Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Nenda Ekelege, `kisiki` kilichomshinda Chami!

20th May 2012
Print
Comments

Ninamtaja Charles Ekelege kutokana na kushika wadhifa muhimu katika utumishi wa umma, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Nchini (TBS).

Kama Ekelege angekuwa baba wa nyumbani anayeshughulikia mashamba ama mifugo yake kijijini, angekuwa mfanyabiashara binafsi, ‘nisingekutana’ naye hapa.

Lakini aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBS, taasisi iliyokabidhiwa majukumu kadhaa, ikiwemo kuthibitisha ubora wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Ndio maana moja ya bidhaa zilizotarajiwa kuthibitishwa ubora wake kabla ya kuingia nchini, ni magari.

Zipo bidhaa nyingine zinazokadiriwa kufikia 50 kwa aina zake, yakiwemo mafuta ya ndege, zimetajwa kwenye orodha ya zilizoingizwa nchini pasipo kukaguliwa.

Ili kurekebisha utendaji kazi wa TBS kwa maslahi ya umma, kamati ndogo ya Bunge ilitumwa kwenda nchini Singapore na Hong Kong kujiridhisha kama ukaguzi wa magari katika nchi hizo unafanywa kwa mujibu wa sheria.

Ziara hiyo ilimuwezesha Ekelege kutangulia katika nchi hizo, akiwa (kama) mgeni wa wabunge, kwa maana TBS anayoingoza ilipaswa kutoa maelezo.

Kwa mujibu wa wabunge hao, hapakuwa na dalili zozote za kuashiria kuwepo kwa mawakala wa ukaguzi wa magari kwenye nchi hizo.

Kwamba hata ofisi walizofikishwa wabunge na kukutana na Ekelege, hazikuwa na picha ya Rais, ramani ya Tanzania ama kielelezo chochote cha kuashiria wamiliki wake walikuwa Watanzania ama wakifanya kazi za Tanzania.

Hakuna ukaguzi wa aina yoyote uliofanywa kwa maana wabunge hawakuona mashine ya ukaguzi.

Yapo mambo mengi yanayoweza kubatizwa jina maarufu la ‘madudu’ ya TBS nje ya nchi, kiasi cha kumfanya Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora kumkwida na kutaka kumpiga Ekelege.

Lugora akasema alifikia hatua hiyo baada ya kuona, pamoja na mambo mengine, Ekelege anawazungumza na kufanya ‘ya kitoto’ kwa mambo yanayoliathiri Taifa.

Hata hivyo, bado taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, zilibainisha kiasi kikubwa cha upotevu wa fedha kupitia uzembe wa TBS.

Hapo wabunge wakapendekeza (hata kabla ya ukaguzi wa CAG), Ekelege asimamishwe kazi ili uchunguzi huru ufanyike.

Waziri wa Viwanda na Biashara aliyekuwepo wakati huo, Cyril Chami hakufanya hivyo, akasema suala hilo lipo nje ya uwezo wake.

Jamii ikamuona Ekelege mfano wa kisiki kilichomshinda Chami. Imani ya wananchi walio wengi kwa serikali ikazidi kufifia, moja ya vyanzo ikiwa ni kutochukuliwa uamuzi mgumu kama uliomstahi Mkurugenzi Mkuu wa TBS.

Sasa Waziri wa Viwanda na Biashara aliyeteuliwa baada ya ‘gamba kuvuliwa’ kwenye baraza lililopo, Dk Abdallah Kigoda, ametangaza kumsimamisha kazi Ekelege.

Hatua ya kumsimamisha inatoa mwanya wa kuchukuliwa hatua nyingine zaidi, kwa mujibu wa maelezo ya Dk Kigoda.

Nikiri wazi kwamba Ekelege akiwa binadamu wa kawaida, kuna mambo mazuri atakuwa ameifanyia nchi hii kupitia nafasi yake ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS.

Kuna nguvu nyingi atakuwa amezitumia katika kuhakikisha TBS inafikia matarajio yake. Swali ni kwamba ‘alidondoka’ wapi hata kufikia hatua ya kuwa miongoni mwa wanaolihujumu taifa?

Inapofikia Waziri wa serikali kumsimamisha Ekelege, asisononeke, asifadhaike, asiwe na kinyongo, aende kupumzika.

Nenda Ekelege, iwe ni kijijini ama sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili ukisubiri hatua zinazopangwa kuchukuliwa dhidi yao.

Wewe ni mmoja miongoni mwa wachache `walionyofolewa’ kutoka kwa Watanzania wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni 40, wakapewa majukumu yenye maslahi kwa umma.

Kwa maana hiyo, maslahi ya umma yalipaswa kuwa kipaumbele cha awali, cha muhimu na cha kulindwa mithili ya mboni ya jicho, kila utekelezaji wa majukumu ulipostahili.

Kuanguka kwako kunaweza kuwa wokovu kwa taifa na umma wakiwemo ndugu zako, jamaa zako, rafiki zako na yeyote mwenye shirika la wewe.

Hivi sasa taifa linapambana na rushwa, ubadhirifu wa mali, fedha za umma na ufisadi wa aina nyinginezo.

Yanayomkuta Ekelege yanaweza kuibua uchungu, hasira na kuifedhehesha sehemu ya jamii pana ya Watanzania, hasa waliokuwa wanufaika wa ‘madudu’ yanayotajwa kuliingizia hasara taifa.

Lakini wapo pia ndugu wa karibu ambao mpaka hapa, wameshaanza kushikwa na kiwewe, hofu na wasiwasi. Kwamba ni nini kitafuata?

Kibinadamu lazima kuguswa na hali hiyo, lakini kwa maslahi ya taifa lililo bora kwa miaka na kizazi kijacho, Ekelege na wengine wanaoguswa na kadhia kama zake, wanastahili.

Ni heri kuwashughulikia watu wachache kwa mujibu wa sheria za nchi, wale wanaoliangamiza taifa ili kuwaokoa mamilioni ya raia wakiwemo wanaokabiliwa na umasikini wa kutupwa.

Kwa maana kama hapakuwa na ukaguzi wa magari japo kwa Singapore na Honk Kong pekee, ni idadi gani ya ‘takataka za magari’ zimeingizwa na kusababisha hasara zipi ikiwemo vifo!

Ukiachilia mbali magari, ni bidhaa gani miongoni mwa zinazofikia 50 kwa aina zake, ziliingizwa pasipo kukaguliwa, kisha zikaawathiri wananchi?

Wangapi wamekufa kutokana na matumizi ya bidhaa zilizoingizwa zikiwa ‘feki’, lakini hazikukaguliwa kutokana na kuwepo ‘mawakala hewa’ kama ilivyotajwa kwenye ripoti iliyohusu ziara ya wabunge nje ya nchi?

Mengi yanaweza kuzungumzwa, kutajwa, kujadiliwa. Lakini jambo la msingi kusema’ nenda Ekelege, jiweke pembeni ili tuuone ujasiri wa serikali katika kufikia uamuzi mgumu.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe; [email protected]

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles