Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Simba kutangazwa bingwa leo?

23rd April 2012
Print
Comments
Timu ya Simba

Simba leo wana nafasi ya kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara lakini jambo hilo litatimia iwapo watawafunga Moro United na Azam watang'ang'aniwa japo kwa sare dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Chamazi jijini Dar es Salaam.

Ushindi kwa vinara Simba utawafanya wafikishe pointi 59 na kubakiwa na mechi moja dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga, wakati sare kwa Azam itawafanya wawe na pointi 51 huku wakibakisha mechi mbili baada ya leo. Azam ni lazima wawafunge Mtibwa leo kama wanahitaji kudumisha matumaini yoyote ya kutwaa ubingwa wao wa kwanza wa ligi.

Akizungumza baada ya mechi iliyopita waliyoshinda 3-0 dhidi ya JKT Ruvu, kocha wa Simba, Mserbia Milovan Circkovic, alisema kwamba hawatabweteka kwa kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi na badala yake, wataendelea kusaka ushindi katika kila mechi ili wajihakikishie ubingwa mapema.

Kama Azam wakiteleza na Simba kuibuka na ushindi, ‘Wanamsimbazi’ watatwaa ubingwa na kuwapoka taji hilo mabingwa watetezi, mahasimu wao wa jadi, Yanga.

Mbali na vita hiyo ya kuwania ubingwa kati ya Simba na Azam, ushindani mwingine uko mkiani mwa msimamo wa ligi ambapo timu nne zinachuana vikali kuepuka kuteremka daraja kama Polisi Dodoma iliyoshuka rasmi jana baada ya kufungwa na mabingwa wa msimu uliopita, Yanga.

Toto African yenye pointi 26  na kubakiwa na mechi tatu, African Lyon yenye pointi 23 na kubakiza mechi mbili, Villa Squad iliyobakiwa na mechi mbili huku ikiwa na pointi 23 na Moro United yenye pointi 19 na kubakiza mechi mbili ndizo zinazochuana kuepuka kuwemo katika orodha ya timu mbili nyingine za kuungana na Polisi Dodoma.

Ili kubaki ligi kuu, Toto watalazimika kufanya vizuri katika mechi zao dhidi ya Azam, Kagera Sugar na Coastal  Union wakati Lyon watalazimika kufanya vizuri pia dhidi ya Mtibwa na JKT Ruvu.

Villa wamebakiwa na mechi dhidi ya JKT Oljoro na Ruvu Shooting huku Moro United wakilazimika kupata matokeo mazuri katika mechi yao ya leo dhidi ya Simba na pia dhidi ya Mtibwa  watakayocheza nayo Mei 5.

Katika hatua nyingine, imedaiwa kuwa Simba imemnasa kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Nizar Khalfan, aliyekuwa akicheza soka la kulipwa katika Ligi Kuu ya Marekani kabla ya kuachwa na timu aliyodumu nayo kwa miezi mitatu ya Philadelphia Union.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa Nizar atatambulishwa kwa mashabiki leo jioni wakati ‘Wekundu wa Msimbazi’ watakaposhuka dimbani kucheza dhidi ya Moro United.

Kabla ya kujiunga Philadelphia, Nizar alikuwa akiichezea Vancouver Whitecaps aliyojiunga nayo Agosti 22, 2009 akitokea Moro United. Kabla ya hapo, Nizar aliwahi pia kuzichezea Mtibwa Sugar Al Tadamon ya Kuwait na Tadamon Sour ya Lebanon.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles