Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Bajeti ya Kilimo yakwama

22nd July 2012
Print
Comments
  Nusu ya wabunge wa kuipitisha wakosekana
Naibu Spika, Job Ndugai

Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika jana ilikwama kupitishwa na Bunge baada ya kukosekana kwa nusu ya idadi ya wabunge bungeni inayohitajika kikanuni.

Tatizo la utoro wa wabunge limekuwa likikemewa kwa mara kadhaa na Spika wa Bunge, Anna Makinda, jambo ambalo lilimfanya kuwataka kuomba ruhusa kwake wanapotoka nje ya Mkoa wa Dodoma.

Dalili za kukwama kwa bajeti hiyo zilionekana mapema jana asubuhi wakati kikao hicho kikianza, ambapo viti vingi vya Bunge, vinavyokaliwa na mawaziri na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), vikiwa tupu.

Kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho cha Bunge na Naibu Spika, Job Ndugai, Mbunge wa Kuteuliwa, (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kifungu cha 112 cha Kanuni za Bunge, kinachomtaka Spika kuahirisha mjadala unaohitaji maamuzi ya Bunge iwapo idadi ya wabunge haitofikia nusu ya wabunge wote.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nimehesabu mara mbili, idadi ya wabunge waliopo humu ndani haizidi 110, wakati idadi kamili ya wabunge wote ni 352 maana yake hatujakidhi akidi inayotakiwa ya kufikia nusu, naomba utuhesabu na ukiridhia uahirishe Bunge,” alisema Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi na kuungwa mkono na wabunge wote wa upinzani.

Naye Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alitumia kifungu cha 77 (1) kuombea mwongozo wake na kufafanua kuwa kifungu hicho kinabainisha wazi kuwa iwapo idadi ya wabunge haitofikia nusu, lazima Bunge liahirishwe kabla ya kutoa maamuzi ya mjadala unaoendelea. Akijibu hoja hizo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alinukuu kifungu cha 77 (3) ambacho kinabainisha kuwa Bunge litaahirishwa pale tu Spika atakapojiridhisha kuwa kuna upungufu wa wabunge na atalazimika kupiga kengele na kuhesabu idadi ya wabunge waliopo.

“Kwa hili nimelipokea lakini naomba kwanza mnipe muda, tuendelee kwanza kupitisha vifungu kupitia kamati ya matumizi kabla ya kuipitisha bajeti nitashughulikia mwongozo wenu,” alisema Ndugai jambo ambalo lilisababisha minong'ono ndani ya Bunge.

Kutokana na majibu hayo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, aliomba mwongozo kwa kutumia kifungu cha 112 na kumtaka Ndugai aahirishwe Bunge kwa kuwa kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara hiyo ya kilimo katika kamati ya matumizi ni sawa na kutoa maamuzi.

Hata hivyo, Ndugai alikuja juu na kutaka utulivu kwa kuwa Spika akishatoa maamuzi Kanuni haziruhusu kuhojiwa. “Najua mnahangaika kwa hili, lakini mjue kuwa hatuko shule ya msingi hapa, hivi vitu ni gharama, nyie ndio wa kwanza kupigia kelele matumizi makubwa, kuahirisha Bunge si jambo dogo ndio maana nimesema nipeni muda,”alisema Ndugai.

Hali hiyo ilimfanya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, alionekana kutoka nje na kuingia ndani ya Bunge, ikiwa ni jitihada za kuwataka wabunge waliokuwa nje ya ukumbi kuingia ndani ya ukumbi.

Baada ya kupitisha vifungu vya bajeti hiyo, Ndugai alipiga kengele ya kuwaita wabunge lakini hatimaye alilazimika kuahirisha Bunge hilo bila bajeti hiyo kupitishwa kwa kuwa idadi wa wabunge waliopo ndani ya Bunge hilo haikutosheleza akidi inayotakiwa.

“Niliomba muda ili na mimi nijiridhishe kwa kuangalia kwanza kama kuna Kamati yoyote inayoendelea, lakini mjue kuwa kuna wabunge 18 na mawaziri wamepewa ruhusa ya Spika kwenda Zanzibar kuzika kutokana na ajali ya meli ya Mv Skagit iliyotokea juzi,” alisema.

Aidha, alisema pia wapo wabunge aliowaruhusu kwenda kwenye mazishi ya mama yake mzazi mbunge wa Longido Lekule Laizer .

Hivi karibuni, Spika Makinda aliwajia juu wabunge wanaokimbia vikao vya Bunge na kusema kuwa, iwapo tabia hiyo itaendelea, ipo siku Serikali itashindwa kupitisha bajeti yake.

Aidha siku chache baadaye, Spika huyo aliwataka wabunge kuhakikisha kuwa kabla ya kuondoka kwenye vikao vya Bunge na kwenda kwenye shughuli zao nje ya Dodoma kupata kwanza ruhusa kutoka kwake huku Mawaziri wakitakiwa kuomba ruhusa hiyo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wakati huohuo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anna Abdallah alijibu tuhuma alizorushiwa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa upande wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili kuhusu matumizi mabovu ya fedha za Bodi ya Korosho yaliyotumika kulipia posho katika kikao kimoja.

Mbunge alikiri yeye pamoja na wajumbe wengine watatu ambao ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Mudhihir Mudhihir na mjumbe wa bodi hiyo, Jerome Bwanausi ambapo pia alikiri mke wa Mudhihir kulipwa fedha lakini si kama mjumbe wa bodi hiyo.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa bunge Mbatia alisema“Kusudio letu si kukomoana hata kidogo, sisi tunalitendea haki Taifa yetu…kama unataka ubunge uhakikishe unawajibika,”alisema Mbatia.

Naye Mkosamali alisema kwa muda mrefu Bunge limekuwa likipitisha bajeti bila kufuata kanuni inayowataka wabunge kuwa nusu ya idadi ya wabunge wote wakati wa kupitisha maamuzi.

Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema kinachofuata ni kumuomba Spika kuwapatia orodha ya idadi ya wabunge waliojiorodhesha wakati wa kupitisha bajeti zilizopita.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment