Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Shibuda kutimuliwa Chadema?

21st May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda

Sakata la Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), John Shibuda kutangaza kwamba atagombea urais mwaka 2015 kupitia chama hicho na kumuomba Rais Jakaya Kikwete awe meneja wake wa kampeni sasa limechukua sura mpya baada ya Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) kuanza vikao vya kumjadili wiki hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, Shibuda ataanza kujadiliwa Alhamisi wiki hii kupitia vikao halali vya baraza hilo na mapendekezo yao yatapelekwa kwenye vikao vya juu vya chama.

Alisema Bavicha wamefikia hatua hiyo baada ya mashauriano na Katibu wake Deogratias Siale, viongozi wengine na wanachama.

Aliwataka wanachama wa Bavicha kuwa wavumilivu wakati Baraza likianza kuchukua hatua dhidi ya kauli hiyo ya Shibuda.

Hivi karibuni Shibuda akiwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), mjini Dodoma alitangaza kwamba atagombea urais na kwamba meneja wa kampeni zake za atakuwa ni Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete.

Bavicha walisema kupitia kikao hicho, Shibuda alivishambulia vyama vya upinzani na kusema kuwa ni dhaifu na kwamba haviwezi kuongoza nchi hii ili hali yeye mwenyewe akiwa ni mwanachama tena mbunge
wa chama cha upinzani.

Heche alisema kauli hiyo iliwasikitisha wao kama vijana na kwamba lazima ijadiliwe na kuchukuliwa hatua za haraka.

Alifikia hatua ya kutoa kauli ya Bavicha baada ya  kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa Baraza hilo katika maeneo mbalimbali nchini.

"Nilieleza pia kuwa kama vijana ndani ya chama hatuwezi kuvumilia vitendo vya mtu yeyote ambavyo vinaonekana kuwavunja moyo mamilioni ya Watanzania, ambao wana matumaini na (Chadema).

Katika taarifa hiyo Heche alieleza kwamba mamlaka za nidhamu hazitakaa kimya na kuziachia kauli za namna hiyo ziendelee kutolewa.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles