Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Operesheni vua gamba, vaa gwanda inavyoisumbua CCM

9th May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe akihutubia moja ya mikutano.

Harakati za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), tangu kuzindua Operesheni  ya kuvua magamba na kuvalisha magwanda, operesheni maarufu kwa jina la Movement For Change imezidi kushika kasi ya ajabu, kwa kupokea maelfu ya wafuasi wa Chama cha Mapinduzi kujiunga na chama hicho.

Operesheni hiyo iliyozinduliwa Machi 23 mwaka huu, katika Hotel ya Naura Spring Jijini Arusha,Movement For Change inaongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini,Godbless Lema, ambaye hadi sasa tangu avalie njuga kampeni hizo,amefanikiwa kuvuta wafuasi wa Chama cha CCM zaidi ya 2,000.

Kati  yao wamo viongozi wa Umoja wa Vijana CCM MKoa wa Arusha na mabalozi wa nyumba kumi hali ambayo imekuwa gumzo kubwa hasa katika Jiji la Arusha na kwenda mbali zaidi kwa baadhi ya watu, kuitabiria CCM kuwa sasa inakaribia kuanduka.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wafuasi wake wengi, wakiwemo Mabalozi Wenyeviti wa Vijiji
na Mitaa kuhama chama hicho kwenda Chadema.

Lakini wakati haya yakifanyika imebainika pia wapo Wabunge wanaotaka kuhama Chama cha Mapinduzi na kujiunga Chadema, ili waweze kuendeleza Movement For Change, kwa lengo la kuchukua dola mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anasema kuwa tangu kuzindua kwa Movement For Change,imeonyesha matunda makubwa na ya ajabu, kwani licha ya kuhama kwa Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya na kuzua zogo kubwa nchini, amepokea maombi ya Wabunge wa CCM 70 wanataka kujiunga na chama hicho.

Anasema kuwa kati ya hao  Wabunge, tisa walioapishwa kuwa mawaziri wapya, ni miongoni mwa walioomba kujiunga na Chadema, pamoja na wanachama zaidi ya 1000 wa Wilaya za Jiji la Arusha, hali inayoonyesha
kuwa harakati za ukombozi  zinaendelea.

“Mimi kama Kamanda Mkuu nimewaambia wafanye haraka waje, kabla ya milango hatujafunga, sababu itafika wakati Safina ikijaa na kufunga milango hatutafungua tena, na hii inaashiria tutafanya chaguzi ndogo ndogo nyingi kuliko kipindi chochote kile tangu Uhuru upatikane Tanzania,”anasema.

Mbowe anasema hiyo ni ishara kuwa gari la CCM limechakaa na linaenda kupaki, kwa sababu hata Kamanda Mkuu ambaye ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ameanza kuvunja hata misingi ya nchi iliyowekwa na kusababisha gari kwenda kombo zaidi.

“Huyu Kikwete amevunja Katiba yetu  kwa kujipa madaraka  ya Bunge ya kumteuwa Mbunge saa nane na saa tisa kabla ya kuapishwa na Bunge anampa Uwaziri, huu ni ukiukwaji mkubwa wa katiba yetu na analifahamu hili, ila amefanya kwa makusudi na sisi hatuwezi kuvumilia , tunamsubiri na baraza lake bungeni Bunge la bajeti,”anasema.

Anasema kuwa siyo hilo tu, bali amevunja katiba kwa mara ya pili  kwa siku hiyo hiyo ya uteuzi wa Mawaziri kwa kuwateua Wazanzibari kwenye Wizara ambazo siyo za Muungano, kama Afya aliyomkabidhi, Dk. Hussein Mwinyi.

Mbowe anasema kwamba kuna Wizara za Muungano zinapaswa kuwa na Mawaziri Wawili wa Bara na Visiwani na Wizara zisizo za Muungano, zinatakiwa kuwa na Mawaziri wa Tanzania Bara tu, lakini yeye amekiuka Katiba.

Aidha Mbowe anasema kuingiza kwa wanachama wengi wa Chama cha Mapinduzi, hakuwezi kuangamiza chama hicho kwa sababu wako imara na Chama hakiwezi kuangamizwa na mamluki wa CCM.

“Ila nawaambia wanachama wa CCM mnaoingia katika Safina ya Chadema,mjuwe kuwa huku ni kazi tu na hakuna rushwa wala ulaji, huku ni mzigo kweli kweli, hivyo msije mkadhani kuna ulaji kma CCM na ukiona huwezi bora usije,”anasema.

Hata hivyo anawaomba wanachama na wafuasi wa Chama cha Chadema kutokuwa na shaka  na wanaotoka CCM na kujiunga na chama hicho, bali wanapaswa kuwapokea kwa mikono miwili na kuwaonyesha njia sahihi ya kutafuta ukombozi wa kweli.

Anasema wafuasi wanaopata hofu kuwa James Ole Millya ametumwa na Mbunge wa Monduli, Edwad Lowassa, kuja kupeleleza Chadema, wawe na amani kwasababu chama kiko imara na hakiwezi kuhujumiwa na kundi au mtu yoyote kw anguvu wala mbinu yoyote.

Mbowe anasema wanaofikiri Lowassa na wengine  wenye ukwasi  wa kuweza kununua viongozi wa Chadema, kujiuliza  kwa nini  hawakuweza  kufanya hivyo, kipindi chote walichokitumikia  kukijenga  chama hicho,ambacho ni tishio kwa CCM na mafisadi wote.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Taifa (BAVICHA), John Heche, anasema Chama chao kipo imara na hakiwezi kuwa na vibaraka kama vyama vingine vya upinzani na hilo limejidhihirisha wazi juzi Rais
alipomteua James Mbatia wa NCCR  Mageuzi kuwa Mbunge.

Anasema kuwa hiyo inaonyesha jinsi CCM walivyopandikiza vibaraka vyama vya upinzani, lakini haliwapi homa na watazidi kupiga kelele pale mambo yanapokwenda kombo kama vile ukubwa wa Mawaziri ambalo wamelipigia kelele apunguze kutoka Mawaziri 50, japo badala ya kupunguza ameongeza na kuwa 55 juzi alipoteua baraza linguine.

“Lakini inabidi tumhurumie Kikwete wakati anafahamu wananchi wanaishi maisha ya shida, anadiriki kuteua Waziri asiye na Wizara Maalum, Marck Mwandosya, inasikitisha sana na kushangaza,”anasema.

Heche anasema kuwa Mawaziri walioiba fedha za umma  na kununua nyumba ya milioni 700, wanadiriki kupaza sauti hadharani kuwa hizo sio pesa, hiyo ni dharau kwa watanzania kama zile za Chenge aliyesema ni vijisenti.

Anasema lakini waelewe watanzania wa leo sio kama wa jana, watu wamechoka na wizi wa CCM, hali inayosababisha kuwa na mlipuko wa watu kuhama CCM, ambapo yeye kwa mwezi mmoja amepokea wanachama 300 Dar es Salaam na wakati akiwapokea na Mbunge wa Moshi Mjini, Phillimon Ndesamburo, amepokea wanachama 18 wakiwemo mabalozi wa nyumba kumi na Wenyeviti wa serikali za mitaa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana CCM, Mkoa wa Arusha (UVCCM), James Millya,ambaye sasa amejiunga na Chadema, anasema atakuwa mstari wa mbele kutetea ukombozi maeneo ya umasaini kwa sababu jamii yao imetengwa na kunyanyasika miaka hamsini ya Uhuru.

“Sisi wamasai tumekuwa watumwa miaka hamsini ya Uhuru, ukiangalia kule Ngorongoro, Serengeti tunafukuzwa tuende maeneo mengine, sasa imetosha na mimi nitazunguka maana nimepata mwanga, baada ya kuwa gizani katika chama cha CCM,’Anasema.

Anasema CCM ni chama cha watoto wa Vigogo na matajiri, hivyo watoto wa maskini waliopo ambao hawataki kutoka kwa kutegemea kupata angalau Mkuu wa Wilaya au cheo fulani watazeeka bila kupata hayo, hivyo anawaomba waondoke mana huko sio kwao.

Mwanachama mwingine aliyehama CCM na kujiunga Chadema, ambaye alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM MKoa wa Arusha, Ally Bananga, anasema ameamua kwa dhati kukihama chama hicho na mke wake Alia Bananga, mama yake mzazi Imma Hussein na Meneja kampeni wake aliyekuwa katika uchaguzi Arumeru, Lazaro Macha, baada ya kuchoshwa ana ubabaishaji wa CCM.

Anasema kuwa kwa namna ya pekee anamshukuru Jakaya Kikwete na Ridhiwani Kikwete kwa kuwaudhi Vijana, kwasababu kumewafumbua macho na kugundua mabaya ya CCM, hivyo anaomba Mungu amsamehe kwa dhambi alizofanya ndani ya CCM .

“Lakini pia nawaomba waswahili wenzangu yaani Waislamu, tubadilike na tuachane na propaganda za kuwa Chadema ni cha udini na baadhi ya makabila huu uwongo na kama hatuingii ndani tunasemaje haya, tuingie ndani ndipo tuseme kama hatutakiwi, siyo mwanamke unamlaumu anapika mchicha kila siku wakati hutoi fedha ya nyama,sisi tumetangulia tunasafisha njia ingieni,”anasema Bananga.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles