Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mwenyekiti kamati ya ligi aliyejizulu, amtaka Tibaigana aombe radhi

31st March 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa kamati ya Nidhamu na Usuluishi, Alfred Tibaigana

Wakati hatma ya wachezaji wa Yanga waliokuwa wamefungiwa na Kamati ya Ligi kuu ya Bara ikitarajiwa kujulikana Jumanne katika kikao cha kamati ya Nidhamu na Usuluishi, Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ligi iliyotoa adhabu kwa wachezaji hao, Said Salim aliyetangaza kujizulu juzi nafasi hiyo amemtaka Mwenyekiti wa kamati ya Nidhamu na Usuluishi, Alfred Tibaigana kuomba radhi.

Salim amemtaka Tibaigana aombe radhi kwa wadau wa soka na wajumbe wa kamati hiyo ya Ligi kwa kitendo chake cha kuwaita 'wanasiasa' kufuatia maamuzi yao ya kuwapa adhabu wachezaji hao wa Yanga.

"Tibaigana ni lazima atuombe radhi sisi (Kamati ya Ligi) na wadau wa soka kwa ujumla kwa matamshi yake ambayo si ya kiuwanamichezo," alisema Salim.

 

Alisema, Tibaigana aliidharau kamati hiyo kwa kusimamisha adhabu waliyokuwa wameitoa kwa wachezaji wa Yanga waliokuwa wamevunja kanuni za soka kwa kumpiga mwamuzi Israel Nkongo. 

 

Katika hatua nyingine hatma ya wachezaji hao wa Yanga walisitishiwa adhabu zao kwa muda sasa itajulikana Jumanne katika kikao cha Kamati ya Nidhamu na Usuluishi ya Kamanda Tibaigana.

Awali, kikao hicho kilikutana juzi chini ya mwenyekiti Tibaigana lakini hakikutoa maamuzi kwa kuwa pande mbili za Yanga na Kamati ya Ligi hazikufika kwenye kikao hicho.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Afisa Habari wa Shirikisho la soka (TFF), Boniface Wambura alisema hatma ya wachezaji Stephano Mwasika na wenzake wanne waliofungiwa itajulikana Jumanne baada ya kikao cha pamoja cha pande tatu hizo.

"Awali tulitegemea maamuzi na hatma ya wachezaji wale wa Yanga waliofungiwa ingepatikana jana (juzi) baada ya kikao cha kamati ya Tibaigana lakini sasa maamuzi yatatolewa Jumanne baada ya kikao cha pamoja," alisema Wambura.

Alisema kuwa kulikuwa na dosari baada ya taarifa za kikao hicho kushindwa kuwafikia Yanga na Kamati ya Ligi.

Aidha, alisema kuwa tayari pande zote zimetaarifiwa juu ya kikao hicho kitakachofanyika Jumanne ambapo zimetakiwa kufika na vielelezo.

Wambura alisema kuwa Sekretarieti ya TFF imeshakusanya vielelezo vyote vinavyotakiwa kwa ajili ya utetezi wa uamuzi wa kuwafungiwa wachezaji hao wa Yanga ambao walihusika katika vurugu za kumpiga mwamuzi wa mchezo dhidi ya Azam FC Israel Nkongo, uliochezwa Machi 10 Uwanja wa Taifa.

Mbali na Mwasika aliyefungiwa kucheza mpira kwa mwaka mmoja pamoja na kulipa faini ya sh. milioni moja kabla ya Kamati ya Tibaigana kusimamisha, wachezaji wengine ni:

Nadir Haroub 'Canavaro' na Jerry Tegete waliokuwa wamefungiwa kucheza michezo sita pamoja na faini ya sh. laki tano kila mmoja, na Omega Seme na Nurdin Bakari waliokuwa wamefungiwa kucheza michezo mitatu pamoja na faini ya sh. laki tano kila mmoja.

Kufuatiwa kutotolewa kwa maamuzi kwenye kikao cha kamati ya Tibaigana kilichofanyika juzi, wachezaji hao wanaweza kucheza mchezo wa leo wa ligi kuu ya Bara dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga.

Wachezaji hao walishakosa michezo miwili dhidi ya Villa Squad na African Lyon ambapo katika michezo hiyo yote Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi unaofanana wa goli 1-0.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles