Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Toeni mikopo nafuu kwa wakulima -Pinda

17th May 2012
Print
Comments
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amezitaka benki za biashara nchini kujenga uaminifu na wakulima wadogo kwa kuwapatia mikopo ili kufanya kilimo kuwa ni uwekezaji wa kuvutia.

Alisema benki zinapaswa kutenga fedha ambazo zitawawezesha wakulima kupata mikopo kwa riba nafuu sambamba na kutoa huduma za kibenki vijijini.

"Benki wanapaswa kuwafikiria upya wakulima kwa kuwa wanaweza kuwa na sifa endapo watawafuatilia kwa ukaribu sambamba na kuwapatia elimu ya kisasa ya kilimo na kuwa wakulima wa kisasa,” alisema Waziri Mkuu.

Pinda alisema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili ya Afrika Vijijini na Chama cha Mikopo na Kilimo (Afraca) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Warsha hiyo, inalenga kuimarisha kilimo na imejadili mikakati ambayo itasaidia kuendeleza kilimo ili kupata chakula cha kujitosheleza katika Bara la Afrika.

Hata hivyo, Pinda alisema wakulima wadogo hawawezi kuendelea kutokana na benki nyingi kutokuwapatia fursa za kupata mikopo ya kutosha kutokana na viwango vyao vya riba pamoja na kukosa dhamana ya mkopo.

"Kwa sababu hiyo, taasisi za fedha lazima zijenge uhusiano na SACCOS katika kuongeza uhamasishaji katika maeneo ya mbali hususani vijijini juu ya umuhimu kwa mkulima kuchukua mkopo," alisema Pinda.

Alisema kilimo kimekuwa na uwezo wa kutoa asilimia 80 ya ajira nchini hasa katika maeneo ya vijijini na inachangia zaidi ya asilimia 75 ya mapato ya nchi kwa mauzo ya ndani na nje.

Alisema kutokana na umuhimu huo wa sekta ya kilimo, wakati umefika sasa kwa benki kuona jukumu la kuwasaidia wakulima ili kupunguza umaskini nchini kwa kuwa ndilo suluhisho la kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ukanda Mdogo wa Afrika Mashariki (AFRACA) ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya wananchi wa Dar es Salaam (DCB), Edmund Mkwawa, alisema lengo la warsha hiyo ni kujadili juu ya masuala na maendeleo kuhusiana na hatua ambazo zitasaidia kupanua ukuaji wa uchumi wa vijijini kwa nchi moja na Bara la Afrika kwa ujumla.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles