Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Hakika Shilingi inahitaji mkombozi

16th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Juni 30, mwaka jana wakati mwaka wa fedha wa 2010/11 ukifika ukingoni na kuashiria kuanza kwa mwaka mpya wa fedha wa 2011/12, tuliandika tahariri iliyobeba kichwa kisemacho ‘Hatua dhabiti zichukuliwe sasa kuiokoa Shilingi dhidi ya Dola.’

Tulisema hivyo wakati huo kwa sababu tulikuwa tumeshuhudia thamani ya Shilingi ikizidi kuporomoka kwa kiwango kikubwa hali ambayo iliathiri mipango mingi ambayo imo kwenye bajeti ya serikali na hata mtu mmoja.

Wito wetu ulilenga kuwataka wote wenye wajibu wa kusimamia sekta ya fedha kuchukua hatua za kunusuru sarafu ya Tanzania. Hata hivyo, wito wetu haukutiliwa maanani na yeyote, si Hazina wala Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ndiyo maana hadi sasa bado changamoto hiyo inaandama sarafu ya Tanzania.

Ukitazama kwa makini, thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola kwa takribani mwaka mmoja uliopita haijawa na nafuu yoyote ya maana, wakati mwaka wa fedha wa 2011/12 unaanza Dola moja ya Marekani ilikuwa ikibadilishwa kati ya Sh. 1,600 na Sh. 1,620 leo hii tunapokaribia kufunga mwaka wa fedha wa 2011/12 hali haina tofauti kubwa kwani iko kati ya Sh. 1,583 na Sh. 1,584, na dalili zinaonyesha kuwa mwelekeo ni kuzidi kuporomoka kwa sarafu yetu.

Zipo sababu nyingi zinazoelezea hali hii, kubwa ni mahitaji makubwa ya Dola ya Marekani kwa ajili ya kununua bidhaa na huduma mbalimbali ikilinganishwa na uwezo mdogo wa shughuli za kiuchumi katika kuzalisha dola hizo. Hii ni pamoja na uuzaji mdogo wa bidhaa nje ya nchi kuliko mahitaji makubwa ya bidhaa hizo kutoka nje.

Hali ya kuzidi kuporomoka kwa thamani ya Shilingi ndiyo imemfanya Waziri mpya wa Fedha, Dk. William Mgimwa, kuahidi kuwa serikali itaanza kutekeleza mkakati wa kulinda thamani yake na kueleza kuwa wanakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kwamba matumizi yote ya fedha na mahitaji ya nchi yanafanyika kwa Shilingi ya Tanzania badala ya Dola ya Marekani ili kuliepusha taifa kuendelea kuathiriwa na kushuka kwa thamani ya fedha yake.

Waziri huyo alisema  taifa lipaswa kuhimiza zaidi matumizi yote na mahitaji ya nchi yafanyike kwa Shilingi ya Tanzania badala ya Dola na kwamba BoT imezipa maelekezo taasisi za fedha na mabenki kupunguza kiwango kilichokuwa kimeruhusiwa kuweka akiba (deposit) ya fedha za kigeni kutoka asilimia 20 hadi kufikia asilimia 10.

Aliainisha mkakati mwingine kuwa ni serikali kujikita katika kuuza bidhaa nyingi nje ya nchi kuliko uagizaji, kuwashauri wawekezaji waliopo nchini na wanaokuja kutumia fedha za Tanzania badala ya Dola ili kuimarisha Shilingi.

Ingawa mawazo na pengine mikakati ya serikali inaweza kuwa mizuri katika kuikoa sarafu ya taifa hili, bado hisia za ama kupuuzwa au kukosekana utashi na mikakati enedevu ya kuimarisha Shilingi zimekuwa na nguvu mno kiasi cha kujenga hoja kwamba hata sasa bado wenye wajibu wa kuchukua hatua hizi hawajawa tayari kutimiza dhima hii ili kuleta mabadiliko ya kweli katika uchumi wa taifa hili.

Kwa bahati mbaya sana tangu kufunguliwa kwa milango ya uchumi, chini ya soko huria, kumekuwa na maoni mbalimbali juu ya njia za kuilinda sarafu ya Tanzania dhidi ya mahitaji makubwa ya Dola, lakini walioko madarakani ama wamekuwa na kigugumizi kuyachukua na kuyafanyia kazi. 

Mathalani, tabia ya  baadhi ya watoa huduma na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kupanga bei zao kwa Dola za Marekani hakika kunaongeza shinikizo kwa sarafu ya nchi hii bila sababu.

Uagizaji wa vitu kutoka nje ambavyo huhitaji Dola ya Marekani wakati kimsingi havina maana, tija na wala havisaidii juhudi za taifa hili kupambana na umasikini mbali tu ya kuongeza mahitaji makubwa ya Dola hivyo kuzidi kuikandamiza Shilingi.

Kama ambavyo tulisema mwaka jana, leo tena tunasema kwamba ukitembea kwenye maduka mengi nchini hakika unapigwa butwaa kama kweli kuna uhalali wowote wenye tija kuingiza nchini bidhaa kama mapambo na wanasesere wa plasitiki, vifaa vingine chakavu vya nyumbani kama vyombo, samani za maboksi ambazo hakika haziwezi kudumu hata mwaka mmoja kwa kutumia Dola za Marekani ambazo kimsingi zingehitajika kwa ajili ya kuingiza vitu muhimu na ambavyo hakika haviwezi kupatikana hapa nchini.

Tunahisi labda Waziri Mgimwa ametambua ukweli wa jambo hili na kwa maana hiyo sasa atasaidia kusukuma mbele mikakati ya kutuoandoa kwenye ugonjwa huu wa kutumia Dola ya Marekani bila ulazima wowote, kwa kufanya hivi Shilingi inaweza kusalimika.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles