Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Kavumbagu aahidi makubwa Yanga

6th August 2012
Print
Comments
Mshambuliaji mpya wa klabu ya Yanga kutoka Atletico ya Burundi, Didier Kavumbagu

Mshambuliaji mpya wa klabu ya Yanga kutoka Atletico ya Burundi, Didier Kavumbagu, ameahidi kuifanyia klabu hiyo mambo makubwa wakati wa michuano ya Ligi Kuu Bara itakayoanza Septemba Mosi mwaka huu.

Kavumbagu, ambaye amesaini  mkataba wa miaka miwili kuichezea klabu hiyo, tayari ameanza mazoezi na wachezaji wenzake.

Akizungumza wakati akitambulishwa kwa wanahabari na kukabidhiwa jezi namba 21 ambayo ataitumia akiwa na kikosi cha ‘Wanajangwani, Kavumbagu alisema amekuja Yanga kufanya kazi.

"Nimekuja Yanga kufanya kazi ilionileta, mashabiki wa soka wasubiri kuona kile kilichonileta Yanga," alisema Kavumbagu.

Kavumbagu, ambaye aliifunga Yanga mabao mawili katika mchezo wa fungua dimba wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka huu, anatarajiwa kuendeleza cheche zake katika kuzifumania nyavu za timu pinzani ambazo zitakutana na Yanga katika mashindano ya ligi kuu hapo baadae.

Wakati Didier akitamba kuendeleza cheche zake, uongozi wa Yanga umepanga kumzawadia mchezaji Said Bahanunzi kutokana na mchango mkubwa aliotoa katika michuano hiyo na kuibuka mfungaji bora.

Ofisa habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu, alisema uongozi wa klabu yake umepanga kumpa zawadi mchezaji kama changamoto ya kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mengine yakiwamo ya ligi kuu.

Mbali na Bahanunzi, uongozi huo unatarajia kutoa zawadi kwa timu nzima ambayo ilionesha ushirikiano wakati wa mashindano hayo yaliyofikia ukingoni kwa Yanga kuchukua ubingwa baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-0.

Yanga ambao ni mabingwa wa kombe la Kagame, walisafiri jana mchana kuelekea Bungeni mjini Dodoma baada ya kupata mwaliko kutoka kwa wabunge ambao ni wapenzi wa Yanga kutokana na kile walichokifanya katika mashindano ya mwaka huu ya kombe la Kagame.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment