Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Simba yamng'ang'ania Yondani

28th June 2012
Print
Comments
Kelvin Yondani

Uongozi wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba bado unaendelea kumtambua beki wake wa kati, Kelvin Yondani kuwa ni mchezaji wao halali ambaye bado ana mkataba na wawakilishi hao wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwakani.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa Yondani ni mchezaji wa klabu hiyo na alisaini mkataba mpya Desemba 23 mwaka jana ikiwa ni miezi sita kabla ya mkataba wa awali ambao ulikuwa unamalizika Mei 31 mwaka huu.

Yondani alionekana akiwa anasaini mkataba na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed, akiwa amevaa jezi za timu ya taifa (Taifa Stars) mapema mwezi huu.

Beki huyo tayari ameshaanza mazoezi na Yanga na amekaririwa akisema kwamba ataichezea Yanga na si timu nyingine.

Taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa niaba ya Simba inaonyesha kwamba klabu hiyo bado inamtambua Yondani kuwa ni mchezaji wake kwani jina lake halimo katika orodha ya wachezaji waliomaliza mikataba na timu hiyo wala waliotemwa.

Taarifa hiyo ya Simba iliyotolewa na Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, iliwataja wachezaji ambao wamemaliza mikataba ya kuichezea Simba ni pamoja na Ally Mustafa 'Barthez', Derick Walulya, Gervais Kago na Juma Jabu wakati kiungo, Salum Kanoni ambaye msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo Moro United mkataba wake unatarajia kumalizika keshokutwa Juni 30 mwaka huu.

Wambura alisema pia wachezaji ambao Simba inakusudia kuwatoa kwa mkopo ni Rajab Isihaka, Salum Machaku, Haruna Shamte ambaye alipelekwa Villa Squad na Shija Mkina aliyerudishwa Kagera Sugar. 

Alisema pia Polisi Morogoro iliyopanda daraja msimu huu imeacha wachezaji 17 wakati Tanzania Prisons yenyewe imeacha wachezaji 11 huku Azam ikikatisha mikataba ya wachezaji watatu.

Pia wachezaji wengine 12 wamemaliza mikataba yao katika klabu ya Kagera Sugar.
Alieleza kuwa zoezi la uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.

Wachezaji walioachwa Polisi Morogoro ni Abdul Ibadi, Ally Moshi, Benedict Kitangita, Hassan Kodo, Hussein Lutaweangu, Hussein Sheikh, Juma Maboga, Mafwimbo Lutty, Makungu Slim, Mbaraka Masenga, Method Andrew, Moses Mtitu, Ramadhan Kilumbanga, Ramadhan Toyoyo, Said Kawambwa, Salum Juma na Thobias John.

Tanzania Prisons imewaacha Adam Mtumwa, Dickson Oswald, Exavery Mapunda, Ismail Selemani, Lwitiko Joseph, Mbega Daffa, Mwamba Mkumbwa, Musa Kidodo, Rajab Ally, Richard Mwakalinga na Sweetbert Ajiro.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment