Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ngasa ajifunga Simba miaka miwili

4th August 2012
Print
Comments
Mrisho Ngasa

Winga Mrisho Ngasa ambaye aliifanyia vituko Azam FC akilazimisha kuuzwa Yanga jana alitambulishwa rasmi na Simba ambayo imempa mkataba wa miaka miwili wa kuwachezea mabingwa wa ligi kuu ya Bara hao wa msimu uliopita.

Ngasa alibusu nembo iliyo katika jezi ya Yanga na kuivaa juu ya sare ya Azam katika mchezo wa Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika mashariki na kati mwezi uliopita katika kilichoonekana kama moja ya jitihada za kulazimisha timu hiyo imuuze kwa mabingwa hao.

Lakini tofauti na matarajio yake, Azam ilitangaza tenda na ni Simba pekee iliyojitokeza ikiwa na sh. milioni 25 za kumnunua kwa mkopo.

Ngasa aligoma kwenda Simba, awali, akipinga kuuzwa kama "nyanya" kabla ya kubadli mawazo juzi na sasa atavaa jezi nyekundu, badala ya kijani, mpaka mwaka 2014.

Utambulisho wa mchezaji huyo aliyekebidhiwa jezi namba 16 ulifanyika jana klabuni Mtaa wa Msimbazi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey 'Kaburu', alisema "Ngasa ataichezea kwa mkopo kwa mwaka mmoja uliobakia kwenye mkataba wake na Azam."

Kisha ataanza kuitumikia tena Simba kwa mkataba wa mwaka mmoja, alisema.

Aidha, alisema Simba inaamini mchezaji huyo atatoa mchango wa kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri kwa kuwa ana uwezo unaofahamika ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Ngasa, alisema ameamua kujiunga na Simba kwa kuwa ni timu kubwa na kuahidi kuisaidia kufanya vizuri.

"Nitashirikiana na wachezaji wenzangu kuhakikisha Simba inafanya vizuri kwenye ligi pamoja na mashindano ya kimataifa... naomba wanachama na wapenzi wa Simba watusapoti ili tufanye vizuri," alisema Ngasa.

Mchezaji huyo ambaye alikaririwa wiki hii akisema anaiheshimu sana Yanga kwasababu ametoka nayo mbali, atatambulishwa kwa wanachama na mashabiki wa Msimbazi kwenye siku kuu ya Nane Nane ya maadhimisho ya Simba Day.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment