Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nchunga awavimbia wazee Yanga

10th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Lloyd Nchunga, amesema kwa sasa hawezi kujiuzulu nafasi yake hiyo anayoishikilia na atafanya hivyo endapo ataambiwa na wanachama wa klabu hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Juzi wazee wa klabu hiyo walimtaka Nchunga aachie madaraka kutokana na kushindwa kuiendesha klabu ambapo wachezaji wamekaa muda mrefu bila kulipwa posho zao huku pia kocha Mserbia Kostadin Papic akidai zaidi ya Sh. milioni 24.

Akizungumza na kituo cha redio cha jijini Dar es Salaam juzi, Nchunga alisema kuwa kamwe hawezi kuachia madaraka kwa kufuata maagizo ya wazee hao ilhali yeye alikabidhiwa uongozi na wanachama kwenye mkutano mkuu, hivyo atafanya hivyo endapo mkutano huo utamtaka ajiuzulu.

Nchunga alisema kuwa yeye ataendelea kuiongoza timu kama katiba inavyomtaka na kamwe hataenda kinyume na kilichoelezwa kwenye katiba yao.

"Siwezi kujizulu kwa kusikia kauli hiyo ya Wazee, je vijana nao wana kauli gani, wanawake pia sijui wanasemaje, nitawaeleza wanachama katika mkutano mkuu na kama wataridhia mimi kujiuzulu ndio nitatekeleza matakwa yao, nitawauliza wanachama wanachotaka," Nchunga alisema.

Alisisitiza kwamba yeye hakuweza kuwakabidhi Wazee timu kama walivyoomba kwa sababu katiba haimruhusu kufanya hivyo huku pia akieleza kwamba Wazee hao walishindwa kuweka wazi chanzo chao cha mapato endapo wangekabidhiwa timu.

Mwenyekiti huyo alisema pia asingeweza kuwapa Wazee hao timu kwa maamuzi yake peke yake bila ya kikao cha Kamati ya Utendaji kufanyika na kuridhia suala hilo.

Nchunga alisema kuwa juzi Kamati ya Utendaji ilishindwa kukutana kujadili kipigo cha 5-0 na tathmini ya msimu wa Ligi Kuu ya Bara uliomalizika Jumapili iliyopita kutokana na idadi kubwa ya wajumbe wa klabu hiyo kuwa nje ya jiji la Dar es Salaam.

"Kamati ya Utendaji itakutana kesho (leo) baada ya jana (juzi) kushindikana na baada ya hapo tutaelekeza mambo mbalimbali yatakayoamuliwa kwenye kikao hicho," aliongeza.

Hata hivyo, Nchunga hakuweza wazi ni lini Mkutano Mkuu huyo wa wanachama utafanyika akitoa sababu kuwa ni lazima taratibu za kuitisha mkutano huo zifanyike kama katiba inavyoeleza na si kukurupuka.

Nchunga katika mahojiano hayo pia alikiri mkataba wa Papic kuwa umemalizika na anaudai uongozi malimbikizo yake ya mshahara.

Papic alikuwa jukwaani akishuhudia Yanga ikipokea kipigo cha aibu kutoka Simba ambao tayari walikuwa wameshatwaa ubingwa wa Bara.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles