelezo kuwa anayepaswa kuchukua hatua hiyo ni Rais Jakaya Kikwete ambaye kikatiba anatambulika kuwa ni rais mtendaji.
HATARI YA KUINGIA MITAANI
Mwanasheria wa kituo cha Haki za Binadamu na Utetezi wa Watoto na Wanawake cha mjini Morogoro, Aman Mwaipaja, alisema ukimya wa serikali kuwachukulia hatua mawaziri ipo siku wananchi watachoka na kuingia mitaani kutokana na kukosa imani na serikali.
UMMA UMEANGUSHWA
Mwanafunzi wa sheria wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mwashibanda Shibanda, alisema kilichofanywa na Waziri Mkuu ni sahihi kwa kuwa haana mamlaka kikatiba kuwawajibisha mawaziri hao, hivyo anapaswa kulifikisha suala hilo kwa Rais kwa kuwa ndiye aliyewateua.
Waziri wa Elimu wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) mjini Mbeya, Milanzi Petro, alisema Waziri Mkuu ameshindwa kufanya kile kilichotarajiwa na Watanzania na hivyo hafai tena kuwaongoza.
“Kitendo cha Waziri Mkuu kushindwa kutoa tamko la hatma ya mawaziri wake ambao wametolewa mapendekezo ya kujiuzulu kinaonyesha kuwa hawezi kutoa maamuzi magumu na ameshindwa kufanya kile ambacho Watanzania tulikitarajia, kwa kitendo hizo hata akipigiwa kura ya kutokuwa na imani naye ni sahihi,” alisema Petro.
Mwanafunzi wa Mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Eddo Makata, alisema kitendo cha Pinda kushindwa kutoa tamko juu hatma ya mawaziri waliopendekezwa na wabunge wajiuzulu kinaonyesha kuwa anajali maslahi ya chama chake kuliko maslahi ya taifa.
“Waziri Mkuu anajua akichukua maamuzi ya mazuri atakuwa amekiumiza chama chake, CCM, hivyo ameamua kuweka mbele maslahi ya chama badala ya maslahi ya Taifa,” alisema Eddo.
Alisema mbali na kutozingatia maslahi ya taifa, Waziri Pinda pia amekiuka mfumo mzima wa utawala bora kwa Serikali kushindwa kutii maagizo ya Bunge.
Alisema Bunge kama muhimili wa nchi limechaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuisimamia Serikali na hivyo kitendo cha Serikali kutotii maagizo ya Bunge ni ukiukwaji wa utawala bora.
BUNGE LIMEPUUZWA
Mwenyekiti wa Mtandao wa wasomi wa Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema kushindwa kutangaza hatma ya mawaziri ni dharau ya Serikali kwa Bunge.
“Binafsi nimesikitishwa na kitendo cha Waziri Mkuu kushindwa kutoa hatma ya mawaziri wake, hata kama alikuwa na mtazamo tofauti ange-respond (angejibu) kwa wabunge na kueleza hatma ya mawaziri hao kwa kuwa Watanzania wengi walimtarajia kutoa tamko zito,” alisema.
Aliongeza kuwa tangu kuingia madarakani, Pinda ameonekana kuwa mpole kupita kiasi, hali ambayo inasababisha hata mawaziri kufanya wanavyotaka.
“Waziri Mkuu anapokuwa soft (dhaifu), mawaziri nao wanakuwa siyo aggressive (wakakamavu), hivyo wanafanya wanavyotaka na kusababisha hivi sasa ofisi za serikali kuwa siyo mahala pa kazi bali sehemu ya kugawana fedha,” alisema Mwaihojo.
GHARAMA ITAKUWA KUBWA
Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCo), Rwezaura Kaijage, alisema Waziri Mkuu ameshindwa kutimiza malengo aliyojiwekea ya kutaka kutamka bungeni hatma ya mawaziri wanane waliokuwa wanadaiwa kuomba kujiuzulu, kwa sababu tayari historia inamwanika kwamba ni dhaifu katika kujiwekea malengo yake.
“Kitakachoigharimu serikali hii kwa kipindi kilichobaki, kwanza ni umma wa Watanzania unaonekana kupoteza imani na serikali yao kuhusu suala la uadilifu pamoja na uwajibikaji. Na kuendelea kuwakumbatia mawaziri wanaotuhumiwa pasipo kuchukua hatua kunaondoa imani ya wananchi kwa serikali yao,” alisema.
“Pinda ameshindwa kutimiza malengo aliyojiwekea kwa sababu ni dhaifu katika kujiwekea malengo na huo ndio mfumo wa kuongoza kwa kuridhishana. Hata hivyo, naunga mkono hatua ya wabunge kuungana na kutia saini 75 za kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu,” alisema.
Kaijage alisema Rais Kikwete na Pinda hawajachelewa kuchukua hatua dhidi ya mawaziri hao wanaotuhumiwa iwapo wanataka kulinusuru taifa na mkanganyiko unaondelea hivi sasa.
Mhadhiri mstaafu, Frank Mwaisumbe, alisema Pinda amewaangusha Watanzania waliokuwa nyuma yake wakimwamini.
WANANCHI WANAHANGAIKA
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Dk. Charles Kitima, alisema hata kama lengo la serikali siyo kufanya maamuzi kwa kufuata kila linalosemwa, lakini ingekuwa busara kama Waziri Mkuu angetoa ufafanuzi kuhusiana na tuhuma za wazi zilizotolewa dhidi ya mawaziri.
“Wananchi wapo kwenye mahangaiko kuhusu tuhuma zilizotolewa dhidi ya mawaziri, serikali ilipaswa kusema kitu kuonyesha kwamba inawajali watu wake, lakini pia kuonyesha ipo madarakani kwa ridhaa yao,” alisema Dk. Kitima.
Naye Mwakilishi wa shirika la ACORD Tanzania, Donald Kasongi, alisema hatua hiyo ya Waziri Mkuu kukaa kimya kuhusu sakata hilo la mawaziri, kutapunguza imani ya wananchi kwa serikali yao.
Hata hivyo, alisema kuwa mfumo wa uongozi unambana Waziri Mkuu kutochukua hatua hadi pale atakapokuwa amefanya mashauriano na kiongozi mwenye dhamana ya juu kabisa ya mamlaka ambaye ni rais.
“Si jambo zuri kwa serikali kukaa kimya wakati tayari wananchi kupitia wawakilishi wao (wabunge) wamekuwa na heka heka za hapa na pale kuhusu sakata la mawaziri,” alisema.
Mkazi mwingine wa jijini Mwanza, Cosmas Mhoja, alisema hatua ya rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kuruhusu takrima ilichochea wabunge wengi kupatikana kwa rushwa.
Kwa msingi huo alisema hata kama mawaziri watajiuzulu au kufukuzwa, watakaoteuliwa pia watakuwa ni wale wale ambao wametokana na mfumo wa rushwa.
HESHIMA IMESHUKA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie, amesikitishwa na kitendo cha Waziri Mkuu kutotoa tamko lolote kuhusu kujiuzulu kwa mawaziri juzi bungeni alipokuwa akiahirisha Mkutano wa Bunge.
Aliongeza kuwa kitendo hicho kitaivunjia heshima serikali pamoja na CCM. “Watu wengi walikaa kwenye TV zao wakiangalia na mimi nikiwa mmoja wapo ili kuona kama Waziri Pinda atasema lolote kuhusiana na kujiuzulu kwa mawaziri saba.
“Lakini hakutamka lolote, na hii itaisababisha serikali na CCM matatizo makubwa sana kwani wananchi hawatakuwa na imani tena na serikali yao iliopo madarakani,” alisema
Loisulie.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha California Berkeley nchini Marekani, Dk. Willy Makundi, alisema Waziri Mkuu alizungumzia kwa ujumla bila ya kutaja hatua maalum za kumchukulia kila mtuhumiwa kwenye sakata hilo.
Prof. Makundi ambaye kwa sasa anaishi mjini Moshi, alisema ukimya wa Pinda utawafanya wananchi na wabunge wanaopigania matumizi bora ya rasilimali za taifa kukosa imani na serikali.
“Vijana walio na tabu nyingi za ajira na kipato wakiona mabilioni yanavyotumiwa visivyo au kuibwa bila mtu yeyote kuwajibishwa, basi watakuwa rahisi zaidi kushaurika kujiunga na upinzani,” alisema.
Alisema waziri kujiuzulu ni ishara nzuri ya uwajibikaji wa kisiasa na kwamba kama waliobaki hawatapanguliwa basi tatizo halitakuwa limepona.
MCHEZO WA KUIGIZA
Aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, amesema kitendo cha Pinda kushindwa kutoa majibu ni kama mchezo wa kuigiza.
Kadhalika, Dk. Lwaitama alisema mbali ya kitendo hicho kuonekana kama maigizo, lakini pia kwa mara nyingine kimemdhalilisha Pinda na kuonekana hana maana.
Alisema kama angekuwa yeye angejiuzulu na kwamba Pinda anaogopa kufanya hivyo kutokana na kuwa mtoto wa mkulima.
Aliongeza kuwa licha ya Pinda kudhalilishwa, lakini pia alijaribu kujiongezea madaraka asiyokuwa nayo baada ya kusema kuwa hajapokea barua za mawaziri, wakati anajua barua zikiandikwa zinatakiwa kwenda kwa Rais na wala siyo kwake.
“Ningekuwa na sifa za kuwa Waziri Mkuu halafu hili likatokea ningejiondoa na wala nisingesubiri kudhalilishwa namna hii,” alisema.
“Pinda anaonewa bure na kudhalilishwa bila sababu kwa sababu yeye hana mamlaka ya kuwaondoa kazini mawaziri licha ya kuwa ni mkuu wa shughuli za serikali bungeni,” alisema Dk Lwaitama.
PONGEZI KWA WABUNGE
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema serikali iliamua kuzima hoja za wabunge ili kulinda heshima yake na kwamba kama ingechukua hatua kwa mawaziri wake wapinzani wangepanda chati.
Hata hivyo, Dk. Bana aliwapongeza wabunge kwa kuibua hoja nzito kama ile na kwamba wameweka historia katika nchi hii kwani haijawahi kutokea.
Alionya kuwa ikiwa serikali itakaa kimya, Bunge la bajeti lijalo msuguano utakuwa mkali na hata baadhi ya vitu ikiwemo bajeti za serikali zinaweza kukwamishwa.
TUCTA MAANDAMANO YAJA
Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limecharuka na kumtaka Rais jakaya Kikwete kuwawajibisha mawaziri waliotajwa na kamati za kudumu za Bunge kuwa ni wabadhirifu wa mali za umma, vinginevyo wataandaa maandamano ya nchi nzima kumshinikiza.
Naibu Katibu Mkuu wa Ticta, Hezron Kaaya, alisema rais anatakiwa kuwawajibisha mawaziri hao kwa kuwa wamekuwa wabadhirifu wa mali za umma na kusababisha Watanzania wengine wawe na maisha magumu.
Alisema Rais anatakiwa kuacha kuwalea viongozi wabadhirifu, aliahidi kuwa Tucta wataanza mapambano dhidi ya viongozi wabadhirifu wa mali za umma kwa kuwataja hadharani.
Imeandikwa na John Ngunge, Arusha; Ashton Balaigwa, Morogoro; George Ramadhan, Mwanza; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Godfrey Mushi, Iringa; Jacqueline Massano, Dodoma; Salome Kitomari, Moshi; Richard Makore na Jimmy Mfuru, Dar.