Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ajenda ya gamba kitendawili Nec

10th May 2012
Print
Comments
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekataa kuthibitisha kama miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) mwishoni mwa wiki, ni utekelezaji wa azimio la kikao kilichopita la kuvuana magamba.  

Kikao cha Nec kilichopita kilichofanyika mwishoni mwa Novemba mwaka jana, kiliagiza kamati za usalama na maadili ngazi zote kupokea na kushughulikia malalamiko na ushahidi dhidi ya tuhuma za uvunjaji wa maadili miongoni mwa wanachama na viongozi wa chama. 

Alipoulizwa kama suala hilo la utekelezaji wa kujivua gamba litakuwa moja ya ajenda katika kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kitakavyofanyika Jumamosi wiki hii na kufuatiwa na vikao vya Kamati Kuu (CC) na Nec, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alikataa kuthibitisha.

“Nyie (waandishi wa habari) mmeniuliza pale (kwenye mkutano wa waandishi) kuhusu ajenda ambazo zitajadiliwa katika vikao nikawatajia, sasa hayo mnayoyatafuta ni ya kwenu,” alisema Nape juzi akionyesha kutofurahishwa na swali hilo.

Akizungumzia kuhusiana na maazimio yaliyofikiwa baada ya kumalizika kwa vikao vya CC na Nec Novemba mwaka jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, alisema Nec iliagiza CC na kamati za siasa za ngazi zote za chama hicho kuanza mara moja mchakato huo.
 
“Halmashauri Kuu ya Taifa imeiagiza Kamati Kuu, pamoja na kamati za siasa za ngazi zote za chama chetu kupitia kamati ya usalama na maadili za ngazi zao zianze mara moja mchakato wa kutekeleza azimio hilo la kufanya mageuzi ndani ya chama,” alisema Mukama.

Akisoma maazimio hayo yaliyopewa kichwa cha habari cha utekelezaji wa maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu viongozi wanaotuhumiwa, Mukama alisema, Nec imezitaka ngazi hizo za uongozi kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni, taratibu zinazohusika za chama hicho.
 
“Vile vile zoezi hilo lifanyike bila kuchelewa. Baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, taarifa zipelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya maamuzi vya ngazi zinazohusika kwa hatua za utekelezaji,” alisema Mukama aliyeongozana na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Pius Msekwa na Nnauye.

Kuhusu mwitikio, Mukama, alisema hadi sasa takribani miezi saba baada ya azimio hilo kupitishwa, bado halijapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote ya CCM ambao ni walengwa wa azimio hilo.

Alisema bila shaka wakati sasa umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika.

“Lakini utekelezaji wake utafanyika vipi ili haki ionekane kuwa imetendeka? Jibu ni kwamba utekelezaji huo hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za Uongozi na Maadili,” alisema.

Alisema kanuni hizo zinaelekeza hatua zinazopaswa kufuatwa katika kudhibiti viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia wahusika nafasi ya kutoa utetezi wao.

Katika kikao cha Nec kilichofanyika Aprili mwaka jana, kiliazimia jumla ya mazimio 27 ambayo yalilenga katika kukiimarisha chama hicho kwa kukipa sura mpya itakayokuwa na mvuto zaidi kwa wanachama na pia kwa wananchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Mukama, Sektarieti ya Nec imekwisha kutengeneza mpango wa utekelezaji wa maamuzi hayo yaliyopewa jina la kujivua gamba na mpango huo umekwisha kuidhinishwa na Nec.

Katika kikao hicho cha Aprili mwaka jana, Nec iliazimia viongozi wote wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime wenyewe na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama na wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe bila kuchelewa.

Miongoni mwa waliokuwa walengwa wa ajenda hiyo ni Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa. Lowassa aliguswa na kashfa ya kuipa mkataba kwa njia ya upendeleo kampuni hewa ya Richmond ya Marekani ya kufua umeme wa dharura.

Wengine ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Chenge ambaye pia ni mjumbe wa Nec alikuwa anatuhumiwa kwa kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi kwa gharama ya juu ambayo Tanzania iliuziwa na Uingereza wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Rostam Azizi ambaye pia alikuwa mjumbe wa Nec, alikuwa akituhumiwa kutumia kampuni hewa ya Kagoda Agriculture Limited kuchota Sh. bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na mahusiano yake na kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans Tanzania Limited.

Hata hivyo, hadi sasa ni Rostam Aziz aliyetekeleza azimio hilo baada ya kutangaza kujiuzuku nyadhifa zake zote Julai 13, mwaka 2011, akidai kuwa amechoshwa na siasa uchwara ndani ya CCM pamoja na fitina.

Chenge amekwisha kusema mara kadhaa kwamba yeye si gamba, na kwamba hana lolote baya alilofanya katika ununuzi wa rada na hata fedha zake zilizokutwa katika akaunti visiwa vya Jersey hazina uhusiano wowote na rada hiyo.

 Alijitetea kuwa fedha hizo ni akiba ya familia yake inayotokana na kazi zake za uwakili.

Lowassa alizungumza katika Nec iliyopita akilaumu kuchafuliwa na viongozi wa CCM kwa kutumia fedha za chama ilhali ikijulikana wazi kuwa maamuzi yote ya mkataba wa Richmond mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete alikuwa anajua.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles