Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Shibuda akalia kaa Chadema

17th May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda

Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema (Bavicha), limemjia juu Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, kwa kutangaza kwamba, atagombea urais kupitia chma hicho na meneja wake wa kampeni atakuwa Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kwa kauli hiyo, Bavicha imewataka vijana wote wa Chadema kukabiliana na Shibuda kwa madai kwamba ameonekana kuwa ni kikwazo kwa chama hicho katika kuelekea kuchukua dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

“Natoa wito kwa vijana wote wa Chadema kuwa sasa tujiandae kikamilifu katika kukabiliana na mtu yeyote yule ambaye ataonekana kuwa kikwazo kwa chama chetu, matumaini na maslahi ya Watanzania kwa ujumla wake katika kuelekea kuchukua dola mwaka 2015,” Bavicha imesema kupitia tamko lililosambazwa kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa kompyuta jana.

Tamko hilo lilitolewa na Bavicha kupitia Mwenyekiti wake Taifa, John Heche, limesema kuwa wamepokea kwa mshituko mkubwa kauli ya Shibuda hasa kutokana na kuitoa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alitaja sababu za kupokea kwa mshituko kauli hiyo ya Shibuda kuwa ni pamoja na kumtangaza Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kuwa ndiye atakayekuwa meneja wa kampeni zake katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania urais.

Sababu nyingine ni kwa kutamka kwamba hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuiongoza nchi kwa sasa na kutoa matamshi hayo kwa niaba ya Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

“Mambo hayo manne ndio yametushtua na kutufedhehesha sisi vijana wa Chadema na ndio maana tumelazimika kutoa kauli kuhusiana na suala hili,” alisema Heche na kuongeza kuwa kamwe Bavicha hawataruhusu mgombea urais wa Chadema meneja wake wa kampeni awe ni Mwenyekiti wa CCM hata siku moja.

Heche alisema Chadema inao watu wa kutosha na wenye uwezo wa kutosha kuifanya kazi hiyo na hawahitaji msaada huo.

Alisema pia kuwa kamwe hawataruhusu mgombea urais wa Chadema awe anatangaza nia kwenye vikao vya CCM kwa vile haina mamlaka ya kumteua mgombea wa Chadema.

“Na kama Shibuda alikuwa halijui hilo anapaswa kulifahamu kuanzia sasa kuwa vijana wa Chadema hatuchaguliwi mgombea na NEC ya CCM kwani Chadema kuna vikao na taratibu zetu za kuteua wagombea,” alisema Heche.

Alisema kitendo cha Shibuda kusema kuwa hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuongoza nchi ni kuwadhalilisha vijana wa Chadema na Watanzania wote.

Heche alisema vijana wa Chadema na Watanzania wote hivi sasa wanakiona chama hicho kama tumaini pekee la kuwakomboa.

Alisema vijana wa Chadema wanaamini kuwa mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuiachia kauli ya namna hiyo iachwe bila kutakiwa maelezo ya kina.

Kutokana na hilo, alisema wataitisha kikao cha Baraza na kuijadili kauli hiyo na kuwasilisha mapendekezo yao kwenye vikao halali vya chama.

Alisema kama Shibuda anaona kuwa haendani na utamaduni wa Chadema na anaiona haina uwezo wa kuongoza dola anafanya nini kwenye chama ambacho anaona kuwa hakiwezi kuongoza dola?

“Kwanini atafute urais kwenye chama ambacho anaona hakiwezi kuongoza dola? Anawatania Watanzania?” alihoji na kusema kuwa ni heri akaenda kwenye hicho ambacho anaamini kuwa kinaweza kuongoza dola, kwani lengo la chama chochote kile ni kuchukua dola na siyo vinginevyo.

Alisema Chadema kimejiandaa kikamilifu kuongoza dola na kuwataka vijana na Watanzania wote kutokuwa na hofu na maneno yaliyotamkwa na mbunge huyo.

Shibuda alitangaza azma yake hiyo Jumatatu wiki hii mbele ya wajumbe wa NEC ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na APRM.

Shibuda ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo anayewakilisha vyama vya upinzani.“Nakupa pole, kazi ya urais ni ngumu sana, bila shaka utakumbuka kuwa nami nilitaka kuwa mbadala wako, hata hivyo naamini utakuwa meneja wangu wa kampeni za urais mwaka 2015,” alisema Shibuda akimweleza Rais Kikwete.

Huku wajumbe wa NEC wakishangalia, Rais Kikwete alimwuliza: “Unataka urais kupitia chama gani?” Shibuda akajibu kwa kujiamini: “Kupitia Chadema, huku niliko sasa.”
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment