


.jpg)
Jumla ya gesi asili yenye futi za ujazo trilioni 20.97 imepatika katika kina cha maji marefu, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospteter Muhongo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana.
Alisema kiasi hicho cha ujazo wa gesi kinajumuisha kisima kilichogundulika wiki iliyopita (Juni 13, mwaka huu), cha Lavani na Kampuni ya Statoil ambayo inashirikiana na Kampuni ya Exxon Mobil kwenye kitalu namba mbili Mashariki mwa mkoa wa Lindi takribani kilometa 80 kutoka nchi kavu.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa na kasi kubwa katika utafutaji wa mafuta na gesi asili hapa nchini. Utafutaji huu umejikita zaidi kwenye bahari ya Hindi kwenye maji ya kina kirefu,”alisema.
Alisema ugunduzi huo umefanyika Mashariki kwa mikoa ya Mtwara na Lindi.
Aidha, Profesa Mulongo, alisema kampuni ya Petrobras kutoka nchini Brazil nayo ilichimba kisima kimoja mwishoni mwa mwaka jana kwenye kitalu namba tano.
Hata hivyo, alisema kisima hicho kiitwacho Zeta-1 ambacho kilichimbwa hadi kufikia urefu wa mita 3,695 chini ya bahari, kwa bahati mbaya kisima hicho hakijagundua mafuta wala gesi asili ingawa dalili zilionyesha kuwa nzuri.
Alisema katika visima vilivyochimbwa kwenye bahari ya kina kirefu, visima saba vimegundua gesi asili.
Alisema kisima kimoja kingine (Papa-1) kinaendelea kuchimbwa kwenye kitalu namba tatu na kwamba kisima hicho kinategemewa kukamilika Julai mwaka huu.
Alisema utafutaji wa mafuta ya gesi kwenye bahari ya kina kirefu unagharimu fedha nyingi na kwamba kisima kimoja kinagharimu takribani dola za kimarekani milioni 100 hadi milioni 150 baada ya gharama za ukusanyaji takwimu za mtetemo.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kasi hii ya utafutaji mafuta na gesi inaendelea na serikali itatoa msukumo zaidi kwa makampuni hayo kuendeleza utafutaji,”alisema.
Pia alisema visima vitatu vimekamilika ambapo viwili vikiwa vimegundulika Songo Songo na Magharibi mwa Mtwara.
Alisema kisima kilichokamilika Mei mwaka huu katika Songo Songo kina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo milioni 60 kwa siku.
Profesa Muhongo alisema makampuni makubwa duniani ya utafutaji wa mafuta na gesi asili yapo hapa nchini kwa ajili ya kufanya utafiti.
Aliongeza kuwa kulikuwa na makampuni 19 yaliyokuwa yakifanya utafiti huo, hadi kufikia Juni 14, mwaka huu.
Profesa Mulongo alisema pia leseni 28 zimetolewa kwa makampuni hayo, ukiondoa kampuni ya Antrim ambayo ina leseni ya Zanzibar wanakofanyia shughuli za utafiti.