Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ni utoto Ngassa kuvaa jezi ya Yanga

28th July 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika Mashariki na Kati linafika kilele leo kwa timu mbili za Bara kukutana katika fainali kama ambavyo yalikuwa matakwa ya shirikisho la mchezo huo (CECAFA).

Tulishuhudia katika wiki mbili za michuano hii timu za nyumbani, hasa Simba na Yanga, zikionekana dahiri kubebwa ili zipate matokeo mazuri ndani ya uwanja na ikiwezekana, kama ambavyo ilikuwa mwaka jana, zicheze tena fainali leo.

Angalau, basi, mikakati ya CECAFA imefanikiwa kwa kiwango fulani na patakuwa na watazamaji wa kutosha kiasi katika pambano hilo kuliko kama ambavyo Yanga nayo ingetolewa mapema kama Simba.

Je, watazamaji wa kutosha kiasi hao leo watashuhudia Mrisho Ngassa aakivaa na kubusu jezi ya Yanga kama alivyofanya katika mchezo wa kwanza wa nusufainali kati ya Vital na Azam juzi?

Azam, kama klabu, imelipuuzia jambo hilo na kusema ni kitu cha kawaida.

Ni kitu cha kawaida kweli kama ambavyo Azam imesema lakini katika misingi ya uungwana, Ngassa ni msaliti na ni mchezaji ambaye alistahili kukemewa na benchi la ufundi la timu ya washindi hao wa pili wa ligi kuu ya Bara msimu uliopita.

Mafanikio katika timu ya soka huletwa na mambo kadhaa yanayokwenda pamoja, na cha msingi zaidi katika hayo ni mshikamano kikosini.

Kama kikosi hakina mshikamano baina ya wachezaji ndani na nje ya uwanja, ni vigumu timu kama hiyo kupata mafanikio kama ambayo Azam ilipata mwaka jana ilipokaribia kutwaa ubingwa wake wa kwanza wa Bara miaka mitano tu tangu iwe timu ya ligi kuu.

Kwa sababu wachezaji wa Azam ni kikosi kilicho na mshikamano miogoni mwao, vinginevyo timu isingepaa kiwango ilichofikia msimu uliopita, Nipashe tunaona kitendo cha Ngassa kinatishia ustawi na kuendelea kuwepo kwa umoja huo wa wachezaji.

Kwa sababu hiyo, basi, ni mategemeo yetu kuwa kocha Stewart Hall angalau atamuonya mchezaji huyo kuacha utoto wa kuvaa jezi za timu pinzani kwa lengo la kuonyesha mapenzi kwayo.

Tunafahamu Nipashe kwamba Azam inafahamu kuwa Ngassa alivaa jezi hiyo ama kwa hasira, ama kama moja ya mikakati yake ya kuona anarudi Jangwani hata msimu huu baada ya kukosa namba katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ya Chamazi.

Lakini, anachotakiwa kufanya Ngassa, Nipashe tunaona, ni kujibiidisha katika mazoezi ili kurudisha namba ambayo alikuwa nayo wakati akinunuliwa kwa zaidi ya sh. milioni 50 miaka miwili iliyopita.     

Kulazimisha kurudi Yanga, kimsingi, ni kujimaliza kimchezo kwa winga ambaye aliwahi kuchukuliwa kuwa mchezaji mwenye nafasi kubwa zaidi ya kuwa wa kwanza nchini kucheza soka la kulipwa, la kueleweka, katika moja ya klabu kubwa za Ulaya.

Ni kujimaliza kimchezo kwasababu anachotakiwa kufanya Ngassa, Nipashe tunaona, ni kubaki Azam na kuhakikisha anapigania namba ambayo ameporwa na Kipre Tche Tche wa Ivory Coast ambaye uchezaji wao usingeweza kuwa tofauti zaidi ya ulivyo sasa.

Tche Tche ana nguvu kuliko Ngassa, kwanza, jambo ambalo liliwahi kuelezwa kuwa kasoro kwake baada ya winga huyo wa Taifa Stars kurudi kutoka kufanya majaribio katika klabu ya West Ham ya Uingereza.

Tche Tche pia hufanya majaribio mengi ya kufunga mchezoni kuliko Ngassa.

Aidha, Tche Tche ni mshambuliaji kama Ngassa, lakini katika soka la kisasa washambuliaji pia wana jukumu la ziada la kusaidia kazi ya ulinzi katika timu kama ambavyo walinzi na viungo hufunga magoli; jukumu ambalo si lao la msingi.

Tche Tche hurudi nyuma kila timu yake inapopoteza mpira kumsaidia beki wake wa pembeni kukaba, tofauti na jitihada zinazoonyeshwa na Ngassa.

Hivi ni baadhi tu ya 'vitu' ambavyo Ngassa alipaswa kuviiga mazoezini na kuvifanya kwa kiwango cha ziada ili kupata tena namba yake badala ya kutaka kwenda Yanga na kutarajia kuwa huko atapata namba kwa tu kubusu jezi ya timu hiyo alipokuwa Azam.

Ni imani yetu, Nipashe, kwamba kinachomkuta Ngassa sasa Azam kitamkuta pia Yanga kutokana na ubora wa walimu wa timu zote kuwa wa kiwango sawa.

Kama ambavyo Hall amekaririwa akisema analazimika kumpiga benchi Ngassa kwa sababu haridhishwi na kujituma kwake katika mchezo, ndivyo ambavyo tumemsikia Tom Saintfiet akimkosoa Jerry Tegete, mshambuliaji ambaye ana kila sifa ya kuwa chaguo la kwanza katika safu ya mbele ya Yanga lakini akalazimika kutupwa benchini baada ya mechi ya ufunguzi wa Kombe la Kagame kutokana na kutofanya majukumu ya ziada katika timu -- kama Ngassa.
   

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment