Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

CCM matokeo ya urais yapingwe mahakamani

18th May 2012
Print
Comments
  Pia yashauri madaraka ya rais yajadiliwe
  Yagusa uteuzi wa waziri mkuu, mawaziri
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakihojiwa na makundi mbalimbali ya jamii na kutaka yawekwe katika Katiba mpya, likiwamo la kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais, yamekubaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujadiliwa kwa mapana katika mchakato wa kupata Katiba hiyo.

Mambo hayo yalijadiliwa na kukubaliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM katika semina kuhusu ‘Mwongozo  wa CCM katika kushiriki mjadala wa Katiba mpya’ iliyofanyika mkoani Dodoma, Mei 13, mwaka huu na kuongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema mambo hayo yanahusu uendeshaji wa serikali na kutaka wananchi wapewe fursa ya kuchangia maoni yao kwa kadiri kila mmoja anavyoona inafaa kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Aliyataja mambo hayo ambayo alisema yapo wazi kwa mjadala mpana kuwa ni pamoja na mambo yanayosababisha kuwapo kwa kero za Muungano zilizopo, hususan orodha ya mambo ya Muungano.

Mengine ni utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Rais, taratibu za uteuzi wa mawaziri na waziri mkuu, utaratibu wa uteuzi wa tume huru ya uchaguzi na suala la mgombea binafsi katika uchaguzi wa dola.

Mengine ni kuhusu muundo wa Bunge na Baraza la Wawakilishi na aina ya wabunge na wawakilishi, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa Rais, uwapo wa baraza la pili la kutunga sheria, ukomo wa idadi ya wabunge, mfumo wa mahakama na nafasi ya Rais wa Zanzibar katika uongozi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Suala la kuwepo kwa mgombea binafsi limekuwa likipendekezwa kwa muda mrefu, lakini serikali imekuwa ikilipinga licha ya Mahakama kutoa hukumu kadhaa za kuruhusu wawepo.

Mahakama Kuu ilitoa hukumu mbili za kuwaruhusu katika kesi zilizofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila.

Hata hivyo, serikali ilikata rufani katika Mahakama ya Rufani na mwaka 2010, jopo la majaji saba wa mahakama hiyo likiongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu, Agustino Ramadhani, lilibatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu kwa kusema kuwa mahakama haina mamlaka ya kuliamua kwa kuwa ni la kikatiba kwa maana ya kutungwa kwa sheria na linapaswa kurejeshwa bungeni.

Tangu mabadiliko ya 11 ya Katiba yalipomwondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais na kubakia kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wazanzibari wamekuwa wakihoji na kulalamika kuwa ameshushiwa hadhi.

Kuhusu Tume ya Uchaguzi, makundi mbalimbali yakekuwa yakishinikiza kuwepo kwa tume huru kwa madai kuwa tume ya sasa inaundwa na makada wa CCM wanaokipendelea chama hicho.

Kuhusu uteuzi wa mawaziri na Waziri Mkuu, kumekuwepo na maoni kutoka makundi mbalimbali kwamba mfumo wa Westminster wa kuteua mawaziri kutoka bungeni uachwe badala yake utumike mfumo wa mawaziri kuteuliwa nje ya Bunge ili kuwezesha uwajibikaji.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa Ibara ya 51 (2) Rais anaruhusiwa kumteua mbunge wa kuchaguliwa kutoka jimbo la uchaguzi anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi bungeni au kama hakuna chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi anayeelekea kuungwa mkono na wabunge walio wengi kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano.

Waziri Mkuu hatashika madaraka hadi uteuzi wake kwanza uthibitishwe na Bunge.

Ibara ya 55 (1) hadi (4) inasema kuwa, mawaziri wote ambao ni wajumbe wa baraza la mawaziri watateuliwa na Rais baada ya kushauriana na Waziri Mkuu.

Mawaziri na naibu mawaziri watateuliwa kutoka miongoni mwa wabunge.

Vile vile, madaraka ya Rais yamekuwa yakilalamikiwa kwamba ni makubwa mno; kwamba amepewa madaraka ya kuteua wateule wengi kuanzia mawaziri naibu mawaziri, wakuu wa mikoa, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa wilaya, wakuu wa vyombo vya dola, majaji, wakurugenzi na makamishna wa taasisi mbalimbali, wenyeviti wa bodi na wateule wengine.

Wote hao hawathibitishwi na mamlaka nyingine yoyote nchini.

Jambo jingine ambalo limekuwa likilalamikiwa ni matokeo ya uchaguzi wa urais kutohojiwa na chombo chochote, ikiwemo Mahakama.

Ibara ya 41 (7) inasema kuwa iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais, hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka kuchunguza kuchaguliwa kwake.

MAMBO 15 YA KUBAKI KATIKA KATIBA

Hata hivyo, Nape, alisema NEC imetaka mambo 15, ukiwamo muundo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwa wa serikali mbili yabaki au yaingie ndani ya Katiba mpya kwa kuwa ndiyo misingi mikuu ya taifa.

“Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilijadili na kukubaliana kuwa wanachama na wananchi kwa jumla wahakikishe kuwa misingi mikuu ya taifa letu inabaki katika Katiba mpya itakayoandikwa,” alisema Nape.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwa serikali mbili; ambayo ni Serikali Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema muundo wa serikali mbili ndio msingi na sera ya CCM, ambayo haina upungufu.

Misingi mingine mikuu ya taifa aliitaja kuwa ni kuendelea kuwapo kwa mihimili mitatu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuendelea kuwapo kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuendelea kuwapo kwa umoja wa kitaifa, amani, utulivu, usawa na haki.

Alisema CCM haijaona kama ni wakati muafaka wa kuwa na mhimili wanne wa dola ambao ni wa vyombo vya habari, kama ambavyo umekuwa ukitajwa kama mhimili wa dola usio rasmi.

Misingi mingine ni kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalum na kuzingatia haki ya kupiga kura kwa kila mtu mwenye sifa zinazohitajika kwa mujibu wa sheria, kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa haki za binadamu na kuheshimu usawa mbele ya sheria, kuendeleza sera ya dola kutokuwa na dini rasmi, bali inaruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka mwenyewe.

Mingine ni kuendeleza sera ya serikali kuwa ndiye mmiliki wa rasilimali kuu za nchi, hususan ardhi, kuendeleza sera ya kuwapo kwa usimamizi madhubuti wa maadili ya viongozi kwa kuupa nguvu za kikatiba na kuimarisha madaraka ya umma.

Mingine ni kuhamasisha sera ya msingi ya kujitegemea, kusimamia usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine maalum katika jamii, kusimamia hifadhi ya mazingira na kuendelea kuwapo kwa Rais Mtendaji.

Nape alisema baada ya NEC kukubaliana mambo hayo, chama kitaandaa na kupeleka maoni yake kwa Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kwa ajili ya Mabadiliko ya Katiba ya nchi.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles