Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tulisema `wameula`, sasa wamekula

29th April 2012
Print
Comments

Kama kuna kauli inayonikera wakati mawaziri na watendaji wengine wa serikali wanapoteuliwa, kisha kula kiapo cha utumishi ni ile inayosema, ‘fulani ameula.’

Kwamba kama ameteuliwa kuwa Waziri, basi ameula! Naibu Waziri, ameula! Katibu Mkuu, ameula! Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri, ameula!

Hata inapokuwa katika nafasi ya kuchaguliwa na umma kama udiwani, ubunge, urais utasikia ‘fulani ameula.’

Makada wa chama wanapoteuliwa kuwa Wakuu wa Wilaya, wameula! Wabunge walioshindwa katika uchaguzi na ‘kupozwa’ kwa ukuu wa mkoa, utasikia ‘ameula’!

Kila nafasi yenye majukumu mazito kwa utumishi wa umma, ile isiyohitaji kukimbiliwa hasa kama mhusika ni mtu mwadilifu, inakuwa nafasi ya kula…ameula!

Kauli hiyo imekuwa kichocheo cha wizi, kichocheo cha kubuni mbinu chafu za kuliangamiza taifa kupitia ufisadi, rushwa wizi na ubadhirifu mwingine wa mali za umma.

Tazama, hata inapotokea Rais anawaapisha mawaziri, mabalozi, makatibu wakuu ama mteuliwa yeyote, inakuwa ni sherehe.

Mathalani, utakuta wajawazito wanateseka wodini wakisubiri kujifungua pasipo uhakika wa huduma bora na ukosefu wa vifaa, panapofanyika sherehe za kuapishwa ‘wanaoula’ inakuwa ni ‘kutungua maisha’. Wanasherehekea.

Baada ya kula kiapo, wakiwa wamefuatana na wazazi wao, wenzi wao, marafiki zao, ndugu na jamaa zao, wanavishana mashada! Ya nini? Eti kupongezana!

Wanajitokeza, kwa mfano, mbele ya mlango mkubwa wa kuingia kwenye jengo la Ikulu, wanapiga picha na Rais. Hilo si tatizo.

Picha ni kwa ajili ya kumbukumbu, lakini zinapowekwa katika taswira ya kusherehekea ‘kuula’, inapoteza maana yake.

Hata wakishapiga picha, wateuliwa wanapongezwa, wanakumbatiwa kiasi cha kutoa vicheko wakiamini kweli ‘wameula.’

Wakitoka hapo wanakutana na wahudumu wanaogawa vinywaji laini kama soda na juisi, kila mtu anawekewa kwenye glasi na kusogezewa vitafunwa, inakuwa vicheko vitupu, watu wameteuliwa kuutumikia umma, ‘wameula’!

Lakini kwa uhalisia wake, watu walio waadilifu hawawezi kujiaminisha ama kusherehekea kwa namna yoyote baada ya kupewa jukumu zito la kuutumikia umma.

Kuutumikia umma kwa kufuata misingi ya maadili na utashi usiokuwa na nia ovu kwa nchi na watu wake, si jambo la kuchekelea, si jambo la kuanza kuvishwa mashada hata kabla ya kukiona kiti cha ofisi mpya, si jambo la kugonganisha glasi…hata kidogo!

Ni kama alivyowahi kutamka Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba mtu muadilifu hawezi kukimbilia utumishi wa umma, bali umma unapaswa kumkimbilia ili autumikie.

Kwa maana umma una mahitaji yake, una shida zinazoukabili, una kila aina ya matatizo kwa kila rika, yote hayo yanamuelekea mtumishi ama mtendaji wa umma.

Hospitali zikikosa dawa na vifaa, shule zikikosa madawati, vitabu na maabara, wanyamapori wakitishia kutoweka, mbuga na hifadhi za taifa zikivamiwa, nishati ya umeme ikihujumiwa, yote hayo na mengine yanaelekezwa kwa serikali.

Ni nani aliye mwadilifu akalitambulia hilo, kisha ajiridhishe na kuanza kusherehekea uteuzi katika nafasi yoyote, akijiaminisha kwamba ‘ameula’?

Labda kwa mtu mwenye hulka wizi, ufisadi, uhujumu uchumi, asiyeguswa na umasikini wa nchi na watu wake, anayeijua leo katika kujineemesha binafsi na si Tanzania inayodumu kizazi hata kizazi, atashangilia.

Ndio hao wanaoendekeza kauli ya kuula. Mazingira yanayojengeka tangu kuteuliwa, kuapishwa na hatimaye kuingia katika utumishi, yanaelekeza katika kuula.

Jamii inapowaandaa wateuliwa kwa kuamini kwamba ‘wameula’, ndivyo inavyokuwa hata wanapoingia kazini, wanakula kila kilicho cha umma, ili waonekane kweli wameula.

Kwa maana anaona akitoka bila kula, atachekwa, ataulizwa ‘kwani ulifanya nini tangu kipindi kile tulikupongeza kwa kuula, ulipoteuliwa?”

Umefika wakati pawepo na mfumo thabiti (unaoweza kuanishwa hata kwenye Katiba mpya), utumishi wa umma usigeuzwe kuwa pango la mafisadi, walanguzi na wenye kujineemesha.

Haiwezekani nchi iwe na adhimisho la kila mwaka, kusherehekea ufisadi, wizi na ubadhirifu wa fedha za umma kupitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kama ilivyofikia mwaka huu, inapaswa moto uliowashwa bungeni usizimike. Uendelee kuwaka, umulike kila kona yenye mali ya umma, itakaponyofolewa, wahusika wachukuliwe hatua kwa ukali na haraka.

Kwa maana kuwaacha wateuliwa na wengine ‘wanaoula’ kwa njia tofauti waendelee kutamba kwa uovu wao, Tanzania haitasonga mbele kwa kadri inavyopaswa.

Ndio maana ninashawishika kuamini kwamba hata wanapoteuliwa na kuapishwa hasa Ikulu jijini Dar es Salaam, hafla zisizokuwa na mashiko zipigwe marufuku.

Badala ya kuongozana na ndugu na jamaa zao, wateuliwa wafike wakiwa na watendaji wengine katika eneo husika, wakabidhiwe Katiba, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.

Wakiyapokea, waape kwamba wamepokea ili watayalinda hayo, vinginevyo hatua muhimu za kulinda hadhi na rasilimali za umma zitachukuliwa ikiwa watayakiuka hayo.

Hata sasa inawezekana, kupitia mamlaka kama ofisi za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Upelelezi (DPP) na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wanaweza kuanzia na mawaziri wanaotuhumiwa sasa.

Wachunguzwe kwa kina, hesabu moja hadi nyingi, mali kwa mali na hatimaye utajiri wote waliojilimbikizia, kisha itakapobidi, hatua zichukuliwe kwa ukali na haraka, hapo tutasonga mbele.

Kwa maana taarifa za jinsi ‘walivyotafuta’ mabilioni ya Shilingi ni sawa na mtu aliyekuwa na haraka ya kula chakula, akajikuta anabugia pasipo kunawa mikono.

Inatisha sana.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE.Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; [email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles