Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mbunge Nassari ajipeleka Polisi

9th May 2012
Print
Comments
  Afuatana na wakili wake
  Ni juu ya Jamhuri ya Meru
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari (kushoto), akiwa na wakili wake, Alberth Msando, wakingia katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Arusha jana baada ya kutii wito wa kujisalimisha.(PICHA: CYNTHIA MWILOLEZI)

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, jana alijisalimisha kwa Jeshi la Polisi akiwa na wakili wake Albert Msando, ambako alihojiwa kwa zaidi ya saa nne kuhusu tuhuma za kutoa maneno yanayodaiwa kuwa ya uchochezi.

Hata hivyo, baada ya mahojiano hayo majira ya jioni, Nassari alipata dhamana ya Polisi kwa kudhaminiwa na James Ole Millya, lakini anatakiwa kuripoti tena polisi leo.

KAULI YA WAKILI WAKE
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka kufanya mahojiano na makachero wa Polisi, Wakili Msando, alisema kila kitu kilikwenda sawa na aliwashukuru polisi kwa kumpokea mteja wake kwa heshima zote.

Alisema katika mazungumzo, polisi walisema kosa analodaiwa kufanya Nassari linaangukia katika kifungu namba 63 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, cha kutoa kauli ambayo inaweza kuleta uchochezi dhidi ya Jamhuri.

Kwa mujibu wa kosa hilo, adhabu anayoweza kupewa mtu anayedaiwa kutoa maneno hayo ni faini ya Sh. 1,000 au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.

NASSARI AZUNGUMZA
Kwa upande wake Mbunge Nassari alisema polisi walitaka kujua maana ya maneno aliyoyatoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Arusha Jumamosi iliyopita.

Akifafanua Nassari alisema lengo kubwa la kauli yake ni kuweka mabadiliko ya kihamasa katika mikoa hiyo ili wengine waone wivu wa kimaendeleo kwa mikoa ya kaskazini ambayo imeonyesha mabadiliko makubwa.
“Mimi ni mtu mdogo tu, sina nguvu hizo za kutangaza uhuru wa sehemu yoyote ya nchi,” alisema.

Juzi Naibu Kamishina wa Polisi, (DCP) Isaya Mngulu, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa walikuwa wakimtafuta Mbunge Nassari kwa maneno yaliyotamkwa wakati wa mkutano wa  ‘Vua gamba, vaa gwanda,’ uliofanyika Jumamosi iliyopita, ambao yeye pamoja na wenzake watatu walidaiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Aliwataja wanachama wengine waliohojiwa kuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche, aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini kabla ya kujiunga na Chadema, Alphonce Mawazo na aliyekuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha kabla ya kujiunga na Chadema, Ally Bananga.

DCP Mngulu alidai kuwa maneno wanayodaiwa kuyatamka kwenye mkutano huo ni, “kama polisi hawatawakamata watu waliohusika na mauaji ya Mwenyekiti wa Chadema tawi la Usa River, wilayani Arumeru, Msafiri Mmbwambo, basi watajitangazia uhuru wa eneo la Meru pamoja na mikoa ya kaskazini kwa kushirikiana na baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.”

Alisema walitamka kwamba wanampiga marufuku Rais na Waziri Mkuu kutembelea Mkoa wa Arusha.

Pia wanadaiwa kutamka kwamba  Ridhiwani Kikwete anatembea na wanawake na kisha kumshauri baba yake Rais Jakaya Kikwete, ambaye naye huwateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi.


HALI ILIVYOKUWA JANA
Kwa mara ya kwanza, Nassari alifikia makao makuu ya Polisi mkoani hapa, saa 6: 12 mchana akiwa ameongozana na wakili wake.

Baada ya kuteremka kwenye gari aina ya BMW lenye namba za usajili T722 BCK walikwenda katika ofisi za Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Wakiwa katika ofisi hiyo, walielezwa kwamba Kamanda hakuwepo ofisini na baada ya kusuburi kwa dakika chache walitoka nje wakisema wangerudi tena ofisini hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi, Wakili Msando alisema  amepata taarifa ambazo siyo rasmi kwamba mteja wake anahitajika kuripoti polisi.

Alitaja taarifa hizo kuwa zilitolewa kwenye mitandao na ujumbe mfupi wa simu.

“Hatujui anatafutiwa nini… mtu tuliyemkuta ofisini ametueleza kuwa kamanda ayupo…tutarudi baadaye kuonana nao,” alisema.

Kwa upande wake, Nassari alisema Jumapili iliyopita alitumiwa ujumbe mfupi wa simu toka kwa ofisa mmoja wa upelelezi akijulishwa kuwa anatafutwa.

“Nimefika hapa sijawakuta, naondoka kwenda kuendelea na shughuli zangu huko Arumeru,” alisema na kuongeza hata hivyo kuwa Jumapili alifika ofisini hapo kuonana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Thobias Andengenye, kuagana naye.

Kamanda Andengenye amehamishiwa makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam ambako atakuwa Mkuu wa Idara ya Utawala.

Wakati wakiwa wameondoka, DCP Mngulu alifika ofisini na alipewa taarifa kwamba Mbunge Nassari alifika kujisalimisha, lakini kwa
vile hakumkuta alisema angerudi tena.

DCP Mngulu alifika ofisini hapo majira ya saa 6:28 mchana na akasema alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.

Hata hivyo, alionyesha kushangaa kwa Mbunge huyo kufika na kuondoka kwa maelezo kuwa wapo viongozi  wengi wa Polisi ambao angeweza kuripoti kwake.

Hata hivyo, aliendelea kumsubiri hadi majira ya saa 7:13 muda ambapo Nassari na mwanasheria wake waliporejea tena ofisini hapo.

Wakati anafika kwa mara hiyo ya pili alipokewa na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Akili Mpwapwa, na wakaongozwa moja kwa moja ofisi hadi ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Mkoa na waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuwepo ndani.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles