Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tanroads Dar wanamkwaza Magufuli

9th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye hana wa kufanana naye katika uchapakazi kwenye baraza jipya la mawaziri na lililopita kutokana na kujituma kwake, alifanya ziara jijini Dar es Salaam kukagua maendeleo ya miradi miwili mikubwa, kwanza ujenzi wa barabara ya New Bagamoyo kipande cha Mwenge hadi Tegeta ambayo inapanuliwa kuwa njia nne.

Kadhalika siku hiyo Magufuli alitembelea mradi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi maarufu kama Dart, ambao unalenga kupunguza masongamano uliokithiri wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Huu ni mradi utakaogharimu takribani Sh. bilioni 39.6 ukihusisha ujenzi wa njia za kupita juu kwenye makutano ya barabara katika jiji la Dar es Salaam.

Waziri huo kama ambavyo imekuwa ni kawaida yake katika uwajibikaji, alitaka kujua maendeleo yaliyofikiwa katika mitadi hiyo, lakini pia kujua changamoto zinazowakabili wakandarasi wanaoendesha kazi hiyo, ili asaidie kusukuma mambo kwa nia ya kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa kulingana na mpango wake wa kazi.

Ni katika ziara hiyo, Waziri Magufuli alilitaka Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kuondoa nguzi za umeme eneo la barabara ya Dart ili kusaidia juhudi za kufanikisha kazi hiyo, alitoa siku saba kwa shirika hilo la nishati kuhakikisha kazi hiyo inatekelezwa, vinginevyo angeagiza Wakala wa Barabara (Tanroads) kuifanya bila kusita.

Aina ya utendaji kazi wa Magufuli ni wa kiongozi anayeshiriki kwa vitendo halisi kutembelea maeneo yake ya utawala, kutambua mwenyewe nini kinaendelea na kwa maana hiyo kutafuta majawabu ya changamoto anazokumbana nazo, hasubiri tu kupelekewa ripoti mezani ili abweteke kwamba mambo yanakwenda wakati hali ni kinyume chake kabisa.

Inajulikana wazi kuwa katika taifa hili miaka ya hivi karibuni wamezaliwa watendaji wa kizazi kipya, wajuzi wa kupika taarifa na ripoti, wajuzi wa kutoa matamko wakiwa wanapulizwa na viyoyozi maofisini, lakini wakiwa katika kiza kinene juu ya hali halisi ya mambo katika hayo yanayoletwa mezani kwao na kuyasoma kwa kukariri tu.

Unapokuwa na watendaji wa namna hii, hakika njia ya kuepuka kitanzi kama kile kilichoondoka na mawaziri sita hivi karibuni, ni kuwa kama Magufuli, kuondoka ofisini na kwenda kufanya ziara eneo la kazi kujithibitishia kama kweli kazi inafanyika, na inafanyika kwa kiwango gani.

Huu ni utendaji wa Kimagufuli, ambao tunaamini wale wote anaowasimamia wangeiga mfano wake.

Kwa mshangao mkubwa kabisa, baadhi ya watendaji walio chini ya Magufuli wanashindwa kuelewa hasa nini kinaendelea katika staili ya usimamizi wa bosi wao, bado wapo watumishi wanaopaswa kuwa nje ya ofisi wakikaguza kazi zinazofanywa je, lakini wamejifungia ofisini wakisubiri ripoti.

Mfano mmojawapo ni Tanroads mkoa wa Dar es Salaam, ofisi hii ina barabara nyingi inazosimamia, mojawapo ni hii inayoanzia Mbezi Kwa Yusufu, kwenda Mpigi Magoe kupitia Hifadhi ya Pande hadi Boko, ikunganisha barabara ya Morogoro na New Bagamoyo. Ni barabara muhimu na kiungo kikubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, ikiwa inahudumia pia na taasisi nyingi za kijamii.

Ukiacha usanii ambao Tanroads imeacha ufanywe mwaka baada ya mwaka kwa wanaopewa kazi ya kuitengezeza kwa kupitisha tu greda juu na kushindwa kabisa kujenga mitaro, hivyo kuacha barabara hiyo ikimomonyolewa na mvua kila wakati, sasa wamevunja rekodi kwa kumwaga kifusi ambacho hakifai kuwa barabarani katika eneo la barabara hiyo.

Kifusi hiki kibaya kimemwagwa na tipa umbali mrefu, hakijatandazwa baada ya kuibuka kwa malalamiko ya wananchi wanaotumia barabara hiyo, mvua zilizonyesha wiki iliyopita barabara hiyo iligeuka kuwa kitu cha ajabu, ni janga.

Tunataja barabara hii kuonyesha mfano mmojawapo hai wa watendaji kukaa ofisini na kuacha vitu vya ajabu vikitokea katika maeneo ambayo wanapaswa kusimamia.

Kama kweli kuna mkandarasi alipewa kazi ya kuweka kifusi kipya juu ya barabara hii, swali linaloibuka hapa inakuwaje anamwaga kifusi ambacho kitaalam hakiruhusiwi kuwa barabarani?

Kuna usimamizi gani hapa? Kwa nini watendaji wa Tanroads Dar es Salaam hawataki kufuata nyayo za bosi wao, Waziri Magufuli?

Tunasema wazi, cheo ni dhamana, na dhamana hii ni lazima ifanye kazi, si vema kuwa na watendaji wasiofaa na ambao wanakaa ofisi kusubiri kupelekewa taarifa za kupika wakati wananchi wanaumia.

Ni kwa jinsi hii tunamwambia Dk. John Pombe Magufuli, watendaji wa namna ya Taroads Dar es Salaam wanakwaza uwajibikaji wako usiotiliwa shaka.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles