Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Azam, Mtibwa kurudiana leo Taifa

4th May 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah

Mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya Azam na Mtibwa Sugar ya Manungu Morogoro ilivunjika katika dakika ya 88 kwenye Uwanja wa Chamazi sasa itarudiwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kufuatia maamuzi ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi iliyo chini ya Kamanda Mstaafu, Alfred Tibaigana.

Maamuzi hayo yamefikiwa baada ya kamati hiyo kujiridhisha kuwa refa Rashid Msangi wa Dodoma ndiye aliyekuwa na makosa ya kuvunja mchezo na kushindwa kufuata taratibu za kumaliza mechi.

Awali Kamati ya Ligi iliamua kuipa Azam pointi 3 na magoli 3 huku ikiitoza Mtibwa Sugar faini ya Sh. 500,000 na kuinyima mapato ya mechi hiyo lakini Aprili 29 klabu ya African Lyon iliamua kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Angetile Osiah, alisema kuwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi iliyokaa juzi Mei 2 iliamua mchezo huo urudiwe kwa sababu ilijiridhisha kwamba mwamuzi ndiye aliyekuwa na mapungufu hivyo kuipa Azam ushindi na kuitoza faini Mtibwa Sugar ni sawa na kuionea.

Osiah alisema kuwa Kamati hiyo ya Tibaigana ilifanya maamuzi hayo kwa kuzingatia kanuni ya 56 ya FIFA ambayo inaeleza endapo mchezo haukumalizika kutokana na sababu ambazo si za majanga, itabidi mchezo huo urudiwe.

Alisema pia maamuzi hayo yametajwa pia kwenye kanuni ya 31 (1) ya FIFA kwamba endapo hakutakuwa na timu iliyofanya utovu wa nidhamu mechi itarudiwa na si kuipa ushindi timu mojawapo kama ilivyoamuliwa na Kamati ya Ligi.

Osiah alisema kwamba kutokana na maamuzi hayo mechi hiyo imeamuliwa kufanyika kwenye uwanja usio wa nyumbani wa timu hizo mbili.

Katibu huyo alieleza kwamba katika rufaa ya African Lyon ilieleza kuwa hawana imani na wajumbe wa Kamati ya Ligi kwa sababu wanafanya maslahi kwa kuzingatia timu walizotoka jambo ambalo si sahihi kwa sababu maamuzi yote yanazitangia kanuni na kuongeza kuwa wanaweza kukata rufaa endapo hawataridhika na maamuzi hayo.

Msemaji wa Azam, Jaffer Iddi, alisema kuwa klabu yake imekubaliana na maamuzi hayo na kwa sababu ilianzishwa kwa lengo moja la kucheza soka.

Iddi alisema kuwa wanaamini kuwa ndoto yao ya kutwaa ubingwa bado iko pale pale na hakuna kitakachowarudisha nyuma.

Kutokana na maamuzi hayo sasa Azam inashuka dimbani ikiwa na pointi 53 na iko kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi wakati Mtibwa Sugar yenyewe ni ya nne na imejikusanyia pointi 36.

Simba ndio vinara wa ligi hiyo kutokana na kuwa na pointi 59 ambazo zinaweza kufikiwa na Azam endapo itashinda mechi ya leo na ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar hapo Jumapili.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles