


.jpg)
Baada ya timu yao kupokea kichapo cha magoli 5-0 kutoka kwa watani, Simba, Wazee wa Klabu ya Yanga, wamemtaka Mwenyekiti wa klabu yao, Lloyd Nchunga, kujiuzulu nafasi hiyo haraka.
Hata hivyo, Nchunga tangu juzi amekuwa hapokei simu yake ya mkononi na kuzungumza hali ilivyo kwenye klabu hiyo na badala yake amekuwa akichagua vyombo vya habari.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake, katibu wa kundi hilo, Ibrahim Akilimali, alisema kuwa mbali na kumtaka Nchunga ajiuzulu nafasi hiyo pia wamemtaka asithibutu kuwatimua wachezaji wa timu hiyo kwa madai kwamba waliihujumu timu katika mechi yao dhidi ya Simba iliyofanyika Jumapili iliyopita.
Akilimali alisema kuwa ilionekana mapema kuwa Nchunga hana uwezo wa kuiongoza Yanga kuelekea mechi hiyo yenye ushindani na hicho ndicho kilichosababisha wao kutaka kuisimamia timu na kuhakikisha wachezaji wanalipwa malimbikizo ya posho na madai ya fedha za usajili ambayo yalikuwa hayajakamilishwa tangu mwanzo wa msimu huo wa ligi.
"Nchunga asikwepe majukumu na kuwatupia lawama wachezaji, aangalie alipojikwaa, asilaumu alipoangukia, kila siku tunatakiwa tukumbuke shina, wazee ni dawa," alisema Akilimali.
Aliongeza kuwa ilikuwa ni vigumu timu yao kushinda mechi hiyo wakati wachezaji hawakuwa na ari na kipigo hicho walichopata Yanga si ya kwanza kwa sababu pia hivi karibuni timu ya Manchester United na Arsenal (zote za Uingereza) zimeshakumbana na vipigo vya aina hiyo lakini wachezaji hawakutuhumiwa kuhujumu timu, hivyo Nchunga asiwaangusie lawama wachezaji.
Alisema kuwa maamuzi ya kutaka kufukuza wachezaji ndio yataongeza mpasuko ndani ya timu yao kama ilivyotokea miaka ya nyuma.
Aliwashukuru wanachama wa timu hiyo waliojitokeza kuokoa jahazi baada ya wachezaji kutishia kugomea mechi hiyo Jumapili, ambao wanadaiwa kuwa waliwapatia wachezaji Sh. 300,000 kila mmoja.
Naye Bakili Makele, alisema kuwa Nchunga ndio msaliti na alijua Yanga itapoteza mechi hiyo ndio maana akakataa ushauri aliopewa wa kuikabidhi timu kwa wazee.
Makele alisema pia inaonyesha wazi kwamba Nchunga ameelemewa hivyo ni vyema akakaa pembeni na kuwapisha wengine waendelee kuiongoza Yanga.
Pia alisema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) 'linawabeba' viongozi hao walioko madarakani kwa kukiuka katiba ambapo tangu wachaguliwe hawajawahi kuitisha mkutano mkuu wa wanachama na vile vile wakishindwa kuwachukulia hatua wanachama wenzao waliofungua kesi mahakamani kuzuia kufanyika kwa mkutano.
"Tumechoka sasa. Kwa nia nzuri tunamuomba aondoke, Nchunga anavuruga katiba, tunaiomba TFF ituondolee mtu huyu kwa sababu haitendei haki klabu yetu," aliongeza Bakili.
Wazee hao pia walitishia kwenda kuvamia klabu yao wakimaanisha kwamba watafanya mapinduzi jambo ambalo kwa sasa halikubaliwi na TFF.