Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanaohamia Chadema ni kwa hiari yao -Mbowe

7th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema hajawahi kufanya dili yoyote kati yake na Rais Jakaya Kikwete au Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), ili kuwavua magamba wanachama wa CCM na kuwavesha magwanda.

“Sina dili na Lowassa, sina mpango na Lowassa wala Rais Jakaya Kikwete na hawawezi kuninunua…CCM hawana ujanja wa kuinunua Chadema,” alisema.

Mbowe juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa NMC jijini hapa, ambapo wanachama na viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka CCM walitambulishwa rasmi kuwa wamejivua magamba na kuvaa magwanda.

Akihutubia maelfu ya wanachama hao, kuhusu operesheni ya chama hicho ya ‘Vua gamba, Vaa gwanda,’ Mbowe,  alisema “makamanda njooni Chadema…huku hakuna msosi wala rushwa bali ni mzigo tu wa kuwakomboa Watanzania na kuwaletea maendeleo.”

Alisema Chadema kimewapokea kwa mikono miwili aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Mkoa wa Arusha, James Ole Millya na wenzake.

Alisema hatua ya kuwapokea makada hao wa CCM ilipokelewa kwa hisia tofauti huku baadhi wakidai kuwa huenda ametumwa na  Lowassa, kwa lengo la ama kukipeleleza chama hicho au kukinunua.
 
Alisema Millya ni mtu safi na ndio maana chama chake kimempokea na akawafafanua sio vibaya kwa wanaojivua magamba na kuamua kuvaa magwanda.

Alisema ujio wa akina Millya kutoka CCM ni maamuzi waliyofanya wenyewe na hakuna dili lolote lililofanyuwa kati yake na Rais Kikwete au Lowassa.

Huku akitoa mifano michache, Mbowe alisema hatua hiyo sio ya kwanza kwani ilishawahi kutokea kwa Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye ni Rais wa mioyo ya Watanzania, Dk. Wilbrod Slaa  na Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje ambao awali walikuwa CCM wakati Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi alikuwa TLP kabla kuvua gamba na kuvaa gwanda.

Hata hivyo, Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, amemkosoa Mbowe na kumshauri kuwa mwangalifu juu ya kauli anazozitoa hadharani, kwani baadhi zinapotosha wananchi.

Nape alisema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya Mbowe juzi kutangaza hadharani kwamba kuna wabunge 70 na mawaziri saba wameomba kujiunga na Chadema.

Alisema hayo kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) alioutuma kwa mwandishi baada ya kutakiwa na NIPASHE kutoa maoni ya CCM kuhusiana na kauli hiyo ya Mbowe.

Nape alisema katika hali ya kawaida kama yaliyosemwa na Mbowe yangekuwa kweli asingeyasema hadharani.

“Ni sawa na mtu anayetaka kupigana akijua atapigwa anapiga kelele akidai ashikwe asiue,” alisema Nape.

Aliongeza: “Namshauri Mbowe aonyeshe anastahili kuwa mwenyekiti wa chama na kiongozi wa upinzani bungeni. Asipoangalia watu watamtafsiri vinginevyo.”

Baadhi ya vyombo vya habari Mbowe jana (sio NIPASHE), vilimkariri Mbowe akieleza kuwa wabunge 70 wa CCM wameomba kujiunga na Chadema.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles