Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Jumatano mwisho usajili Airtel Rising Stars

21st May 2012
Print
Comments

Usajili wa wachezaji kwa ajili ya michuano ya Airtel Rising Stars 2012 unatarajiwa kufikia tamati keshokutwa Jumatano kwa mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Arusha, Mbeya na Arusha. Jumla ya timu 24 zinatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo ngazi ya mikoa na hatimaye taifa itakayofanyika mwezi Julai Jijini Dar es Salaam.

Mikoa shiriki ilichanguliwa kutokana na kufanya vizuri kwenye michuano ya taifa ya Shule za Sekondari (UMISSETA) iliyoisha hivi karibuni. Uzinduzi rasmi wa Airtel Rising Stars 2012 ulifanyika hivi karibuni chini ya mchezaji wa zamani wa Manchester United ya Uingereza, Quinton Fortune kwenye Hoteli ya Sea Cliff, Dar es Salaam.

Timu sita za wasichana zitashiriki kwenye ngazi ya taifa.

Akiongea kuhusu wasichana kushiriki kwenye michuano hiyo, Mkurugenzi wa Masoko Airtel Tanzania, Cheikh Sarr, alisema: "Airtel imeamua kujumuisha wasichana kwenye michuano hii ili kuwapa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao na pia kuipa timu ya taifa ya wanawake ya Twiga Stars fursa ya kupata vipaji vipya.

Wakati wavulana wakitarajiwa kushindana kuanzia ngazi ya mkoa ili kuchanguliwa kupata nafasi ya kucheza taifa, timu moja ya wasichana kutoka kila mkoa itashiriki moja kwa moja fainali za taifa na hivyo kufanya timu 12 kushiriki katika ngazi hii ambapo sita ni za wavulana na sita wasichana.      

Akizungumzia sababu ya Airtel Tanzania kuwekeza kwenye soka, Cheikh Sarr, alisema: "Tunajisikia furaha kukuza vipaji vidogo kuanzia ngazi ya chini kabisa, huu ndio muda kila mtu alikuwa akiusubiri. Ni muda mwafaka kwa Tanzania kuibua nyota wake."

Michuano ya ARS ngazi ya mkoa inarajiwa kuanza Mei 25, huku Dar es Salaam ikiwa na timu sita kutoka Kinondoni, Ilala na Temeke. Shule hizo ni Twiga, Goba na Makongo Sekondari (Kinondoni) Mbande, Kurasini na Kiravi Sekondari (Temeke) huku Ilala ikiwakilisha na Airwing, Benjamin Mkapa na Msongola Sekondari.

Shule nyingine zitakazoshiriki kwenye michuano hii ni Southern Highland Secondary, Mbeya High Sekondari na Wenda Sekondari (Mbeya), Lindi Sekondari, Mpunyule na Ngowe Sekondari (Lindi) huku Arusha ikiwakilisha na Sinoni Sekondari, Kaloleni na Bishop Durning Sekondari.

Michuano wa Airtel Rising Stars ni mpango kambambe kwa Afrika nzima ambao ni wa kutafuta na kukuza vipaji vya soka vinavyochipukia kwa wavulana na wasichana wenye miaka chini ya 17 ambao watapata muda wa kuonyesha vipaji vyao na kukutana na wataalamu wa mpira wa miguu ambao watawapa mafunzo zaidi na kupata nafasi ya kukuza vipaji vyao.

Airtel Rising Stars ni ushirikiano kati ya Airtel na klabu ya Uingereza ya Manchester United ya kukuza vipaji vya soka barani Afrika. Mwaka jana, klabu ya Manchester United ilitoa walimu wake wa soka ya vijana kuendesha kliniki ya soka ya kimataifa zilizofanyika Tanzania, Afrika Kusini na Gabon.

Kliniki nyingine kama hiyo itafanyika Nairobi, mwezi wa Agosti mwaka huu huku ikitanguliwa na michuano ya kimataifa itakayohusisha timu bingwa wa michuano ya Airtel Rising Stars.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles